26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda: Kashfa IPTL imetia doa Serikali

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

NA ELIAS MSUYA, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali imetiwa doa na kashfa ya IPTL ambapo zaidi ya Sh bilioni 200 zinadaiwa kuchotwa kwenye akaunti maalumu ya ‘Tegeta Escrow’, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Pinda ambaye yupo jijini London, Uingereza kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Afrika na wawekezaji wa Ulaya, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) .

Alisema madai hayo yametia doa Serikali kwa kuwa tayari wahisani wameshakata misaada waliyoahidi kuitoa kwa ajili ya bajeti ya 2014/15.

Pinda alisema Serikali inafanya uchunguzi kupitia Takukuru na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Madai haya yanatia doa kwa maana yamesemwa na vilevile wanaweza (wahisani) kukata kutoa misaada, ni mbaya sana. Kwa bahati mbaya sana wakuu wamechukua hatua (kukata misaada) kabla hata matokeo yenyewe hayajajulikana,” alisema.

Pinda alipotakiwa kusema kama pamoja na kashfa hiyo wawekezaji ambao atakutana nao London watamwelewa, alisema: “Itategemea uchunguzi unaoendelea, jambo hili limejitokeza kama tuhuma na tulichofanya kama Serikali tumekiagiza chombo kinachohusika na rushwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali mara moja kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo.”

Alisema Tanzania ni kati ya nchi zinazojitahidi katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizohudhuria mkutano huo ni Nigeria, Ghana, Uganda, Rwanda na Togo.

Hivi karibuni nchi wahisani zilitangaza kuikatia misaada Serikali ya zaidi ya Sh trilioni 1 kutokana kashfa ya fedha za mradi wa kuzalisha umeme wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).

Hivi karibuni, Balozi wa Finland ambaye pia ni mwenyekiti wa wadau wa maendeleo nchini, Sinikka Antila, alithibitisha nchi za Ulaya hazijatoa pesa yoyote kati ya dola za Marekani milioni 558 milioni sawa na Sh bilioni 937 zilizoahidiwa katika bajeti ya mwaka 2014/15.

Antila alisema kuwa watazitoa fedha hizo endapo wataridhishwa na matokeo ya uchunguzi wa malipo ya fedha za IPTL kwa Pan African Powers Solution Tanzania Ltd (PAP).

ATANGAZA KUGOMBEA URAIS KIMYA KIMYA

Akizungumzia suala la kugombea urais, Pinda alikiri kuwa mmoja kati ya makada wa CCM waliojitokeza kugombea.

“Kwahiyo ndiyo umetangaza kugombea urais?” aliuliza mtangazaji wa kipindi hicho, Salim Kikeke na ndipo Waziri Mkuu Pinda alijibu: “Rasmi bado, lakini ile kimya kimya ile imekuwa ikiendelea.”

Kisha akaulizwa tena: “Kwahiyo umetangaza kimya kimya?”… “Ndiyo,” alijibu Pinda.

Awali Kikeke alimuuliza kuhusu mtu anayefaa kubeba mikoba ya Rais Jakaya Kikwete baada ya kustaafu.

Huku Pinda akionekana kuzunguka swali hilo, alieleza utaratibu wa kumpata rais tangu kwenye chama na Serikali hadi kweye Uchaguzi Mkuu.

“Mikoba yake inaweza kuvaliwa na yeyote ambaye ataonekana mwisho wa safari na utaratibu ndani ya chama na Serikali yenyewe kama nchi atakayekuwa amepatikana kuwa anafaa,” alisema Pinda na kuongeza:

“Waliojitokeza hadi sasa ni wengi na mimi nawaunga mkono,” Kisha alikatishwa na swali la Kikeke kama na yeye yumo…

“Umesikia kuwa nimo? … Basi kubali na yeye yumo. Lakini wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu…”

Jibu la Pinda lilikatishwa tena na Kikeke akisisitiza jibu la moja kwa moja kama kweli atagombea. Lakini Pinda aliendelea kukwepesha.

“Hawa wote waliojitokeza ni katika jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana,  fanyeni hivyo kwa mwingine na mwingine na mwingine,” alisema Pinda na kuongeza:

“Mwisho wa yote, kura zitakazopatikana kwenye mkutano mkuu kama ni kwa chama kinachotawala na hatimaye, Watanzania watakaojitokeza kupiga kura Oktoba mwakani kutokana na wagombea watakaokuwa wamepatikana kwa vyama mbalimbali, huyo ndiyo atapata urais.”

Wagombea ambao wamejitokeza wazi ndani ya CCM ni mbunge wa Nzega, Khamis Kigwangallah na Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba.

Wanaozungumziwa lakini hawajangaza rasmi ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri Ofisi ya Rais, Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

KATIBA

Kuhusu Katiba inayopendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Pinda alipinga hoja kwamba imeegemea upande wa CCM peke yake bali imezingatia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Si kweli kwa sababu unajua Katiba ile kama ambavyo tumeieleza, sehemu kubwa ya maoni yametokana na ya Tume ya Warioba (Jaji Joseph) kama yalivyo. Michango yote iliyoingizwa pale ni asilimia 20 tukayaingiza kwenye Tume ya Mzee Warioba,” alisema Pinda na kuongeza:

“Kwahiyo kudai kwamba yaliyomo mle ni ya upande mmoja si kweli. Ndiyo maana nikasema jambo hili limekuwa likiwekwa kwa namna ambayo inawafanya watu wachanganyikiwe bila sababu ya msingi.”

Huku akisisitiza kuwa taratibu za kisheria zilifuatwa, Pinda alisema inawezekana kura ya maoni kuhusu Katiba mpya ikafanyika Machi na kisha Uchaguzi Mkuu ifikapo Oktoba mwakani.

“Nchi iko tayari kwa kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu… inawezekana Oktoba,” alisema Pinda.

- Advertisement -

Related Articles

6 COMMENTS

  1. Tatizo hili limekuzwa na Serikali yenyewe. Kwani lilipoibuliwa kwa mara ya kwanza Bungeni, Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikanusha vikali kwamba fedha zile hazikuwa za Umma! Sasa kama kweli fedha hizo hazikuwa za Umma kama AG alivyodai kwanini Wafadhili wachukue hatua hiyo? Na kwa nini basi kama si fedha za Umma Serikali baada ya shinikizo ikubali uchunguzi kufanywa na Mkaguzi na Madhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)? Lakini kama hiyo haitoshi, hivi inaleta picha gani kwa Ofisi yenye hadhi ya juu kama ya CAG kuahidi kwamba ingetumia siku 45 kukamilisha uchunguzi lakini sasa ni zaidi ya siku 200 haijatoa ripoti wala kueleza ni kwa nini imekaa kimya hadi mashikizo haya ya Wafadhili? Sasa katika mazingira kama haya ya u-kigeugeu na usiri katika fedha za Umma kweli tunatarajia Wafadhili waendelee kutumwagia fedha za Walipa Kodi yao? TUJISAHIHISHE.

  2. ENYI VIONGOZI WA NCHI HII MNATUPELEKA WAPI,INASIKITISHA SANA KUONA MPAKA NCHI WAHISAN WATUNISHE MSULI NDIPO MKUBAL KUNYOOSHA MAELEZO MBONA UDHALIMU UMEWAZIDI,PINDA HUNA HATA HAYA KWA MUNGU WAKO ETI UCHUNGUZI UNAFKIRI RICHMOND NA WANAWE TUMEISAHAU.PESA HZ NI MRADI WA SERIKAL AKIWEMO PINDA KWAN KWA USHAHIDI WA KIMAZINGIRA YALIYOMPATA MH.KAFULILA BAADA YA KUHOJI MRADI(PESA) HUU TULISHUHUDIA SOTE.KAMA HAPA IMEMWAGA UNGA WA AG ZANZIBAR BASI VITENDO VYA AG TANZANIA BAADA YA KUHOJIWA PESA ZA ESCROW VILITOSHA AMWAGE UNGA AMA APEWE ONYO KALI.MM NI MNYONGE KAMA WANYONGE WENGINE LAKINI NATAMAN WAFADHILI WAGOME KABISA KUTOA MISAADA KWAN HATUNA FAIDA NAYO.WITO;ENYI WANYONGE WENZANGU ZINDUKENI TUITAFUTE NGUZO YA USWEZI NA KAMA HATUONI KUPOTEA KWAYO TUMSUBIRI MYUNANI(SOCRATE) ATUMULIKIE.TAFAKARI!!!

  3. Wizi kwa Watanganyika ni sehemu ya maisha yao ndio wakawa hawashughuliki wala hawageuki katika kashfa na ufusadi uliokithiri.Wagonjwa wanakufa Ocean Road kwa kukosa dawa watawala wanadai fedha hakuna lakini fedha za kuendesha Bunge zipo,za uchaguzi wa serikali za mitaa zipo,za kura ya maoni zipo.za kuiba kwa ajili ya kampeni ya uraisi 2015 zipo.Watanzania tafuteni madereva wa usafari mwengine uliopo haukidhi mahitaji kwa watanzania masikini.Huu ni mwaka wa 50 tunapelekwa wapi?

  4. Ni AIBU KUU kwa viongozi wa Tanzania kwa jinsi wanavyolinda wezi na mafisadi kwa kiasi kikubwa jinsi hii. Zilipoliwa pesa za EPA sehemu kidogo tu ya pesa hizo zilirudishwa ‘kimya kimya’ Hatujasikia hata mmoja aliyerudishwa amepelekwa mahakamani. Tena kiasi kilichorudishwa hakijulikani kwa usahihi, na haijulikani zilipelekwa wapi. Pesa za radar zilipoliwa waziwazi, wahusika hawakufanywa lolote japo serikali ya Uingereza ilirudisha zile zilizozidi. Ni ushahidi zaidi wa aina gani unatakiwa ili kuthibitisha pesa zimeibiwa kuliko huo wa kurudishiwa pesa na Uingereza? Lakini wahusika wamelindwa tara-ti-bu. Huu wizi wa ESCROW umejulikana waziwazi, mpaka wahisani wamekata misaada lakini waliokula bado wanalindwa. MASIKINI TANZANIA YETU. !

  5. Nafikiri nchi yetu viongozi wake wamekosa uzalendo ule wa akina marehemu Julius Nyerere na Thomas Sankara,hata basi wangemwogopa Mungu wakakumbuka wanyonge wa nchi hii ambao wanataabika hata kwa kukosa hata paracetamol.Nafikiri kuna sababu ya watanzania kuuona ukweli wa hawa viongozi wetu,hivyo itusaidie kutafuta kiongozi/viongozi watakao tusaidia walau kuutambua unyonge wetu watusaidie hata kupat mkate uangukao mezani mwao.

  6. Ama kweli sasa tumefikia mahali pagumu. Ujanjaujanja unafika mwisho. Hii ni aibu kubwa kwa serikali. Inakatisha tamaa jinsi fedha za nchi hii zinavyoliwa bila huruma. Mbunge wa Kigoma alipoibua kashfa hii ya fedha za Escrol alikuwa karibu apoteze maisha. Mpaka sasa ameshtakiwa mahakamani kwa kuibua kashfa hiyo bungeni. Ni aibu kubwa sana Waziri Mkuu kukiri leo kuwa eti suala la IPTL imeitia doa serikali. Lakini yeye alikuwa bungeni wakati wabunge wa chama chake walipotaka kumtundika msalabani Mhe. Kafulila. Kashfa zote zilizoibuliwa bungeni ziliibuliwa na wapinzani na kupingwa vikali na wabunge wote wa chama tawala. Aibu kubwa. Ninaogopa sana kwamba muda si mrefu, amani yetu inaweza ikatoweka haswa kwa kuwa walio madarakani hawapo tayari kukubali mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani yaani kupitia sansduku la kura.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles