23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kilio chatawala uchimbaji madini ya Tanzanite

Tanzanite (1)Na ELIYA MBONEA

-SIMANJIRO

UTAJIRI mkubwa wa madini ya Vito aina ya Tanzanite yanayochimbwa katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, umeendelea kutoakisi maisha ya wananchi wake, hasa katika miundombinu na huduma za kijamii.

Tangu kuanza uchimbaji wa madini ya Tanzanite katika maeneo ya milimani iliyopo miji mdogo ya Mirerani, maeneo ya KIA,Osunyai, Mbuguni na mengineyo, wananchi wake wameendelea kukabiliwa na umaskini wa wa hali ya juu japokuwa wamezungukwa na utajiri.

Kutokana na kukabiliwa na matatizo hayo ya umaskini kwa miaka kadhaa, halmashauri ya wilaya hiyo imeamua kuanzisha mnada wa madini hayo ya vito utakaowezesha kuongeza pato la ushuru kwa ajili ya kusaidia huduma za kijamii.

Akizungumza hivi karibuni kwenye Baraza la Madiwani wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yefred Myenzi, alisema uimarishaji wa ukusanyaji wa mapato ni sehemu ya agizo la kitaifa linalolenga kusogeza huduma za kijamii karibu na watu.

Myenzi alisema inasikitisha kuona utajiri mkubwa wa rasilimali za madini ya Tanzanite yanayopatikana wilayani Simanjiro ukiwa hauakisi kabisa maisha ya wananchi wanaoishi kwenye wilaya hiyo.

“Hii ni hatari, Tanzanite hii inayochimbwa wilayani humu haiakisi kabisa maisha ya watu wetu hapa, miundombinu nayo haifanani na utajiri tulionao. Ukiangalia kwenye elimu, afya, maji na umeme, huduma za kifedha na mawasiliano, hatuna tofauti na ambao hawana rasilimali hii,” alisema Myenzi.

“Wenzetu waliotangulia wamefanya walichoweza kwa nafasi zao nasi tumepewa fursa hii tuitumie kuandika historia na tuache urithi usiofutika,” alisema.

Akizungumzia kuhusu wigo wa eneo la kijiografia la wilaya hiyo, alisema haliwiani na idadi ya wataalamu wa halmashauri kukusanya mapato huku ukwepaji kodi unaohusisha ukosefu wa uadilifu wa watumishi, wafanyabiashara na wananchi ukionekana kutawala zaidi.

“Msukumo wa Mbunge, James ole Millya, unahitajika sana katika kubadili sheria ili kuwezesha ushuru kuongezeka kwani bila hivyo hawa walipa kodi wakubwa hasa wenye migodi wataendelea kukwepa,” alisema Myenzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck, alionyesha kuwapo kwa matarajio makubwa na Mkurugenzi Myenzi na hivyo aliahidi kutoa ushirikiano zaidi kwa masilahi  ya umma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles