25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wakurugenzi watakaodanganya kung’olewa

WAZIRI-Mkuu-Kassim-MajaliwaNa Mwandishi Wetu, Morogoro

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa,  amesema Serikali haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao wakurugenzi wote watakaoshiriki katika kutoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Hayo aliyasema juzi mkoani Morogoro  wakati akipokea taarifa ya mkoa huo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo  kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi umekamilika wakati haujajengwa, hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema Majaliwa

Kutokana na hali hiyo alitumia fursa hiyo kuwataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea miradi yote inayojengwa katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alisema Serikali haihitaji halmashauri kutoa ajira za mikataba kwenye kada zilizopo katika muundo wa ajira hivyo ameziagiza halmashauri zote nchini kufanya mapitio ya watumishi wa mikataba.

“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwemo madereva msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema.

Akizungumzia suala la watumishi hewa mkoani Morogoro, Majaliwa alisema ni vema wakaendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika kwa waliohusika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, alisema mkoa wake unaendelea kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzitaka taasisi zote za Serikali kufanya uhakiki wa mishahara hewa na malipo batili ya watumishi.

Alisema mkoa umebaini watumishi hewa 315 ambao wameisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 2.132 ambapo timu ya uhakiki bado inaendelea na zoezi hilo na taarifa kamili itatolewa mara kazi hiyo itakapo kamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles