25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

‘Skendo’ ya Lugumi yazikwa bungeni

Lugumi
Lugumi

NA WAANDISHI WETU, DODOMA

 

SAKATA la mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kudaiwa kupewa tenda na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 vya polisi nchini, limezimwa rasmi bungeni.

 

Hii inatokana na hatua iliyofikiwa na kutangazwa jana na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, akiiagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo wa vifaa vya utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi unafanya kazi ndani ya miezi mitatu kuanzia jana.

 

Dk. Tulia aliyasema hayo jana baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kumaliza kusoma hotuba ya kuliahirisha Bunge hadi Septemba 6 mwaka huu.

 

Sakata la Lugumi liliibuliwa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na baadaye kutinga bungeni ambapo Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliunda kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa PAC ambaye pia ni Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilary (CCM).

 

Katika maelezo yake, Dk. Tulia alisema PAC kwa kushirikiana na kamati ndogo, zilikuwa zimekamilisha uchunguzi ingawa hakukuwa na uhakika kama ripoti hiyo ya uchunguzi ingewasilishwa bungeni jana.

 

Pamoja na Dk. Tulia kuiagiza Serikali kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi, pia aliagiza kamati hiyo ifuatilie na kutoa taarifa katika taarifa ya mwaka ya kamati.

Alisema Bunge la 10 lilitoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuhusu mradi wa kufunga mashine za utambuzi wa alama za vidole kati ya mkataba huo.

“Naagiza Serikali kuhakikisha mashine hizo zinafanya kazi kuanzia kesho na kamati ya PAC, itafuatilia na ilete taarifa katika taarifa ya kamati ya mwaka,” alisema.

Alisema katika uchunguzi wake, kamati ilibaini kuwa mradi huo unafanya kazi katika vituo 14 kati ya vituo 108 jambo ambalo lilikuwa linaenda kinyume na mkataba.

“Kutokana na changamoto hiyo,
PAC ilimtaarifu Spika wa Bunge ambaye aliwaruhusu kuunda kamati ndogo ambayo nayo ilikagua na kubaini upungufu.

“PAC kupitia kamati ndogo, ilikubaliana kukabidhi taarifa hiyo kwa Spika ambapo na yeye ameona kuwa inastahili kuwasilishwa.

“Kwa mujibu wa kanuni ya 117, fasili ya 17, Spika ataweka utaratibu wa kujadili taarifa ya kamati endapo kamati yoyote katika utekelezaji wa majukumu yake itaona kuna mambo ya utekelezaji, inaweza kutoa taarifa maalumu kwa waziri husika ili aweze kuchukua hatua zinazostahili,” alisema Naibu Spika.

 

Naye Aeshi alipokuwa akizungumza na MTANZANIA, alisema kamati yake ilipitia taarifa ya kamati ndogo na kwa pamoja walikubaliana kuiwasilisha kwa Spika ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kukubali ijadiliwe au la.

 

“Sisi tumekabidhi ambacho kimeonekana huko na mapendekezo yetu yapo, nadhani unakumbuka tuliomba kuchunguza kwa Spika hivyo yeye ndiye mwenye mamlaka,” alisema.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa kamati hizo, waliponda uamuzi huo wa Naibu Spika na kusema si sahihi kwani katika uchunguzi wao, walibaini upungufu mwingi ambao ungetakiwa kujadiliwa bungeni.

 

Mradi wa kuweka mashine za utambuzi wa vidole katika Jeshi la Polisi, ulifanywa na Kampuni ya Lugumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles