33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Samia Suluhu aomba majeshi Afrika kukabiliana na ugaidi

suluhu
Samia Suluhu Hassan

 

Na Harrieth Mandari,

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa majeshi ya ulinzi na usalama barani Afrika kuunda mkakati wa pamoja wa kuimarisha ulinzi na usalama ambao utaweza kukabiliana na tishio la usalama ikiwemo ugaidi.

Suluhu alitoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya wiki 47 juzi jijini Dar es Salaam kwa makamanda wa majeshi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na China katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC), ambapo alisema ugaidi, biashara ya uuzwaji binadamu na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya limekua ni janga duniani.

“Kutokana na nchi nyingi barani Afrika kuwa na changamoto za kiusalama zinazoshabihiana, ni vyema kushirikiana kwa pamoja ili si tu kuimarisha usalama bali hata uhusiano mzuri,” alisema Suluhu ambaye alikuwa akimwakilisha Rais John Magufuli.

Jumla ya makamanda 39 walitunukiwa vyeti kwa ngazi ya Shahada ya udhamiri, Shahada na Stashahada katika ulinzi na usalama.

Akizungumzia matukio ya utekaji nyara, biashara ya dawa za kulevya na usafirishaji binadamu, alisema ni changamoto ambazo ni lazima kuungana kwa pamoja ili kukabiliana nazo kwa urahisi.

“Ili kukabiliana na majanga haya tunaweza kuyakabili kwa kutumia si tu kwa kutumia silaha lakini pia kwa utaalamu wa kiintelijensia,” aliongeza.

Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho, Meja Jenerali Yakoub Mohamed, aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanautumia vizuri ujuzi waliopata wakati wa mafunzo kwa manufaa ya nchi zao na bara la Afrika kwa ujumla.

“Mafunzo ya aina hii ni muhimu kwa watendaji wetu katika vyombo vya usalama ili kuimarisha ulinzi kwa wananchi wote,” alisema.

Wahitimu hao kutoka nchi za Botswana, Burundi, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na China walitunukiwa vyeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles