27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bil 1.5 zamweka Mtanzania rehani Pakistan

Mtzd Design Friday templateSiah.indd

NA MWANDISHI WETU,

MAPYA ya MTANZANIA, Adamu Akida anayeshikiliwa na kundi la maharamia nchini Pakistani, kutokana na  kudaiwa kuwekwa rehani ughaibuni na kaka yake aitwaye Juma Neti, mkazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, yazidi kuibuka.

Adamu ambaye ni mkazi wa Magomeni Mtaa wa Chemchem na Idirsa, inasemekana aliwekwa rehani kwa ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa karibu wa Mtanzania huyo zinasema kuwa, Adamu aliwekwa rehani na kaka yake huyo akitakiwa kulipa fedha za unga (mihadarati) aliochukua.

“Aliyesababisha yote hayo ni Adamu kwa sababu ndiye aliyekwenda naye Pakistani kwa kisingizio kwamba fedha zinapatikana kwa urahisi huko,” alisema ndugu huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Wakati hayo yakiendelea, jana usiku askari polisi walivamia nyumba ya Juma Neti kwa ajili ya kumkamata kwa tuhuma za kuuza dawa za kulevya.

Nyumba hiyo ambayo ipo Kunduchi, maeneo ya Ununio, Manispaa ya Kinondoni, ilivamiwa na askari hao baada ya gazeti hili kuanza kuripoti uwepo wa Mtanzania nchini Pakistani anayeshikiliwa na kundi hilo la maharamia.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo hakupokea na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakuujibu.

Pamoja na Neti kutaka kukamatwa jana, taarifa zinasema polisi wamekuwa wakimtafuta kwa muda mrefu kutokana na tabia yake ya kujihusisha na biashara hiyo bila mafanikio.

Taarifa zaidi zinasema kwamba, Neti amekuwa na utajiri wa kutisha kwa kuwa miaka michache iliyopita, alikuwa na maisha ya kaiwada ingawa sasa anaonekana kuwa miongoni mwa Watanzania wenye ukwasi mkubwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, hivi karibuni Neti aliingia ubia na kampuni moja ya Kenya baada ya kuwekeza Dola za Marekani  400,000, sawa na zaidi ya Sh milioni 800 za Tanzania.

Mmoja wa watu wa karibu na Mtanzania huyo anayeshikiliwa ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliiambia MTANZANIA, kuwa Adamu ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya Akida na alikuwa anaishi Magomeni Dar es Salaam, Mtaa wa Sunna.

Mtoa taarifa huyo, alisema kwamba alipondooka nchini miezi minane iliyopita, aliacha mke na kwamba baba yake kwa sasa anaishi Mlingotini Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mtoa taarifa huyo anazidi kueleza kuwa, Adamu ni kinyozi maarufu eneo la Magomeni, Mtaa wa Idrisa na pia ni mtunzi na msomaji mzuri wa kaswida aliyekulia katika Madrasat Damba iliyopo Mtaa wa Chemchem.

Tukio la Akida kuwekwa rehani nchini Pakistani lilijulikana mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kipande cha video kinachoonesha alivyoshikiliwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

Baada ya picha hizo kusambaa, MTANZANIA lilifuatilia kwa kina na hatimaye kufika nyumbani kwao Magomeni na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake waliothibitisha ndugu yao huyo kushikiliwa na maharamia hao.

Mmoja wa ndugu hao ambaye jina lake tunalihifadhi, alisema kabla ya kwenda nchini humo, Adamu alikwenda kwa kaka yake (Neti) ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma na kuomba msaada wa fedha kwa kuwa kazi ya kunyoa aliyokuwa akiifanya, ilikuwa haimlipi.

Kutokana na uwepo wa tukio hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeshasema inafuatilia tukio hilo kwa kuwasiliana na Serikali ya Pakistani kwa ajili ya kuangalia namna ya kumwokoa Mtanzania huyo.

Kwa upande wake Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nayo imesema inafuatilia tukio hilo kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles