24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mashine za EFD na faida kwa mfanyabiashara

EFD

NA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

KATIKA makala ya wiki iliyopita tulielezea umuhimu wa matumizi ya Mashine za Kodi za Kielekroniki EFDs ambapo leo tunaendelea kwa kuelezea faida zake iwapo mfanyabiashara ataitumia.

EFDs zina faida kubwa sana kwa mfanyabiashara kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali bila kufutika kwa muda wa usiopungua miaka mitano na kumfanya mfanyabiashara kuepukana na usumbufu wa kuchapisha vitabu vya risiti pamoja na uhifadhi wa nakala za risiti.

Pia EFDs zinatoa haki katika makadirio ya kodi kutokana na utoaji wake wa taarifa sahihi kulingana na mwenendo wa biashara kwa mtandao kwenye mashine yenyewe na kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kupunguza malalamiko.

Mfumo wa matumizi ya mashine za EFDs, ni mfumo ambao unafanya kazi kwa uwazi na kwamba kwa kuzitumia mashine hizi ni rahisi kwa TRA kujua mauzo ya siku, mwezi na mwaka ikiwa ni pamoja na kodi ya kulipa kwa kutumia mauzo hayo.

Mashine hii ya EFDs ni zaidi ya risiti kwani mfanyabiashara anaweza kuitumia kwa kufanya shughuli nyingine kama kufanya mauzo na kutuma taarifa za mauzo kwenye taasisi nyingine mfano. EWURA, SUMATRA, Benki Kuu au Idara ya Takwimu kwani hizi zimeunganishwa na mtandao wa GPRS.

Kwa kutumia mashine ya EFDs, mfanyabiashara anaweza kutuma na kupokea fedha (Mobile Money), kulipa kodi, umeme, maji nk. hali itakayomrahisishia na kupunguza muda wa kwenda ofisi husika kupata huduma.

Mashine hizi zinatumia lugha ya Kiswahili na kiingereza, zina uwezo wa kufanya kazi masaa 48 pindi umeme unapokuwa umekatika na zinaweza kutumia betri.

Pia zinarahisisha upatikanaji wa ripoti za mauzo kwa kipindi kisichopungua miaka mitano pamoja na kuwezesha kujua mwenendo wa mauzo wakati wowote, zinarahisisha marejesho ya kodi kutokana na utunzaji wake wa kumbukumbu sahihi, zinapunguza wizi wa wahudumu katika biashara, zinapunguza idadi pingamizi na rufaa za kodi ikiwa ni pamoja na kutoa risiti ambazo ni vigumu kugushiwa.

Faida kwa upande wa serikali, mashine hizi zitasaidia kuongezeka kwa mapato serikalini ambayo yataiwezesha kutoa mahitaji ya kijamii na uchumi kwa wananchi kiukamilifu kutokana na kodi inayolipwa kufika moja kwa moja serikalini, ikiwa ni pamoja na kupanua wigo wa kodi endapo kila mfanyabiashara anayestahili kutumia EFD atatumia.

Pia matumizi ya EFDs yanawezesha usawa katika makadirio ya kodi pamoja na kuiwezesha serikali kupanga mipango ya uchumi kulingana na mapato ya ndani.

Mashine za EFDs pia zina faida kwa wanunuzi kutokana na risiti zinazotolewa baada ya kukamilika kwa manunuzi, zinampa mteja uhalali  wa umiliki wa bidhaa aliyonunua pamoja na kupata uhakika wa kuwa kodi yake imelipwa serikalini

Kwa mujibu wa sheria, iwapo mashine haifanyi kazi mtumiaji atatakiwa kutoa taarifa ya maandishi kwa msambazaji pamoja na TRA ndani ya masaa 24 na msambazaji anawajibika kuirekebisha ndani ya masaa 48.

Pia mtumiaji wa mashine anatakiwa kununua mashine kutoka kwa mmoja wa wasambazaji 11 waliothibitishwa na TRA kwa kadiri ya makubaliano.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Tanzania (TRA), Richard Kayombo.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles