24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mbuzi wa tambiko aua watu watano wa familia moja  

NA WAANDISHI WETU
VILIO, simanzi na hofu vimetanda kwa wakazi wa Kitongoji cha Lotii, Kijiji cha Mwitikira, Tarafa ya Olboloti, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara baada ya watu watano wa familia moja kufariki dunia kwa namna ya kutatanisha.

Watu hao wanadaiwa kufikwa na mauti baada ya kula nyama ya mbuzi iliyotolewa kutekeleza mila ya kutatua mgogoro uliojitokeza katika familia mbili zilizopo Kijiji cha Kaachini kilichopo wilayani humo.

Akisimulia tukio hilo la aina yake kijijini hapo, mmoja wa majirani wa familia hiyo, Juma Kijaji, aliliambia  MTANZANIA kwa simu jana kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi kati ya familia ya Kilangazi Mbao na majirani zao (majina tunayo).

Kijaji alisema kuwa awali familia hizo zilikubaliana kulipana mbuzi baada ya kutofautiana katika masuala kadhaa kulingana na mila na desturi za jamii yao.

Alisema baada ya siku sita, walikubaliana mbuzi huyo achinjwe na nyama hiyo igawanywe kwa majirani wengine katika kitongoji hicho.

“Hata hivyo siku chache baadaye kulizuka uvumi kijijini hapa kwamba nyama hiyo haikupaswa kuliwa na familia ya Mzee Mbao, jambo ambalo lilifuatiwa na vifo vya mfululizo kutoka familia hiyo,” alisema.

 

MWENYEKITI WA KITONGOJI

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Ally Msambo, aliieleza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto kuwa kabla ya vifo hivyo, wanafamilia hao walivimba mwili mzima.

Msambo aliwataja wana familia waliotangulia kufariki dunia kuwa ni watoto wawili, Juha Mbao (3) na Mwajuma Mbao (5).

Alisema siku moja baadaye babu yao, Chirangas Mbao naye alipatwa na ugonjwa huo huo wa ajabu na kufariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.

Katika mfululizo huo wa vifo, mtoto mwingine, Agnes Mbao naye alipoteza maisha na kufuatiwa na baba yake Chilangas Chilangas aliyefia katika kitongoji hicho baada ya kutoroka hospitalini na kukamilisha idadi hiyo ya watu watano wa familia moja kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

Mwenyekiti huyo wa kijiji aliiambia kamati hiyo kuwa baada ya wanakijiji kushtushwa na vifo hivyo, walikubaliana kutozika miili ya mtoto na baba yake hadi kwanza wapate ufumbuzi wa kiini cha vifo hivyo.

 

MKUU WA WILAYA

Akisimua tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, alisema hali hiyo imesababisha wananchi kuingiza imani za kishirikina kwa kudai kuwa kuna kitu kimefanywa ili kiweze kuwadhuru wanafamilia hao.

Alisema tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji hicho.

Nzoka ambaye alikiri kuwapo kikao hicho cha upatanishi, alisema mama mmoja ambaye mumewe na watoto wake walifariki katika tukio hilo, alienda kukopa mbuzi kwa jirani yake ambaye ni Mmasai.

Baada ya kupata mbuzi huyo, alitakiwa amchinje ili wananchi waliojitokeza kwenye kikao kilichokuwa kinafanyika kijijini hapo wale ile nyama.

“Baada ya kula nyama hiyo, mtoto wa mama huyo alifariki, siku iliyofuata alifariki mtoto mwingine na siku ya tatu alifariki baba mdogo wa watoto hao,” alisema Nzoka.

Alisema wananchi walichukua maiti hizo na kwenda kuzika, lakini baadaye alifariki mtoto mwingine wa familia hiyo.

“Siku iliyofuata (juzi) alifariki baba mzazi wa watoto hao, hali iliyosababisha kujitokeza kwa hofu kwa wananchi wa kijiji hicho na kudai kuwa mbuzi huyo amefanyiwa mambo ya kishirikina ili watu wa familia hiyo waweze kufariki.

“Nilikwenda jana (juzi) mimi na timu yangu ya madaktari kutoka wilayani kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo,” alisema Nzoka.

Alisema baada ya kuzifungua maiti, zilikuwa zimevimba sana hivyo madaktari walizifanyia upasuaji kwa kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa madaktari ambaye alihusika kufanyia uchunguzi maiti ya watoto wawili waliofia hospitalini, alisema mapafu yalikutwa yameharibika.

 

VIFO VINGINE FAMILIA MOJA

Kutoka mkoani Mara, watoto wanne wakiwamo watatu wa familia moja wamekufa maji katika matukio mawili tofauti yaliyotokea ndani ya wiki moja Manispaa ya Musoma na wilayani Butiama.

Watoto watatu wa familia moja walikufa maji katika Kijiji cha Mirwa wilayani Butiama baada ya kunasa kwenye tope wakiwa wanaogolea kwenye mto Mei 9, mwaka huu, saa 8 mchana.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Leonard Chacha, aliliambia MTANZANIA kuwa watoto hao waliokuwa wakiishi na mama yao, Mtabutwa Cherehani, waliondoka nyumbani kwa lengo la kwenda kuoga mtoni.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Wambura Kizengo (11) mwanafunzi wa darasa la tano, Dismas Kizengo (7) mwanafunzi wa darasa la kwanza, wote katika Shule ya Msingi Mirwa na Mkirya Kizengo (4) mwanafunzi wa chekechea.

Chacha alisema baada ya kupata taarifa za watoto kupotelea mtoni, ilipigwa ngoma kwa ajili ya kuwakusanya wananchi kwa lengo la kwenda kuwakoa, lakini walipofika mtoni walikuta tayari wamefariki dunia.

Diwani wa Kata ya Mirwa, Pitalis Odero, alisema wamesikitishwa na vifo vya watoto hao.

Katika tukio jingine lililotokea Manispaa ya Musoma, mvua iliyoambata na upepo mkali iliyonyesha juzi jioni, imesababisha kifo cha mwanafunzi Benaderta Aley (12) aliyekuwa anasoma darasa la pili Shule ya Msingi Kamnyonge.

Kaka wa mwanafunzi huyo, Delta Aley, alisema mdogo wake akiwa na wenzake walikwenda kusaga mashineni, wakati wanarudi mdogo wake alianguka kwenye mtaro uliokuwa unapitisha maji kwa kasi na kusombwa.

Alisema mwili wa marehemu ulipatikana baada ya siku mbili ukiwa umbali wa kilomita mbili.

Habari hii imeandaliwa na MOHAMED HAMAD, MANYARA NA PATRICIA, KIMELEMETA, DAR ES SALAAM, SHOMARI BINDA, MUSOMA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles