25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ukimpa mwanafunzi mimba jela miaka 30

George Masaju
George Masaju

Na Arodia Peter, Dodoma

MAREKEBISHO ya Muswada wa pili wa  Sheria mbalimbali wa mwaka 2016 kuhusu elimu, umepitishwa rasmi na Bunge jana huku ukiacha maswali kadhaa kuhusu utekelezwaji wake.

Muswada huo uliowasilishwa mwishoni mwa wiki na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, unapendekeza adhabu kwa anayempa ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi ama sekondari, kuoa au kuolewa na mwanafunzi na mwanafunzi kuoa mtu yeyote, kuwa ni kifungo cha miaka 30 jela na faini ya Sh milioni tano.

Wakichangia mjadala wa muswada huo  Bungeni jana, baadhi ya wabunge walihoji jinsi sheria hiyo itakavyotekelezwa huku wengine wakishauri   vinasaba (DNA) vitumike mahakamani  kuondoa uwezekano wa kufungwa watu wasiohusika na kosa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) alishauri badala ya mtuhumiwa kufungwa na baadaye kutakiwa kulipa faini, suala hilo liwe kinyume chake, yaani alipe kwanza faini na baadaye atumikie dhabu ya kifungo   mtoto aliyezaliwa apate matunzo.

Mlata  pia alionyesha wasiwasi wake kuhusu namna ya kuwaadhibu wanawake wanaowatelekeza watoto.

Alisema sheria iko kimya juu ya suala hilo.

Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo (CCM), alisema sheria hiyo imewabagua wanawake watu wazima ambao wanawateka na kuwaweka kinyumba wanafunzi wa kiume na kusababisha wao kupata mimba.

“Mheshimiwa Naibu Spika hii sheria iangalie upya masuala haya, kuna watoto wetu wa kiume wanatekwa na kuwekwa kinyumba na wanawake watu wazima, je, nani atapaswa kushtakiwa hapa?

“Ni vema na huyu mwanamke aliyesababisha kupewa mimba na mwanafunzi ashtakiwe na hata kulipa faini.

“Pia hii sheria inaweza kusababisha watu wengine kufungwa kwa kusingiziwa mimba, ni vema suala la DNA hapa litumike ipasavyo.

“Hizi kesi zisiamuliwe zisubiri mpaka binti aliyepewa mimba ajifungue kwanza ili athibitishwe na DNA kujua muhusika halisi wa mimba vinginevyo vijana wengi wataonewa sana,” alisema Mwalongo.

Akihitimisha hoja yake, AG Masaju alisema sheria hiyo si mpya bali imeongezwa vifungu kutokana na mahitaji ya sasa.

“Sheria ya kanuni ya adhabu imeweka wazi, kumpa mimba au kuwa na uhusiano naye wa  mapenzi hata kama mmekubaliana mtoto chini ya miaka 18, sheria inakutambua kuwa ni mbakaji.

“Mtu akimpa ujauzito mtoto au mtu mzima akapewa mimba na mtoto, sheria haiwabagui,” alisema.

AG alisisitiza wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto ikizingatiwa sheria pekee haziwezi kusaidia kuondoa au kumaliza makosa hayo.

“KIla mzazi awajibike kulea mtoto ili awe na tabia nzuri, tusitengeneze taifa la wahalifu, watu ambao hawaheshimu watu wazima kila kitu kwao ni sawa si sahihi,” alisema Masaju.

Katika Muswada huo, Kifungu namba 60 A kinapendekeza adhabu ya Sh milioni tano au kifungo cha miaka mitano gerezani au vyote kwa pamoja kwa mtu atakayebainika kusaidia, kushawishi au kufanikisha mwanafunzi wa shule ya msingi ama sekondari kuolewa au kuoa,”alisema AG.

Awali, adhabu kwa makosa ya kumpa ujauzito mwanafunzi ilikuwa faini isiyozidi Sh 500,000 na kosa la pili   faini Sh 500,000 au jela miaka mitatu.

Kamati ilikubaliana na mabadiliko hayo ikisema yanalenga kumjengea mwanafunzi wigo wa ulinzi na mazingira mazuri ya kumwezesha akamilishe masomo yake kwa ngazi hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles