30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ndalichako alikoroga

Profesa Joyce Ndalichako*Adaiwa kukiuka sheria kusimamisha vigogo TCU

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, anadaiwa kulikoroga kutokana na uamuzi wake wa kuwasimamisha viongozi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Profesa Ndalichako anadaiwa kuikanyaga Sheria ya Vyuo Vikuu ya Mwaka 2005 na Kanuni zake za mwaka 2013 ambazo zinaipa Tume mamlaka ya kuteua watendaji na kuwawajibisha   inapobidi.

Inaelezwa kwamba majukumu ya Waziri hayahusiani na masuala ya utendaji wa Tume kwa mujibu wa sheria,  ila Tume ina jukumu la kumshauri Waziri katika masuala ya elimu ya juu   nchini na kwingineko.

Sheria hiyo inaeleza kuwa endapo Waziri hataafiki ushauri wa Tume kwa jambo lolote kuhusu masuala ya elimu ya juu, ni budi aeleze kwa maandishi sababu za kutofautiana na ushauri wa Tume.

Hayo yamebainika siku chache baada ya Waziri  Ndalichako, kuwasimamisha kazi vigogo   wa TCU akiwamo Katibu Mtendaji,  Profesa Yunus Mgaya, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kiishweko, Mkurugenzi wa Ithibati, Dk. Savinus Maronga na Ofisa Mwandamizi wa Takwimu, Stambuli Kimboka.

Watendaji hao walisimamishwa Mei 25, mwaka huu  kupisha uchunguzi wa kasoro katika udahili wa wananafunzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha St. Joseph kwenye programu ya Shahada ya Ualimu katika Sayansi.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa awali, Mwenyekiti wa TCU, Profesa Awadhi Mawenya, alipokea barua kutoka kwa Waziri Ndalichako ikimtaka awapumzishe watendaji wakuu wa TCU.

Profesa Mawenya  aliitisha kikao cha dharura cha Tume  kujadili maagizo ya Waziri.

Inaelezwa kuwa kwa mujibu wa  majukumu ya Tume, kikao kiliamua kufuata utaratibu wa sheria na kumwandikia barua Katibu Mtendaji kumtaka atoe maelezo katika  masuala mbalimbali yaliyoainishwa kwenye barua ya Waziri.

Hata hivyo Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa  Mgaya, alijibu maelezo hayo kwa kina katika barua hiyo ya  Mei 14, mwaka huu

Kutokana na majibu yake, kwa mujibu utaratibu uliowekwa na sheria, Tume ilijadili maelezo ya Katibu Mtendaji na kuridhika kwamba hakuna kosa lolote la utendaji na kwamba mengi yaliyotajwa yalishughulikiwa na Tume na Wizara ilihusishwa kwa ukamilifu.

“Hata hivyo kuna jambo la kushangaza kidogo, Waziri anajua sheria na suala hili lilikuwa ndani ya uchunguzi maalumu je, inakuaje anaingilia na kulijadili bila kufuata sheria zilizoanzisha TCU?

“… alisema hasara iliyopata Serikali kutokana na wanafunzi wasiokuwa na sifa ni Sh milioni milioni 700 wakati si sahihi.

“Hapa kuna jambo ambalo lipo limejificha nyuma ila tutaliona tu, watu wamekuwa wakionewa kinyume cha sheria.

“Hawa watendaji wa Rais nini wanafanya zaidi ya kufanya upotoshaji na kusigina sheria,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Baada ya hatua hizo na maelezo kutolewa kuhusu tuhuma hizo zilizoainishwa kwenye barua ya Waziri kwa Mwenyekiti wa Tume, majibu kamili yalitayarishwa na kuwasilishwa kwa Waziri kabla ya hotuba yake Bungeni.

Kutokana na mawasiliano hayo na Waziri Ndalichako, alitakiwa kujibu kwa maandishi kuwa amekubali ama kukataa mapendekezo ya Tume kama inavyotakiwa katika sheria.

Hii ingewezesha Tume kuliangalia suala zima kwa utaalamu na kumshauri Waziri iwapo maoni ya Tume yanakinzana na Sera ya Elimu au la.

“Kutokana na historia ya suala zima la maadili na viwango vibovu vya elimu nchini kwa muda mrefu, haikuwa mwafaka kulijadili suala hili bungeni kabla ya kulichunguza kwa mapana zaidi,” alisema.

Mtoa habari huyo alisema   tatizo hilo kwa msingi limetokana na vigezo vya udahili kwenye programu ya Ualimu katika Sayansi iliyopitishwa na Tume mwaka 2013 na kuendeshwa na Chuo Kikuu cha St. Joseph, Kampasi ya Arusha.

Alisema programu hiyo ilibuniwa  kusaidia kupunguza uhaba wa walimu wa Sayansi nchini na ililenga kudahili vijana waliomaliza kidato cha nne katika masomo ya sayansi na kwa wale wasiosoma sayansi, wawe wamefaulu Hisabati na Baiolojia.

“Huu si utaratibu mpya kwani ulianza tangu mwaka 2013 kwa makubaliano na Wizara ya Elimu. Kutokana na mwongozo mpya wa Wizara, vigezo vya udahili vilibadilishwa kwa kuviongeza kutoka ufaulu wa daraja la nne (division four) kwenda daraja la tatu (division three) ili kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo

“Hatua hizo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba vigezo vya Wizara vinatimizwa kwa kuchukua madaraka ya kudahili moja kwa moja badala ya kukiachia chuo jukumu hilo. Kitendo hiki kilifanyika mwaka 2015 ili kuondoa uhafifu katika masuala ya ufundishaji wa programu hii.

“Hata hivyo Tume ilisimamisha udahili mpya na kukiagiza Chuo kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaishia kwenye ngazi ya diploma ya ualimu wa sayansi.

“Madhumuni ni kuhakikisha kwamba hii programu haiendelei tena  kwa vile  Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) lina uzoefu wa kutosha kusimamia elimu  katika ngazi ya diploma vyuoni, Tume ililishirikisha Baraza kurekebisha mtaala wa programu hiyo  kuwawezesha wanafunzi kumaliza masomo yao kwa ngazi ya diploma ya Chuo cha St. Joseph,” alisema.

Alisemna pamoja na hali hiyo tume ilichambua viwango vya ufaulu wa wanafunzi kwenye  programu hiyo na kubaini wale wanaokidhi vigezo na wale wasiokidhi vigezo vya kudahiliwa.

Alisema yaliyoelezwa na Waziri Ndalichako hayahusiani na utovu wa nidhamu uliosababisha Waziri kuchukua hatua kali za kuivunja Tume na kuwaadhibu watendaji hata kabla ya matokeo ya uchunguzi wa Kamati aliyoiteua.

Mei 25, mwaka huu Profesa Ndalichako, alitangaza kumsimamisha kazi Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa  Mgaya, kwa kile alichodai ameshindwa kuisimamia  shughuli za TCU   na  wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.

Inaelezwa kuwa  Waziri Ndalichako alichukua uamuzi huo   kwa kumshauri Rais Magufuli moja kwa moja badala ya kusubiri maagizo na ushauri wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa  Zambia kwa shughuli za  kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles