24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbuzi wa ajabu anavyohusishwa na ushirikina

MBUZI WA AJABUNa Upendo Mosha, Kilimanjaro

ILIKUWA ni kama sinema katika Kijiji cha Kimangaro kilichoko Kata ya Mwika Kusini, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, pale ambapo kiumbe chenye umbile la ajabu kilipozaliwa na mbuzi.

Mbuzi huyo ambaye ni mali ya Simon Ngowo, alikufa akiwa na mimba na baada ya kupasuliwa ili kuangalia kilichopo ndani ya tumbo ndipo alipokutwa kiumbe huyo wa ajabu.

Hakika suala hilo lilishangaza wengi na kuvuta umati mkubwa kushuhudia kiumbe huyo baada ya taarifa kuenezwa kuwa anafanana na binadamu.

Kama ilivyo ada, kila mmoja aliyeshuhudia tukio hilo aliweza kuoanisha kila kiungo katika mwili wa kiumbe huyo na baadhi ya viongo vya wanyama wengine wakiwamo binadamu na nguruwe.

Kwa kuwa ni jambo linalogusa hisia za kila mtu aliyeshuhudia ama kusikia ilinilazimu kufuatilia kwa kina ili kujua kama hali hiyo ilishawahi kujitokeza.

Watu wengi kwa mawazo yao ya haraka haraka walikimbilia kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina.

Safari ya kuelekea katika Kijiji cha Kimangaro ilianza huku nikiwa na maswali mengi yasiyo na majibu.

Nilipofika nilipokewa na Kelvin Ngowo, ambaye ni mtoto katika familia hiyo, anaeleza jinsi tukio lilivyotokea huku naye akionyesha kutojua hasa ni nini kilichochangia jambo hilo kujitokeza kwa mbuzi huyo.

“Mbuzi alipokufa tulimpasua na huyo kiumbe hapo (akimwonyesha mwandishi) ndiye tulimkuta,” anasema Ngowo.

Anasema siku mbili kabla ya mbuzi huyo kufa na kupasuliwa, alionekana kuwa na tatizo na ndipo walipoamua kumuita daktari wa mifugo ili kumtibu.

“Baada ya daktari kuja alimpima na kumchoma sindano mbili na baada ya siku mbili aliaza kuvimba mwili hatimaye kufariki dunia akiwa na kiumbe chake tumboni,” anasema.

Anasema baada ya mbuzi huyo kufa, familia hiyo iliamua kumpasua na kukuta kiumbe hicho cha ajabu ambacho kiliwashtua watu wengi katika kijiji hicho na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

Akizungumzia mwonekano wa mwili wa mbuzi huyo, baada kutolewa ndani ya tumbo la mama yake, anasema alikuwa na miguu iliyofanana na ya nguruwe, mikono, kichwa kilichokuwa na masikio na mfano wa pua ya binadamu pamoja na mdomo.

Anasema mara baada ya kukutwa kwa kiumbe hicho, aliamua kwenda kumuita daktari aliyemtibu na alipofika aliwaondoa hofu na kuwaeleza kuwa hilo jambo ni la kawaida.

“Daktari alisema ni jambo la kawaida lakini mimi na familia yetu hatukuridhika kwa sababu hatukuwahi kuliona na hasa ikizingatiwa kwamba uzao wa mbuzi huyo ni wa pili.

“Ndipo tulipoamua kuwaita majirani kuja kushuhudia ambapo pia walishtushwa na kiumbe hicho cha ajabu,” anasema.

 

MTAALAMU WA MIFUGO

Daktari wa Mifugo, Leonard Lyimo, anasema mbuzi huyo si wa ajabu kama watu wengi walivyodhani na kwamba ni tatizo la kawaida ambalo hutokea kwa wanyama.

“Kweli mbuzi yuye alizaa kiumbe wa ajabu lakini jambo hilo si la kushangaza kama lilivyochukuliwa na watu wengi, ni la kawaida ingawa hutokea kwa nadra sana.

“Tatizo la mbuzi huyo kitaalamu hujulikana kama hitilafu ya kimaumbile na kilichotokea ni kwa sababu alikuwa amejaa maji maeneo ya kifuani, usoni, tumboni na miguuni, ndio maana mwonekano wake ukawa tofauti,” anasema Lyimo.

Anasema tukio hilo si la kushangaza kwani hata binadamu huweza kuzaa kiumbe cha tofauti na kwamba kwa mifugo huweza kutokea kwa mbuzi mmoja kati ya mbuzi milioni moja.

 

OFISA MTENDAJI

Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Ester Ngonyani, anasema alipofika katika eneo la tukio alikuta mbuzi huyo ameshachinjwa na walisimamia kuhakikisha haliwi kwa sababu haikujulikana alikufa kwa tatizo gani.

“Tukio la aina hii halijawahi kutokea tangu nimeanza kazi ila wataalamu wa mifugo walisema ni la kawaida na kuwataka waondoe hofu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida,” anasema Ngonyani.

 

WANANCHI

Baadhi ya wananchi wanaeleza tukio hilo kuwa ni la aina yake na halijawahi kutokea katika eneo hilo.

Asanteeli Mongi (89) anasema; “Tangu nikiwa mdogo hapa kijijini sikuwahi kuona kiumbe cha namna hii hivyo nimeshtuka sana. Sijui limesababishwa na nini na ingekuwa ni huko kwa wenzetu tungeweza kusema ni kuoneana wivu.

Kwa mujibu wa Mongi, kama ingekuwa ni miaka ya nyuma ni lazima wangekutana wazee wa eneo hilo ili kufanya tambiko.

“Kama tukio hili lingetokea miaka ya nyuma lazima wazee tungetafutana na kuiuliza mizimu limekuwaje jambo hilo litokee na lina maana gani kwa jamii hiyo,” anasema Mongi.

 

Mary Urio (47), anahusisha tukio hilo na imani za kishirikina na kudai kuwa wako watu ambao hawataki kuona mbuzi wa mzee huyo wakizaana na kuongezeka.

Mama huyo anasema watu wengine hawapendi kuona maendeleo ya wenzao na hivyo kutumia kila njia kuwakwamisha kwa njia wanazozijua wao.

“Unajua kuna watu wana wivu wa ajabu we hushangai hapa kijijini kwetu mtu unaweza akawa na ng’ombe na akazaa lakini maziwa hakuna na hujui yanaenda wapi, yaani unakuwa mtu wa kufuga tu na kufagia samadi,” anasema Urio.

Givos Msaki (22) anasema awali alidhani kwamba mbuzi huyo alikula mfuko wa nailoni kwa sababu mifuko hiyo hufunga tumbo la mnyama.

“Mimi nashauri wataalamu waendelee kulichunguza suala hilo kwa sababu tumezoea kuona mbuzi wanaopata matatizo makubwa au ng’ombe ni wale wanaokula mifuko ya nailoni,” anasema Msaki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles