27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MKANGANYIKO  

EVANS MAGEGE NA KOKU DAVID

UTEKELEZAJI wa sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) umezua mkanganyiko kwa wananchi baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mabenki kutofautiana jinsi ya ukusanyaji wake.

Tayari sheria hiyo imeanza kutumika jana baada ya kupitishwa na Bunge la Bajeti lililomaliza mkutano wake wa tatu juzi mjini Dodoma huku wananchi wanaotumia huduma za kibenki na miamala ya kifedha kwa njia ya simu wakiwa hawajui hasa atakayebeba mzigo wa kodi hiyo.

Utekelezaji wa sheria hiyo mpya ya kodi unamtwisha mzigo mpya wa kodi mwananchi ambaye ni mtumiaji wa miamala ya kifedha kwenye mabenki, miamala ya fedha ya kampuni za simu na taasisi nyingine za fedha.

Tangu Julai mosi mwaka huu, watumiaji wa huduma wa kibenki wanakatwa asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani kwenye kila muamala wanaoufanya ambayo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na TRA ni ongezeko la Sh 152.50 katika kila makato ya Sh 1,000 yanatozwa na benki mteja anapofanya muamala.

Kwa upande wa miamala ya fedha ya simu za mkononi za Vodacom, Tigo, Airtel na Ezy Pesa, mtu anayetuma Sh 10,000 atakatwa Sh 250 pamoja na asilimia 18 ya VAT, anayetoa Sh 10,000 anakatwa Sh 1,250 pamoja na asilimia 18 ya VAT, jambo ambalo mamlaka za Serikali zimepiga marufuku.

Katikati ya sintofahamu hiyo ambayo msingi wake ni tamko lililotolewa na benki mbalimbali zinazofanya shughuli zake hapa nchini, likieleza kuwa kuanzia Julai Mosi, 2016, ada na makato yote ya kibenki kwa wateja yatatozwa kodi ya ongezeko la thamani, Mamlaka ya Mapato imepiga marufuku huku ikitishia kuchukua hatua kwa benki zitakazotekeleza makato hayo kwa wateja wake.

Marufuku ya TRA ilitangazwa jana na  Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TRA jijini Dar es Salaam.

Kidata ambaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumzia mkanganyiko uliojitokeza kwa jamii kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo, alisema makato ya kodi ya VAT katika miamala ya fedha itakayofanywa na wananchi itatokana na ada za huduma ambayo mteja ametozwa na taasisi ya fedha inayompatia huduma.

Alisema hakuna makato yatakayofanyika katika amana ya mwenye fedha na kwamba benki au taasisi yoyote ya fedha itakayoongeza makato kwa mteja wake kwa makusudi au kwa kisingizio cha kulipia kodi itachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, Kidata alisema TRA itatoa maelekezo ya  namna utoaji wa risiti za kielektroniki utakavyofanyika ili kuziwezesha benki na taasisi za fedha kutimiza matakwa ya sheria ya kodi ya ongezeko la thamani ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016.

Alifafanua kuwa BoT ina jukumu la kudhibiti benki zote nchini zisiwakate wateja wake asilimia 18 ya kodi ya VAT juu ya makato ya huduma zinazotozwa sasa na kwa upande wa kampuni za simu jukumu hilo ni la TCRA.

“Kuna taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa makato ya VAT yatatozwa katika amana ya mwenye fedha benki, ndugu waandishi taarifa hizi si za kweli na kama kuna mtu amekatwa tunaomba mtuletee ushahidi ili tuchukue hatua.

“Kwa mfano mteja akikatwa Sh 1,000 na benki kutokana na huduma aliyopewa, Serikali nayo itakata kodi asilimia 18 ndani ya hayo makato ya Sh 1,000. Mfano huo wa Sh 1,000 kwa huduma ya kibenki, asilimia 18 ya VAT itakuwa Sh 152.50 na si vinginevyo,” alisema Kidata.

Wakati Kamishna Kidata akieleza hayo, Sheria ya Fedha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 inaeleza kuwa kodi hiyo itatozwa kwa mtumiaji wa mwisho.

Sheria hiyo inasomeka:-

“Kodi ya Ongezeko la Thamani ni ya mlaji inayotozwa katika bidhaa zinazostahili kutozwa kodi, ikiwa ni pamoja na huduma, mali zisizohamishika na shughuli yoyote ya kiuchumi wakati wowote thamani inapoongezeka katika kila hatua ya uzalishaji na katika hatua ya mwisho ya mauzo.

“Kodi ya ongezeko la thamani  inatozwa kwa bidhaa zote zinazozalishwa ndani na huduma na kwenye maduhuli. Mtu aliyesajiliwa kulipa kodi ya ongezeko  la thamani tu.”

Hata hivyo, agizo hili la TRA linayagusa pia makampuni ya simu ya Vodacom, Tigo, Airtel na Zantel yanayotoa huduma za miamala ya kifedha kwa njia ya simu kutowatoza watumiaji wake makato mapya ya asilimia 10 ambayo Serikali ilitangaza kuyakata kutoka kwenye mapato yake.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa TCRA, Innocent Mungi, alieleza kuwa jukumu hilo si la taasisi yake bali linaihusu TRA na BoT.

Mungi aliliambia MTANZANIA Jumamosi  jukumu la TCRA ni kusimamia mawasiliano kwa kampuni za simu pekee.

Wakati Mungi akitofautiana na kauli ya Kamishna Mkuu wa TRA, Kidata, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, naye alitoa kauli inayotofautiana na mamlaka hiyo ya mapato kuhusu tozo ya kodi hiyo.

Gavana Ndulu alisema VAT hutozwa kwa mtumiaji wa mwisho wa huduma za kibenki na kusisitiza kwamba siku zote mzigo wa VAT humwangukia mtu wa mwisho ambaye ni mteja wa benki.

Alisema taasisi za kibenki ni wakala wa Mamlaka ya Mapato (TRA) katika makusanyo ya kodi ya VAT hivyo kazi yake ni kukusanya kodi kwa niaba ya mamlaka hiyo kutoka kwa wateja wake.

“Kinachokanganya ni nini?  Kwa sababu maana ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inafahamika wazi kwamba mhitaji wa huduma ndiye anayekatwa, hawa benki ni wakala tu wa TRA, wao ndio wanaokusanya makato ya VAT  na kuwasilisha TRA, kwa ufafanuzi mzuri waulizeni TRA,” alisema Gavana Ndulu.

Kuja kwa ongezeko la kodi ya VAT, kumetokana na marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148, yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akisoma bajeti ya Serikali bungeni.

Katika ufafanuzi wa marekebisho hayo, Dk. Mpango alisema Serikali imekusudia kutoza kodi ya ongezeko la thamani kwenye ada za huduma za kibenki zinazotozwa na benki zote nchini ili kupanua wigo wa kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles