31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tambwe aanza mavitu Yanga

tm

 

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Yanga, Mrundi Amis Tambwe, jana alianza kujifua na kikosi hicho huku akionekana kuanza kwa kasi baada ya kuinogesha sehemu ya ushambuliaji ya timu hiyo mazoezini.

Tambwe alifanya uamuzi wa kushtukiza Jumatatu iliyopita baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja Yanga, kufuatia kusitishiwa mkataba wake na viongozi wa Simba.

Katika mazoezi hayo ya Yanga yaliyofanyika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Dar es Salaam, Tambwe alionekana mchangamfu na mwenye furaha, huku akipigiana vema pasi na wenzake na kupelekea timu aliyopangwa nao kushinda bao 1-0, lililofungwa na Simon Msuva.

Tambwe amepewa jezi namba 19 na timu yake hiyo mpya, jezi ambayo ilikuwa ikitumiwa na kiungo mkabaji raia wa Brazil, Emerson de Oliveira, aliyeshindwa kumalizia taratibu za kujiunga na timu hiyo baada ya kukosa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), namba hiyo pia inaashiria idadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita na kumpa tuzo ya mfungaji bora.

Kabla ya Emerson kuchukua namba hiyo, kipa Yussuf Abdul ndiye alikuwa akiitumia kabla ya kuhamia timu ya African Sports ya Tanga, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).

Mara baada ya kumalizika mazoezi hayo, Tambwe aliliambia MTANZANIA kuwa anafurahia kuanza maisha mapya Yanga, huku akiwataka wapenzi wa timu hiyo kukaa mkao wa kula kwani amedhamiria kuifungia mabao ya kutosha kwenye michezo atakayocheza.
“Nimeanza rasmi kujifua leo (jana), hivyo najitahidi kusoma mazingira mapya nikiwa na timu hii, kikubwa wapenzi wa Yanga wakae mkao wa kula, nimepanga kuifungia mabao ya kutosha ya kuisaidia timu kila mara nikipata nafasi,” alisema.

Maximo, Neiva waongoza mazoezi kinyonge

Huku kukiwa na taarifa za kutimuliwa kwa kocha wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo na msaidizi wake, Leonardo Neiva, jana makocha hao waliongoza mazoezi ya timu hiyo lakini kwa kasi ya chini tofauti na ilivyozoeleka.

Makocha hao jana walionekana kukaa pamoja kila mara pale walipomaliza kuwapa maelekezo wachezaji, huku wakionekana kujadiliana baadhi ya mambo.

Staili hiyo ya uendeshaji mazoezi imekuwa ya tofauti kwao, kwani kipindi cha nyuma walikuwa wakitoa maelekezo mara kwa mara wakati wachezaji wakiuchezea mpira uwanjani au kushiriki mazoezi mengine, lakini jana hali ilikuwa tofauti sana.

Habari za makocha hao kutimuliwa zilianza Jumamosi iliyopita mara baada ya timu hiyo kufungwa mabao 2-0 dhidi ya hasimu wake Simba kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe, uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Makocha wanaodaiwa kuchukua nafasi zao ni Mholanzi Hans van der Pluijm na msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa, walioinoa Yanga kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita, ambao inaelezwa wako katika hatua za mwisho za mzungumzo kuchukua nafasi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles