31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tabia zinazowatofautisha wafanyabiashara wanaofanikiwa, wasiofanikiwa

Mfanyabiashara akiwa katika Soko la Kariakoo
Mfanyabiashara akiwa katika Soko la Kariakoo

Na Makirita Amani,

BIASHARA si kuuza na kununua pekee, wengi wanaoingia kwenye biashara kwa mtazamo huu wa kuuza na kununua huwa hawafiki mbali. Na wala biashara si kuwa na wazo na mtaji pekee, wengi wamekuwa na mawazo mazuri na mtaji wa kutosha, lakini walipoingia kwenye biashara hawakuweza kufika mbali.

Biashara inabeba zile tabia ambazo mwanzilishi anakuwa nazo. Hata mfanyabiashara anapoajiri, wafanyakazi wake wanaishia kufanya kazi kama anavyofanya yeye.

Hivyo, kabla hujalalamika kwa nini biashara yako haiendi vizuri, ni vyema ukajichunguza kama tabia zako zinachangia kuikuza au kuiua.

Kuwa tayari kuweka juhudi kupita kawaida ni moja ya tabia ambazo zinawezesha biashara kukua. Biashara si rahisi hata kama mtu una wazo bora na una wasaidizi wengi. Wewe kama mwendeshaji na mmiliki wa biashara unahitajika kuweka juhudi kubwa kwenye biashara yako. Unahitaji kujua kila kitu kinachoendelea kwenye biashara yako na kuona kama uamuzi unaofanywa ni sahihi. Unapoona inakufa, jua kuna uzembe ulikuwa unajitokeza kwa muda mrefu mpaka imefikia hatua ya kuleta hasara. Iwapo mmiliki wa biashara anakuwa karibu na biashara yake na kuweka juhudi kubwa, atakuwa ameshaona mapema tatizo lolote linalojitokeza.

Kama wewe ni mfanyabiashara au unapanga kuingia kwenye biashara, basi jua unahitaji kuweka juhudi kubwa kwenye biashara yako. Unahitaji kuijua ndani na nje, jua kila kinachoendelea kwenye biashara hiyo ili uweze kuchukua hatua mapema pale changamoto zinapotokea.

Kuwa tayari kujifunza kila siku ni tabia nyingine ambayo inasaidia biashara nyingi kukua. Kwa dunia ya sasa, mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa, biashara unayofanya leo hii kuna uwezekano miaka kumi ijayo isiwapo kabisa. Tumeona jinsi ambavyo maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yalivyoweza kuua biashara nyingi. Kwa mfano, kwa sasa kila mtu anaweza kutumia intaneti kwenye simu yake ya mkononi, kwa namna hii wanaofanya biashara ya intaneti imekufa. Ili kuweza kuona mabadiliko ya aina hii, kabla hayajaleta madhara kwenye biashara ni lazima mfanyabiashara awe tayari kujifunza kila siku kuhusu biashara yake na nyingine kwa ujumla. Ni muhimu ajue mwenendo upoje na hatua zipi muhimu za kuchukua. Kwa dunia ya sasa, ni hatari sana kuendesha biashara kwa mazoea.

Kwa wafanyabiashara wote, ni muhimu kujifunza kila siku. Jifunze mbinu bora za kuikuza biashara yako, kuongeza mkopo, kuajiri na kusimamia biashara yako ili uweze kuikuza.

Uaminifu ni tabia muhimu mno kwenye ukuaji wa biashara yoyote ile, bila ya uaminifu hakuna biashara. Kwa dunia ya sasa, hata kama mteja anahitaji kununua kwako mara moja tu, kama hukuwa mwaminifu kwake kwa kumpa kile anachohitaji, ana nafasi kubwa ya kukunyima wateja wengi zaidi. Watu sasa wana nguvu kubwa ya kuweza kuwasiliana na watu wengi ndani ya muda mfupi kwa kutumia mitandao ya kijamii. Jambo lolote ambalo limewakera watu watashirikishana kupitia mitandao hii. Hivyo, kama mteja hakuridhika, ni rahisi kuwaambia wengine na hivyo kukunyima wateja wengi zaidi. Uaminifu ni nguzo muhimu kwenye biashara, kwa sababu hakuna biashara kama hakuna wateja na hakuna wateja kama hakuna uaminifu.

Unapoamua kuingia kwenye biashara, kuwa mwaminifu, ahidi kile unachoweza kutekeleza na tekeleza kile unachoahidi. Usiongeze chumvi ili kuuza, unaweza kuuza mara moja na ikawa ndiyo mwisho wako kumuuzia mteja huyo na wengine wanaofahamiana naye. Kama kuna kitu ambacho bidhaa au huduma yako haiwezi kufanya kuwa mkweli na mweleze mteja wako hivyo, atakuamini na mtafanyabiashara pamoja kwa muda mrefu.

Uvumilivu ni tabia nyingine ambayo imewezesha biashara nyingi kukua. Hakuna biashara ambayo haikutani na changamoto, hakuna biashara ambayo kila wakati tangu inaanza imekuwa inatengeneza faida tu. Kila biashara inapitia magumu, hasa mwanzoni. Kuna wakati biashara inakuwa inajiendesha kwa hasara, wakati mwingine wateja wanakuwa wasumbufu, bado pia wafanyakazi nao wanakuwa changamoto. Biashara yoyote inayoonekana kufanikiwa leo, imepitia changamoto nyingi huko nyuma. Ni uvumilivu wa waendeshaji wa biashara hizo ndiyo umewawezesha kufika pale walipo sasa.

Unapochagua kuingia kwenye biashara, jua unahitaji kuwa mvumilivu. Kama unaingia kwa lengo la kupata faida ya haraka, utakata tamaa mapema. Jiandae kuweka juhudi kubwa huku ukiwa mvumilivu na utapata matokeo bora kupitia biashara hiyo.

Mafanikio ya biashara yako yanaanza na wewe mwenyewe, biashara itakua au kufa kutokana na hatua unazochukua wewe mwenyewe. Chukua hatua bora ili biashara yako iweze kukua.

Mwandishi ni mjasiriamali na muendeshaji wa mtandao wa AMKA MTANZANIA (www.amkamtanzania.com).  Mawasiliano 0717396253 au barua pepe [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles