27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kikwete kuhutubia taifa leo

kk

 

Na Michael Sarungi, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete, leo anatarajiwa kuhutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika mkutano wake huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo jijini humo, pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuzungumzia mwelekeo wa taifa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Abilahi Mihewa, alithibisha kufanyika kwa mkutano huo.
“Unajua katika siku za hivi karibuni Rais alikuwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu na hajapata muda mzuri wa kuongea na wananchi wake, nadhani ameona haja ya kuongea na Watanzania kupitia wazee hawa wa Dar es Salaam.
“Nadhani hata Rais anatambua kuwa wananchi wanahitaji kusikia mengi toka kwake baada ya mambo mengi kupita ambayo yametishia hata kuivunja nyumba yetu (nchi),” alisema Mihewa.
Katika mkutano huo na wazee wa Dar es Salaam, Rais Kikwete anatarajiwa kuweka wazi juu ya sakata la utekelezaji wa maazimio nane ya Bunge likiwamo la kuwawajibisha viongozi waliotajwa katika sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Kwa mujibu wa maazimio nane ya Bunge ilipendekezwa viongozi hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka ya uteuzi kutokana na kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika kashfa hiyo.
Viongozi wanaotakiwa kuchukuliwa hatua na Rais Kikwete kwa mujibu wa maazimio hayo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema ambaye tayari ameshajiuzulu
Pamoja na hilo, Rais pia anatarajia kuzungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka huu ambao ulikumbwa na vurugu katika baadhi ya maeneo nchini ikiwamo watu kupoteza maisha.
Pia anatarajiwa kuzungumzia kuhusu sekta ya elimu pamoja na agizo lake la ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari nchini, upigaji kura za maoni kuhusu Katiba Mpya ukaofanyika Aprili 30 na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura lililoanza kufanyiwa maboresho Desemba 16, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles