25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge, viongozi Chadema kuhojiwa polisi

Cecilia Pareso
Cecilia Pareso

Na ELIYA MBONEA Na JANETH MUSHI,ARUSHA

JESHI la Polisi mkoani Arusha linatarajia kuwahoji wabunge wawili, Mwenyekiti wa Halmashauri na makamu wake wote kutoka Chadema, baada ya kufanya mikutano ya hadhara 14.

Viongozi hao wametakiwa kufika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO) kwa ajili ya kuhojiwa.

Wabunge walioandikiwa barua na kutakiwa kufika ofisini kwa RCO jana  ni Mbunge wa Karatu, Wilbroad Qambalo, Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso, Mwenyekiti wa Halmashauri, Jublet Munyenye na makamu wake, Lazaro Bajuta.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Pareso alikiri kupokea barua yenye kumbukumbu namba KRT/CID/B1/7H/VOL.VIII/344 kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Karatu ya Julai 25, mwaka huu.

Alisema barua hiyo  inamtaka yeye   na viongozi wenzake waliokuwa kwenye mkutano wa hadhara Julai 23, mwaka huu katika Kitongoji cha Ganako Kijiji cha Tloma Kata ya Ganako, wafike ofisini kwa RCO Julai 25, mwaka huu saa 8.00 mchana kwa ajili ya mahojiano.

“Nimepokea barua  mchana huu Saa 6:30 (jana) nikiwa hapa Karatu, sasa siwezi kukurupuka kuanza safari ya kwenda Arusha, nina ratiba zangu.

“Karatu mpaka Arusha mjini kuna mwendo mrefu, kama wao wameniletea barua saa 6:30 mchana nawezaje kufika Arusha mjini saa 8.00 mchana. Nitakwenda ofisini kwa RCO Jumatano saa 4.00 asubuhi,” alisema.

Alisema analishangaa jeshi hilo kwa sababu mbunge ana mamlaka ya kuzungumza na wananchi wake kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Alisema mkutano huo ulioitishwa na Qambalo ulilenga kusikiliza kero za wananchi   na kuhimiza shughuli za maendeleo.

Munyenye alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo, alikiri kuipokea huku akilishangaa jeshi la polisi wilayani humo kufanya kazi bila weledi.

“Huu ni usumbufu usio kuwa na msingi, jeshi la polisi limeacha kufanya kazi kwa maadili yake badala yake sasa wanataka kujipendekeza kwa viongozi kuwa wapo makini,” alisema.

Kutokana na kadhia hiyo, walimpigia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na kumtaka awape ufafanuzi wa mbunge wa jimbo kufanya mikutano ya hadhara.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, alithibitisha viongozi hao kutumiwa barua ya wito.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles