28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kocha Pluijm aahidi makubwa Yanga

IMG_3892

 

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM,

KOCHA mpya wa timu ya Yanga, Hans van Pluijm, ameanza kwa mbwembwe kibarua chake baada ya kuahidi makubwa, huku akidai atahakikisha anarudisha soka la kuvutia na la ushindi ili kuwapa raha wapenzi wa timu hiyo.
Pluijm amerejeshwa kwenye timu hiyo aliyoinoa msimu uliopita baada ya kutimuliwa kwa makocha, Marcio Maximo na msaidizi wake, Leonardo Neiva, ambao wote ni kutoka Brazil.

Mholanzi huyo juzi alianza kibarua cha kuinoa timu hiyo kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, ambapo alianza kwa kufanya mazungumzo na wachezaji ili kuwajulisha anachokihitaji kutoka kwao na wao kumwahidi makubwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Pluijm alisema kwa sasa hataki kuangalia timu yake ilifanya nini nyuma, zaidi anataka kuhakikisha anatimiza mikakati yake iliyomrudisha hapa ili kuifanya Yanga iwe bora.

“Kubwa nataka timu inapokuwa uwanjani icheze mchezo wa kuvutia na wa ushindani hata inapopata ushindi uwe ushindi mzuri kuanzia mwanzo, jana (juzi) nilikaa na wachezaji kabla ya kuanza mazoezi na nikawaambia ninachokihitaji kutoka kwao na wao wakaahidi kutimiza hivyo nina imani kwa kushirikiana kwa pamoja tutakamilisha malengo niliyojiwekea,” alisema.

Akizungumzia kikosi alichokikuta, Pluijm alisema: “Sina shaka na kikosi nilichokikuta kwani kama tutajiwekea mipango mizuri lazima tutafanya vizuri kwa pamoja, kwani kila kitu ni malengo na mikakati.”

“Ukiamini kama utashinda basi utashinda tu lakini ukijiwekea kushindwa pia utashindwa,” alisema.

Alisema atahakikisha anajitahidi mapema kuirudisha timu kwenye kiwango chake, ili iweze kufanya vema katika ligi, kwani bado anajua kuwa mechi nyingi zinawakabili na wanahitaji matokeo mazuri kwa ajili ya kupata ubingwa.

Katika hatua nyingine, Pluijm alikiri kumkosa mshambuliaji Hamis Kiiza kwenye kikosi hicho ni pengo, lakini amepanga kutumia washambuliaji wengine aliowakuta kwenye timu hiyo.

“Ni lazima nione upungufu kwani alikuwa ni mshambuliaji mzuri, lakini hilo halina tatizo kubwa kwangu kwani wachezaji wengine wapo na watafanya vizuri na kuziba pengo lake,” alisema.

Yanga inatarajia kuteremka dimbani Jumapili hii kwa kuvaana na mabingwa watetezi wa ligi, Azam FC kwenye mwendelezo wa ligi hiyo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Jerry Muro, alisema Katibu Mkuu mpya, Jonas Tiboroha, anatarajia kuanza kazi na majukumu mengine ndani ya timu hiyo leo baada ya kupokea uteuzi wake mwishoni mwa wiki iliyopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles