23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Gabo; Wanaisoma namba kimwendokasi!

gabo-4

NA SWAGGAZ RIPOTA,

KATIKA Tamasha la 19 la Kimataifa la Filamu kwa nchi za Jahazi (ZIFF) lililofanyika huko Zanzibar, imedhihirika kwamba nidhamu, kujituma, ubunifu na uaminifu vikiungana kwa pamoja humpa mtu mafanikio.

Kwenye tuzo hizo katika kipengele cha Mwigizaji Bora wa Kiume, msanii Salim Ahmed ‘Gabo Zigamba’, aliibuka mshindi kupitia filamu yake ya Safari ya Gwalu na kuwapiku wasanii wengine wakubwa Afrika Mashariki na Kati, hivyo kuwasomesha namba.

Ushindi huo mnono umepokelewa kwa shangwe na mashabiki wake ambao walikuwa na kiu ya kutaka kumuona Gabo anapata kile anachostahili kutokana na weledi katika filamu alizowahi kucheza kwa kushirikishwa au zake mwenyewe.

Msanii huyu amecheza sinema nyingi zilizompaisha na kudhihirisha kuwa ana uwezo mkubwa kisanii zikiwemo Majanga, Dhuluma, Danija, Fikra Zangu, Mama Ntilie na Bado Natafuta.

Timu ya Swaggaz ilitimba mpaka ofisini kwake Magomeni – Mikumi, jijini Dar es Salaam na kuzungumza naye mambo kadha wa kadha kuhusu ushindi wake na sanaa ya filamu Bongo ujumla wake.

TUZO ZA ZIFF 2016     

Kwenye tamasha hilo anasema alialikwa kama walivyoalikwa wageni wengine. Hakufikiri  kama atakwenda kuchukua tuzo ila ndiyo ikawa hivyo, jambo analoamini muda wake ulifika.

“Nilialikwa kama mgeni, lakini ikatokea nikapata tuzo. Imenipa heshima na hapa ndiyo naamini wakati ni ukuta. Muda umefika nimepata tuzo. Kitu cha muhimu ni kuwashukuru kwa kuniona nastahili, walikuwapo wasanii wengi ila nimeonekana mimi… ni jambo kubwa kwangu,” anasema.

Gabo anasema kufuatia ushindi huo, amefanikiwa kupata connection zaidi za kufanya kazi na wasanii mbalimbali wakubwa Afrika.

“Ni mapema sana, lakini tayari matunda ya tuzo yangu hiyo nayaona. Nimepata kazi na wasanii wengine wakubwa Afrika. Ni mwanzo mzuri,” anasema.

 KUJA NA SIYABONGA

Safari ya Gwalu imempa tuzo na kuwaburuza wasanii wengi, lakini anasema yupo mbioni kuachia kazi nyingine kali zaidi inayoitwa Siyabonga ikiwa na maana ya Asante, kazi hii ni shukrani kwa mashabiki wake.

“Sinema ya Safari ya Gwalu ni ndogo sana mbele ya Siyabonga na wengi wataipenda. Hii itawagusa wengi kwa sababu ni somo kwa watu na serikali kwa sababu inahusu tatizo na migogoro ya wakulima na wafugaji,” anasema.

 SIRI YA KIPINDI CHA BONDENI

Gabo ni msanii ambaye pia ni mwongozaji wa kipindi cha runinga kinachoitwa Bondeni kinachorushwa na Runinga ya TBC 1. Anasema lengo la kuanzisha kipindi hicho kinachofanya mahojiano na Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni kukutana na wadau mbalimbali na kwamba kimesaidia kutengeneza mtandao wa kazi zake nje ya nchi.

SIYO LAZIMA LOVE SCENES

Imezoeleka hadithi za sinema nyingi za Kibongo kuwa za kimapenzi, jambo ambalo Gabo anasema hakubaliani nalo na kwamba amepania kuondoa kabisa kasumba hiyo kwa kushiriki filamu zenye mafundisho zaidi kwa jamii.

Anasema amepania kufanya filamu zenye kuibua changamoto na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii hasa watu wasio na sauti ya kuongea wakasikika.

“Nilitaka kumtengeneza Gabo ambaye huwezi kumfananisha na msanii mwingine kwenye tasnia, yaani anayefanya harakati na wakati huohuo ni mwalimu kupitia filamu anazocheza.

“Waigizaji wenzangu kwenye hizo filamu za mapenzi tayari wameshaweka mizizi. Ndiyo maana mimi nimeamua kuutafuta umimi, niwe na utambulisho wangu ambao hautafanana na mtu yeyote,” anasema Gabo.

IMEANDIKWA NA JOHANES RESPICHIUS NA CHRISTOPHER MSEKENA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles