23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wazabuni walidai Jeshi la Polisi milioni 500/-

blWAZABUNI waliopewa tenda na Jeshi la Polisi ya kulisha jeshi hilo na vikosi vyake nchini, wamelalamikia hatua ya ofisi ya uhasibu Polisi Makao Makuu kushindwa kuwalipa zaidi ya Sh milioni 700 wanazodai tangu mwaka 2008.
Pamoja na hali hiyo wamepinga hatua ya Mhasibu Mkuu wa jeshi hilo, Frank Msaki ya kufanya malipo kwa upendeleo na hata kumtuhumu kuwa amekuwa akificha nyaraka za kumbukumbu za malipo za wazabuni hao.
Wakizungumza na MTANZANIA juzi wazabuni hao walisema hatua ya kushindwa kulipwa inakwenda kinyume na kauli iliyotolewa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ya kulipa madeni yote nyuma.
Akizungumza kwa niaba ya wazabuni wenzake mmoja wa wazabuni hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisotea malipo yao ambayo yamekwamishwa na idara hiyo ya uhasibu.
“Madeni yetu tunadai tangu mwaka 2008 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameinisha tulipwe je inakuaje vocha za malipo zimeandaliwa na hatulipwi?
“Tunadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa kutoa huduma katika vikosi vya polisi vya farasi, makao makuu, FFU Ukonga pamoja na mikoa mbalimbali nchini.
“Malipo yetu yameidhinishwa lakini Msaki (Mhasibu wa Polisi), amekuwa akificha vocha zetu za malipo je hii ni haki kweli?
Hili hapana ni lazima tulipwe fedha zetu, wanalipa kwa kuangalia sura za watu jambo ambalo si sahihi hata kidogo,” alisema mzabuni huyo.
MTANZANIA ilipomtafuta Msaki ili kuweza kupata ufafanuzi juu ya tuhuma za kuficha vocha za malipo alikana kufanya hivyo.
“Ninachotaka kukujibu ni kwamba ni kweli mtu anapokudai anaweza kusema jambo lolote, lakini kiukweli sijaficha vocha za malipo tunalipa kwa utaratibu, Jeshi la Polisi lina utaratibu wake kama kuna jambo zaidi wasiliana na msemaji wetu yeye atakupa maelezo ya kina,” alijibu kwa kifupi Msaki
Alipotafutwa Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alikiri kuyafahamu madeni hayo ya wazabuni huku akiwaomba wawe na subira kwani hulipwa kulingana na fedha zinapopatikana.
“Ni kweli tunadaiwa na wazabuni wetu lakini huwa tunalipa kutokana na fedha inapopatikana na wao ni lazima walipwe ila wawe na subira tu. Suala la kufichwa vocha na mhasibu wetu linahitaji na wewe ufikiri sana maana litakuwa ni jambo la ajabu.
“Tunawaomba wazabuni wetu wawe na subira hakuna ambaye hatalipwa kama anadai fedha zake,” alisema Advera

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles