27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa ataka Mbowe alindwe

Waziri Mkuu wa zamani, Edwald Lowassa, akifungua mkutano wa siku mbili wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa umoja huo, Patrobas Katambi na kulia ni Katibu umoja huo, Julius Mwita
Waziri Mkuu wa zamani, Edwald Lowassa, akifungua mkutano wa siku mbili wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa umoja huo, Patrobas Katambi na kulia ni Katibu umoja huo, Julius Mwita

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

ALIYEKUWA mgombea urais kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewataka vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumlinda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kama nyuki wanavyomlinda malkia wao.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana (Bavicha) jijini Dar es Salaam jana.

Waziri mkuu huyo wa zamani, pamoja na mambo mengine aliwataka vijana wa chama hicho kuacha vita vya ndani kwa ndani na badala yake washikamane na kuwang’ang’ania viongozi wanaowaongoza.

“Tuache vita vya ndani kwa ndani, Mbowe ndiye mwenyekiti wetu wa chama…tumlinde kama nyuki wanavyomlinda malkia wao. Mtu akishakuwa kiongozi tumg’ang’anie,”alisema Lowassa.

Lowassa ambaye alijiunga na upinzani mwishoni mwa mwaka jana alisema kumekuwapo na kawaida ya kuibuka kwa makundi uchaguzi unapomalizika.

Azungumzia uchumi

Katika mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia uchumi ambapo alisema hivi sasa maisha ya Watanzania walio wengi hayana uhakika, huku matumaini kidogo yakielekezwa kwa watu wachache.

“Binadamu anaishi kwa matumaini, lakini mambo yanayoendelea hapa nchini hayatoi matumaini hayo…hali ya uchumi inakwenda vibaya sana, kuna rafiki yangu mmoja ana msamiati wake anasema maisha ni pasua kichwa hivi sasa kwa sababu hayana uhakika,” alisema Lowassa.

Aidha Lowassa alieleza kusikitishwa kwake kwa baadhi ya watu kuacha kuzikana kwa sababu ya siasa ambapo alisema hayo ni mambo ya ovyo.

Ajivunia vijana

Katika hotuba yake hiyo, Lowassa aliwapongeza Bavicha kwa kutii maelekezo ya Mbowe kuhusu kusitisha uamuzi wao wa kwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Niwapongeze kwa kutii maelekezo ya mwenyekiti wetu, najua haikuwa rahisi, mlikuwa mmeshajipanga lakini maelekezo ya mwenyekiti ni mazuri, vitu vingine si lazima uende mbali sana ni kama kwenye simu kwamba ‘message sent’ mlifikisha ujumbe mahsusi hata kama hawakubaliani lakini ujumbe umefika.

“Wala msione aibu mnachofanya, vijana mngefanya tofauti ningeshangaa, nyie ndio chachu ya mabadiliko lazima mje na kitu kipya na mawazo mapya, ninyi ni jeshi la chama.

“Kwa uzoefu wangu CCM lazima watakwenda kumtambulisha mwenyekiti wao mpya katika Uwanja wa  Jamhuri mjini Dodoma, hivyo wananchi wenyewe wataangalia na kupima kama Chadema wanazuiwa kwa nini wapinzani wazuiwe, waachane wapate tabu kujieleza kwa umma” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Kuhusu uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli hivi karibuni, Lowassa aliuponda na kusema ni wa kibaguzi kwa sababu umewatenga vijana wa vyama vya upinzani.

“Kama wewe ni CCM utakuwa mkuu wa wilaya, mkoa na hata mkurugenzi wa halmashauri lakini hali ni tofauti kwa vijana wa upinzani, wanabaguliwa utadhani si Watanzania.

“Hili ni jambo la kutafakari na kukemea kwa sabu ajira ni tatizo hapa nchini, lakini hata hizo chache zinatoka kwa kubaguana pamoja na jitihada zote lakini hazisaidii,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles