24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Donald Trump ni kirusi kilichotumwa kuisambaratisha Republican?

Donald Trump, Hillary Clinton, Bill Clinton na Melanie Trump wakati wa harusi ya bilionea huyo na mkewe Melanie mwaka 2005.
Donald Trump, Hillary Clinton, Bill Clinton na Melanie Trump wakati wa harusi ya bilionea huyo na mkewe Melanie mwaka 2005.

NA JOSEPH HIZA,

WAKATI jinamizi baya la David Moyes katika kuiongoza Klabu ya Manchester United lilipohitimishwa, bango lilionekana uwanja wa Anfield, nyumbani kwa wapinzani wao, Liverpool, likisomeka ‘Wakala Moyes: Kazi uliyotumwa imetimia.

Ni nadharia ya hila, ambayo ilimaanisha kuwa njia ya pekee ya kukibomoa kikosi imara kilichojengwa na Sir Alex Ferguson, meneja aliyeifundisha United kwa mafanikio ilikuwa kupitia ndani.

Kwamba Moyes, akiwa ametumwa, alikibomoa kikosi hicho bila United yenyewe kujua, yaani kwa staili ya ‘Kikulacho kinguoni mwako!

Baadhi ya wanachama wa chama cha Republican nchini Marekani wanamshuku Donald Trump, mgombea urais wa chama kwa bango kama hilo.

Ni aina ya nadharia kinzani, ambazo zinapewa uzito au kuhusudiwa na baadhi ya raia wa taifa hilo, yanapokuja masuala mbalimbali hasa yanayoacha mwanya wa utata.

Ni nadharia, ambazo vigogo wengi huziogopa kiasi cha kuwa makini kutofanya makosa yatakayozipa nafasi kushamiri kwa vile zinapoandaliwa vyema huwaaminisha wengi na kuondoa ukweli au uhalisia wa jambo.

Ni sawa na namna baadhi ya wataalamu mahiri wa propaganda wanavyoweza kugeuza ukweli kuwa uongo na uongo kuwa ukweli.

Moja ya nadharia hizi za njama kinzani zilizowahi kuzikosesha usingizi mamlaka za Marekani kiasi cha kujikuta zikipoteza muda kuzijibu ni; je, Marekani ilituma binadamu wa kwanza mwenzini ile Julai 20, 1969?.

Wakati rekodi hiyo ya kutua mwezini ikionekana wazi, wana nadharia hao wanapinga wakieleza kwa kutumia mifano hai, kwanini jambo hilo halikutokea na kwamba Marekani iliongopa.

Kwa namna ile ile ambayo, Moyes amehusishwa na njama dhidi ya United, Trump naye baadhi ya wana Republican wanamhesabu kuwa kirusi kilichotumwa na Democratic kumsafishia njia mgombea wake wa urais Hillary Clinton.

Ndiyo bilionea huyo humshambulia sana Clinton na utawala wa Democratic chini ya Rais Barack Obama, akiwaita kila aina ya majina mabaya ikiwamo jambazi, mwizi, gaidi, shetani na kadhalika.

Lakini hilo halikutosha bado kuwafanya baadhi ya wana-Republican kumuamini udhati wake.

Huku wakitaka atoswe na chama hicho, wamebakia kuamini kuwa kampeni yake nzima hailengi kuingia Ikulu ya Marekani bali kumsafishia njia Clinton.

Wanaamini kama ilivyo kwa wengi, Clinton, si mgombea anayeaminika kwa wapiga kura wengi mbele ya wanachama wake akiwamo Trump mwenyewe.

Naam, kwamba Trump ana kila sababu ya kumshinda Clinton katika uchaguzi wa urais wa Novemba 8, kwa vile mpinzani wake huyo amepoteza mvuto na umaarufu.

Kwamba kitendo cha kuonekana akishindwa kummudu Clinton kama kura mbalimbali za maoni zinazoendelea kuonesha, akiachwa kwa tofauti ya 8-10, inadhihirisha njama zake hizo.

Kwamba anatoa matamshi ya chuki na kibaguzi yanayomfanya apoteze imani ya Wamarekani wengi kwa makusudi ya kufanikisha njama za kumwingiza Clinton katika Jumba Jeupe.

Wanaamini kauli za kumshambulia Clinton ni danganya toto zenye lengo la kuwapumbaza Republican, kwa vile hazimsaidii yeye wala chama hicho bali kumrahisishia mke huyo wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton.

Ni sehemu ya nadharia za hila zilizozingira kampeni ya mfanyabiashara huyo wa New York.

Na haishangazi kwamba nadharia hizi hutokea wakati watu wanapojaribu kuzifanya zionekane kuwa kweli katika matukio ambayo si ya kawaida, au ambayo yameacha maswali.

Na ndivyo ilivyo kwa ugombea wa Trump, ambaye kuibuka kwake si kwa kawaida na pia hakukutarajiwa.

Nadharia kuwa Trump ni silaha ya maangamizi iliyotumwa na Democrat kuibomoa Republican iliwahi kuelezwa wazi Desemba mwaka jana.

Haikuelezwa na mtu mwingine zaidi ya aliyekuwa mmoja wa wapinzani wake wakati wa kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kuiwakilisha Republican katika uchaguzi wa urais; Jeb Bush.

Mdogo huyo wa Rais wa 43 wa Marekani George W Bush na mtoto wa Rais wa 41 wa taifa hilo, George H. Bush aliandika: “inawezekana Donald ana makubaliano na mshikaji wake Hillary Clinton. Kumsafishia njia yake ya kuelekea Ikulu.

Je, inaweza kuwa kweli? Wana nadharia ya hila wana hili la kuamini, Trump aliwahi kuwa mwanachama wa Democrat.

Aliwahi kumchangia Clinton wakati akipambana na Rais Barack Obama kuwania uteuzi wa ndani ya Democratic mwaka 2008.

Na zaidi ana mtazamo wa karibu wa sera na imani za Democratic kuliko za chama chake cha Republican.

Na zaidi alikuwa rafiki wa familia ya akina Clinton.

Familia hiyo ilihudhuria harusi yake na mkewe wa sasa Melanie mwaka 2005.

Na aliwasifu akina Clinton hasa Hillary, akimwita ‘mwanamke wa aina yake.’

Aidha binti za familia hizo mbili; Ivanka Trump and Chelsea Clinton ni marafiki wakubwa hadi leo hii.

Kwa waumini wa nadharia kinzani ndani ya chama hicho akiwamo Justin Raimond anayejiita mhafidhina wa jadi mwenye mwelekeo wa kiliberali;

Matamko ya ovyo ya Trump, ‘ubaguzi wa wazi wazi, utumiaji hisia na uchonganishi vinaonekana kama vitu vilivyopikwa na Democratic kisha kumtumia mamluki kuvipenyeza kutokea Republican kwa lengo la kukibomoa machoni mwa wapiga kura.

Imani nyingine inayowaaminisha wananadharia hao ni kwamba kwa kawaida wakuja wa kisiasa kwa kawaida hupuuzwa na vyombo vya habari, hali ambao ni tofauti kwa Trump, ambaye hana historia ya kisiasa.

Bilionea huyo kila anapozungumza hata ndani ya kuta, mitandao ya habari hutoa uzito mkubwa habari zake.

Na hilo, lina mchango wake katika kumfikisha Trump hapo alipo.

Tofauti na wenzake, Trump alishinda uteuzi kwa sababu tofauti na wagombea wengine wa Republican, yeye alichochea hofu na mashaka kwa tabaka la wafanyakazi wa Marekani na hivyo kuwa msemaji wao.

Alifahamu fika nini walihofia: kukosekana muimariko wa uchumi; wasiwasi wa uhamiaji; na kwamba dunia yao inabadilika kwa kasi bila uwapo wa breki wa kuzuia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles