23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo wanane NIDA kortini Dar

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu (kulia) na maofisa wenzake wa Mamlaka hiyo wakiwa katika kizimba cha Mahakama ya haklimu Mkaazi Kisutu wakisubili kusomewa mashtaka yao ya uhujumu uchumi.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu (kulia) na maofisa wenzake wa Mamlaka hiyo wakiwa katika kizimba cha Mahakama ya haklimu Mkaazi Kisutu wakisubili kusomewa mashtaka yao ya uhujumu uchumi.

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilifurika watu huku vilio vikitawala wakati aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake saba, walipofikishwa kizimbani kwa mashtaka 27 ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.16.

Ndugu na jamaa waliofurika   katika mahakama hiyo waliangua kilio walipowaona washtakiwa wakiingizwa mahabusu wakitokea polisi walikolala tangu juzi, na vilio viliongezeka baadaye walipoamuriwa kurudi gerezani.

Washtakiwa walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi , Respicious Mwijage, wakikabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.

Hakimu Mwijage, kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka, aliwafahamisha kwamba mashtaka yanayowakabili yako chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi hivyo hawataruhusiwa kujibu kwa vile  Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo iliyofikishwa mahakamani na  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni Meneja Biashara,  Avelin Momburi,  Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji,  George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa akishirikiana na mawakili kutoka TAKUKURU, Janeth Machulya, Leonard Swai, Joseph Kiula na Fatuma Waziri waliwasomea washtakiwa hao mashtaka yanayowakabili.

Mbagwa alidai shtaka la kwanza linamkabili Maimu na Mwakatumbula ambao wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15 hadi 19,  mwaka 2010 katika makao makuu ya NIDA   wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo    walitumia madaraka  vibaya.

Alidai waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na  Benki Kuu ya Tanzania,    kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

Mshtakiwa Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani milioni 1.8, bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili  wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya Dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh milioni sita kwa GIL bila ya kupiga  hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 14, 661,676.76.

Mbagwa alidai Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya NIDA kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya Dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia NIDA kupata hasara ya Sh 167,445,676.76.

Mshtakiwa Ndege anakabiliwa na mashtaka ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri.

Anadaiwa Aprili 16, 2012 katika makao makuu ya NIDA akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Broker ambayo imeingia mkataba na NIDA wa kutoa huduma za bima, kwa nia ya udanganyifu.

Ilidaiwa kuwa Ndege aliwasilisha hati ya malipo yenye taarifa za uongo NIDA akionyesha kwamba kampuni yake inastahili kulipwa Sh 22,582,281 kwa huduma za bima iliyoitoa huku akijua taarifa hizo za uongo na zilikuwa na lengo la kumdanganya mwajiri wake.

Mshtakiwa Momburi, Mwakatumbula na Ntalima wanadaiwa kati ya Februari 22 na Aprili 17, 2012 katika makao makuu hayo walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo ya Sh 22,582,281 kwa Kampuni ya Aste Insurance Brokers hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya kiasi hicho.

Maimu, Mwakatumbula na Ntalima pia wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka wakidaiwa kupitisha malipo ya bima kwa kampuni ya Aste hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya viwango mbalimbali vya fedha.

Mkurugenzi huyo wa NIDA, Mwakatumbula, Ndege na Ntalimwa wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Januari 4,2013 katika makao makuu ya NIDA waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh 55,312,800.

Katika mashtaka mengine, Maimu, Mwakatumbula na Makani wanadaiwa kati ya Januari 29 na 30, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Dola za Marekani milioni mbili kwa IRS Corporation Berhad.

Ilidaiwa kuwa mapendekezo ya utaratibu mpya wa haraka wa upatikanaji wa vitambulisho na vifaa bila ya kufanya marekebisho ya mkataba ulioko kati ya NIDA na kampuni uliiwezesha  IRIS kupata faida ya fedha hizo.

Pia washtakiwa hao Maimu, Mwakatumbula na Makani wanadaiwa kupitisha malipo kwa kampuni hiyo ya IRIS ya viwango mbalimbali hivyo kuifanya ipate faida.

Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni mosi na 6, 2013 katika makao makuu hayo kwa pamoja walikula njama za kutenda kosa la kutumia nyaraka za uongo kwa nia ya kumdanganya mwajiri.

Washtakiwa Mwakatumbula, Ntalima na Kayombo wanadaiwa kati ya Juni 4 na 6,2013 katika makao makuu hayo waliisababishia hasara NIDA ya Sh 45,515,961.

Wakili Swai alidai katika mashtaka mengine kuwa Maimu na Sabina wanadaiwa kati ya Agosti 3, 2010 na Novemba 7, 2011 katika makao makuu ya NIDA wakati wakitekeleza majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya na kuiwezesha GIL kupata faida ya Sh 901,078, 494 na kuisababishia NIDA kupata hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Baada ya mawakili kumaliza kusoma mashtaka, Wakili Mbagwa alidai kati ya washtakiwa wanane, mshtakiwa Momburi na Makani wanadaiwa kusababisha hasara waliyosababisha haizidi Sh milioni 10 lakini alipinga kupewa dhamana kwa sababu mashtaka yako chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Wakili wa washtakiwa hao, Johnson Jamhuri alipinga hoja hizo kwa madai kwamba mashtaka yanayowakabili wateja wake yanadhaminika na siyo ya kuhujumu uchumi.

Hakimu Mwijage baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili aliahidi kutoa uamuzi kesho kwa ajili ya mshtakiwa wa pili na wanne lakini washtakiwa wote kesi yao itatajwa Agosti 31 mwaka huu.

Januari 25, mwaka huu, Rais Dk.John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu  kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali.

Mbali na Maimu, maofisa wengine wanne wa NIDA nao walisimamishwa kazi   kupisha uchunguzi wa jinsi Sh bilioni 180 zilivyotumiwa na mamlaka hiyo wakati wananchi waliopatiwa Vitambulisho vya Taifa wakiwa ni wachache.

Maofisa hao waliokuwa wamesimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.

Akitoa taarifa ya kutenguliwa kwa maofisa hao, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Balozi Ombeni Sefue, alisema kiasi cha fedha zilizotumiwa na NIDA ni kikubwa na kwamba Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi zilivyotumika.

Alisema hiyo ni kutokana na kuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kuna kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho vya taifa vilivyokuwa vikitengenezwa na mamlaka hiyo.

Machi 6, mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba alitangaza kuvunja mikataba ya wafanyakazi 597.

Dk. Kipilimba alisema hatua hiyo ilifikiwa kutokana na ufinyu wa bajeti  na nia ya mamlaka hiyo ya kutaka kuongeza ufanisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles