27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UN yaishutumu tena Sudan Kusini

Lul Ruai Koang
Lul Ruai Koang

JUBA, Sudani Kusini

WARAKA uliotolewa katikati ya wiki hii na Umoja wa Mataifa (UN), umeishutumu Serikali ya Sudan Kusini kuwapa mafunzo ya kijeshi watoto wadogo wiki iliyopita, ikiwa ni hatua ya kujitayarisha kwa mapigano mapya dhidi ya waasi nchini humo.

Waraka huo ambao umechapishwa na Shirika la Habari la Associated Press, umetanabaisha kwamba mwanasiasa mmoja wa ngazi za juu ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais Salva Kiir, ndiye aliyeongoza mafunzo hayo ya kijeshi kwa wavulana wa kijiji kizima.

Kwa mujibu wa DW, waraka huo umedai kuwa mwanasiasa huyo alitumia vitisho kwa vijana waliokataa kupatiwa mafunzo ambapo miongoni mwao wamo watoto wa miaka 12.

Hata hivyo, madai ya waraka huo yamekanushwa vikali na msemaji wa Jeshi la Serikali, Lul Ruai Koang ambaye alisema vijana wote wanaojiunga na jeshi la nchi hiyo huwa hawalazimishwi.

Waraka huo umekwenda mbali kwa kudai kuwa tabia ya Serikali ya nchi hiyo kuingiza watoto jeshini imeanza muda mfupi baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), kupitisha azimio la kutuma wanajeshi wengine 4,000 wa kulinda amani katika taifa hilo.

UN imesema ndani ya mwaka huu watoto 650 wamejiunga na makundi yenye silaha nchini humo na idadi hiyo  iwekwe kwenye majumuisho ya jumla tangu mwaka 2013 ambapo jumla ya watoto 16,000 wameingizwa kwenye makundi mbalimbali ya wapiganaji.

Wakati hayo yakijiri, taarifa mpya nchini humo zinadai kuwa UN imekiri wazi ushiriki wake wa kumsafirisha Kiongozi wa chama cha SPLM, Riek Machar, ambaye amekimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa UN, Farhan Haq, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja huo nchini Kongo (Monusco), kilihusika na operesheni hiyo kwa idhini na mashirikiano ya Serikali ya Kongo.

“Tunaweza kuthibitisha kwamba operesheni hiyo ilifanywa na Monusco kwa misingi ya kibinadamu ili kuwezesha kumsafirisha Riek Machar, mkewe na wengine kumi kutoka eneo fulani nchini Sudan kwa msaada wa mamlaka za Kongo. Na kama ambavyo nimesema, ameshakabidhishwa kwa mamlaka za Kongo na yuko nao sasa,” alisema Haq.

Juzi Chama cha Machar kilithibitisha kwamba kiongozi wao huyo ametoroka nchi hiyo kwa sababu za kiusalama.

Machar, ambaye alirejea kwenye nafasi yake ya umakamu wa rais chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2015, alilazimika kuondoka mjini Juba akiambatana na wanajeshi wake mwezi uliopita, baada ya kuzuka upya kwa mapigano kati ya vikosi vyake na vile vya Rais Kiir.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles