31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi watano wauawa Marekani

Waandamanaji wakiandamana kupinga ukatili wa polisi kwa watu weusi nchini Marekani.
Waandamanaji wakiandamana kupinga ukatili wa polisi kwa watu weusi nchini Marekani.

DALLAS -MAREKANI

MAOFISA watano wa Jeshi la Polisi mjini Dallas nchini Marekani wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine sita kujeruhuwa.

Mauaji hayo yaliyolaaniwa na Rais wa Marekani, Barack Obama, yalitokea juzi usiku wakati wa maandamano ya amani kupinga mauaji mengine ya raia wawili weusi ambayo polisi wanatajwa kuhusika.

Raia wawili weusi waliouawa ni Philando Castile wa Jimbo la Minnesota na Alton Sterling wa Jimbo la Louisiana.

Maofisa wa polisi katika mji huo ambao uko katika ya Jimbo la Texas walisema mauaji hayo yametekelezwa na washambuliaji wawili wa kulenga shabaha.

Obama alisema kuna haja ya kumaliza ubaguzi uliopo kwa sasa kwa kuwa kwa mujibu wa takwimu inaonyesha kuwa idadi ya Wamarekani weusi waliopigwa risasi na maofisa wa polisi ni kubwa ikilinganishwa na ya watu weupe.

“Visa kama hivi vinapotokea, kuna sehemu kubwa ya raia wanaohisi hawatendewi haki kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, kwa sababu hawatazamwi kwa njia sawa, na hili linauma pia ukiangalia mashambulizi ya leo (juzi) yalikuwa hayana maana, yaliyopangwa na mashambulizi ya chuki.

“Mauaji ya kikatili ya watu wawili weusi raia wa Marekani yaliyofanywa na polisi kama mengine yaliyotokea ni jambo kila Mmarekani anayepaswa kulichukia kwa kuwa ubaguzi umesababisha imani ya jamii kupungua dhidi ya polisi,” alisema Obama.

Miongoni mwa maofisa hao waliofariki ni Ofisa wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Brent Thompson (43).

Mkuu wa Polisi wa Dallas, David Brown, alisema maofisa wa polisi bado wanakabiliana na mshukiwa mmoja anayedaiwa kujificha katika jumba linalotumiwa kuegesha magari.

“Mshukiwa huyo ambaye tunawasiliana naye amewaambia maofisa wetu kuwa mwisho unakaribia na ataumiza na kuua wenzetu wengi, akimaanisha maofisa wa usalama na kwamba kuna mabomu yaliyotegwa eneo lote, kwenye gereji na katikati ya jiji.

“Usiku wa leo (juzi) watu wenye silaha waliwashambulia kwa risasi askari polisi 10 kutoka kwenye ngome wakati wa maandamano, askari polisi watatu walifariki papo hapo, wawili wanafanyiwa upasuaji na watatu wako katika hali mbaya, maofisa wengine wawili walipata majeraha madogo” alisema Brown.

Pia alisema mwanamke aliyekuwa karibu na eneo alipojificha mwanamume huyo anashikiliwa na maofisa wa usalama kwa ajili ya mahojiano zaidi na kuongeza kuwa hawezi kusema kuwa wamewakamata washukiwa wote.

Ufyatuaji risasi ulitokea saa tatu kaso robo usiku kwa saa za Texas wakati waandamanaji walipopita barabara za mji na kuwafanya kukimbilia usalama wao.

Inaarifiwa kuwa shambulio hilo lilitokea wakati maelfu ya raia wakiwa katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa ajili ya kupinga mauaji ya watu weusi.

Mtu mmoja ambaye ametambulika kwa jina la, Shetamia Taylor, alipigwa risasi mguuni akiwakinga watoto wake na kwa sasa anapokea matibabu hospitalini.

Vyombo vya habari katika Jimbo la Dallas vimeripoti kuwa kumetokea mlipuko mkubwa eneo hilo licha ya habari hizo kutothibitishwa na polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles