23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Zoka aula rasmi

Zoka akiapishwa IkuluNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

WAKATI Rais Jakaya Kikwete akiwaapisha wakuu wa mikoa, makatibu wakuu wa wizara na makatibu tawala wa mikoa,  aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Usalama wa Taifa, Jack Zoka amekula kiapo cha kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Sherehe za kuapishwa kwa viongozi hao wapya zilifanyika jana katika viwanja vya Ikulu Dar es Salaam.

Zoka aliteuliwa kushika wadhifa wake mpya Septemba 30, mwaka huu wakati wakuu wa mikoa, makatibu wakuu na makatibu tawala wapya walitangazwa kushika nafasi hizo juzi.

Uteuzi wake ulitangazwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili kuchukua nafasi  iliyokuwa inashikiliwa na Balozi Alex Masinde ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Uteuzi wa Zoka kushika wadhifa huo ulikuwa gumzo miongoni mwa wafuatiliaji na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini kutokana na Idara ya Usalama wa Taifa kuhusishwa na masuala mbalimbali ya kisiasa na kijamii nchini wakati akiongoza idara hiyo.

Hata hivyo, anakumbukwa zaidi kutokana na matukio mawili makubwa zaidi.

Hasa kitendo chake kama kiongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa kwa kujitokeza hadharani na kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

Tangu Tanzania kupata uhuru, ilikuwa haijawahi kutokea kwa kiongozi wa idara hiyo nyeti kujitokeza kuzungumza na waandishi wa habari.

Zoka alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza Novemba 4,2010 alipoitisha mkutano na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) kutoa taarifa ya kukanusha tuhuma zilizoelekezwa katika idara hiyo na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.

Taarifa hiyo ilikuwa ikikanusha madai ya Dk. Slaa kwamba maofisa wake wamekuwa wakihusika katika kuiba kura zake na kumwongezea mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM.

“Tunasisitiza kwamba kwa makusudi au kwa kudanganywa na watu wanaojiita maofisa wa Usalama wa Taifa, Dk. Slaa amejikuta akitumia taarifa za uongo kutoa matamshi ya kuwadanganya Watanzania ili kuwachochea kuvunja amani. Kwa lugha ya kawaida tunasema Dk. Slaa ‘ameingizwa mjini’ na yeye ameingia kichwa kichwa,” alikaririwa wakati huo Zoka.

Pia Zoka alijitokeza tena Julai 26, mwaka 2012 kujibu mapigo ya kuhusishwa kwa TISS na utekaji na utesaji wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka na njama za kudhuru viongozi wa vyama vya upinzani.

“Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza taarifa zenye tuhuma kadhaa dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa. Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari zikiihusisha idara hii na matukio ambayo yanaidhalilisha na kuzua maswali mengi kwa wananchi.

“Kati ya tuhuma hizo ni tukio la kutekwa kwa Dk. Stephen Ulimboka, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari na madai ya kufanywa kwa mipango ya kuwadhuru baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani,” alisema wakati huo.

Akizungumzia uteuzi wake, Zoka alisema atahakikisha anasimamia maslahi ya Tanzania nchini humo.

“Ukizingatia Canada kwa sasa inatajwa kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, hivyo nitahakikisha naangalia suala la uchumi la nchini humo linainufaishaje Tanzania,” alisema.

WAKUU WA MIKOA, MAKATIBU WAKUU WAAPISHWA

Rais Kikwete jana aliwaapisha viongozi hao wapya katika sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Ikulu.

Wakuu wa mikoa walioapishwa na mikoa yao kwenye mabano ni Halima Dendego (Mtwara), Dk. Ibrahim Msengi (Katavi), Amina Masenza (Iringa) na John Mongella (Kagera).

Makatibu wakuu ni Dk. Donan Mmbando anayekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Yohana Budeba (Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Mhandisi Mbogo Futakamba (Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji) na Dk. Adelhelm Meru (Wizara ya Utalii na Maliasili).

Wengine walioapishwa ni Charles Pallangyo anayekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita na Ado Mapunda Katibu Tawala Mkoa wa Arusha.

MA-DC presha juu

Katika hatua nyingne, presha inaonekana wazi kupanda kwa wakuu wa wilaya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MTANZANIA jana, wakuu wa wilaya mbalimbali walioomba wasitajwe majina yao gazetini, walisema tangu waliposikia uteuzi huo usiku wa kumkia jana hawakulala.

“Kaka ni presha, presha, presha tupu, yaani tumesikia rais amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa, sijui hatima yangu si unajua vyeo hivi.

“Niliposikia rais amefanya uteuzi huu, kwa kweli usiku wa juzi sijalala sawasawa maana hapa nina mipango mingi ya maendeleo nikitoka itakufa… lakini ndiyo kazi ilivyo.

“Natumia nafasi hii kuwapongeza wenzangu ambao wamepanda kuwa ma-RC maana inaonyesha wazi tunafanya kazi na rais anatambua mchango wetu,” alisema mmoja wa wakuu hao wa wilaya.

DC mwingine kutoka mkoani Singida alisema: “Nasikia rais kafanya mabadiliko, kwa kweli nasubiri kusikia kama nabaki au naondoka, maana ndiyo vyeo vya kuteuliwa vilivyo.

“Nipo njiani hapa nasafiri kwenda sehemu ndani ya mkoa wangu sijui kama nitabaki, kaka…kaka…kaka weeee acha mambo haya, maana nimekunywa juisi tu leo,” alisema.

DC mwingine alisema: “Nilipigiwa simu kutoka Dodoma jana usiku (juzi) na rafiki yangu, nikaambiwa juu ya mabadiliko, unajua unapokuwa kiongozi unakuwa na mambo unayosimamia, ukiondoka yanaweza kukwama.

“Naomba Mungu nibaki ili niendelee kusimamia mipango yangu niliyoanza nayo hapa ili mwisho wa siku wananchi wa wilaya hii wapate kile ambacho walikuwa wanakitegemea.”

DC mwingine alisema: “Siku zote mtu ambaye amesimamia majukumu yake hawezi kuwa na hofu katika hili, ni jambo la kawaida katika uongozi.”

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA imezipata Dar es Salaam jana, zinasema wakuu wengi wa wilaya huenda wakaachwa kutokana na kushindwa kusimamia vizuri agizo la rais la ujenzi wa maabara katika shule za sekondari.

Habari zinasema kabla ya uteuzi huo, umefanyika uchunguzi wa kina juu ya mwenendo wa ma-DC wa kusimamia maagizo yanayotolewa na Serikali.

Pia habari zinasema chanzo kingine cha kuwapo mabadiliko makubwa ni kukosekana maadili, hali iliyosababisha ma-DC kadhaa kuitwa mbele ya Sekretarieti ya Madili ya Viongozi wa Umma katika siku za hivi karibuni.

Juzi Rais Kikwete aliwabadilisha wakuu wa mikoa, huku akiwapandisha wakuu wa wilaya wanne kuwa wakuu wa mikoa.

Katika uteuzi huo, Rais Kikwete alimpandisha Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongella kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Taarifa iliyotolewa juzi kwa vyombo vya habari, ilisema Rais Kikwete amefanya mabadiko makubwa ya wakuu wa wilaya yakiwamo ya kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda atatangaza majina hayo baada ya taratibu za kuwapangia vituo vya kazi.

Katika mabadiliko ya mwisho kufanywa na Rais Kikwete, aliwaacha karibu wakuu wa wilaya 50 kwa sababu mbalimbali zikiwamo za matatizo ya kimaadili na wengine walikuwa walevi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles