30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Vicky Kamata adakwa polisi

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata

MBUNGE wa Viti Maalumu, Vicky Kamatta (CCM), amekamtwa na Polisi Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kuwatumia ujumbe mfupi wa simu za matusi wabunge wenzake.

Chanzo ncha kuaminika kutoka mjini Dodoma kiliambia MTANZANIA kuwa kwa kipindi cha miezi kadhaa Vicky amekuwa akituma sms za matusi kwa wabunge wenzake wa viti maalumu kupitia CCM, Catherine Magige na Lucy Mayenga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui.

Taarifa zaidi zinasema kuwa wabunge hao walikuwa wakitumiwa sms za matusi kwa namba 0653 762 *** ambapo baada ya kuona hali imekuwa ikizidi waliamua kwenda kufungua jalada la malalamiko katika Kituo Kikuu cha Kati mjini Dodoma na kuomba ufanyike uchunguzi ili waweze kumbaini mwenye namba hizo.

Kutokana na maelezo hayo, Jeshi la Polisi lilianza kufanya uchunguzi kuhusu sakata hilo na kubaini namba hiyo imesajiliwa kwa jina la mdogo wa kiume wa Vicky.

Baada ya Jeshi la Polisi kufuatilia, ilibainika namba hiyo ilikuwa ya mbunge huyo ingawa hakuisajili kwa jina lake.

Uchunguzi zaidi ukabaini kuwa sms za matusi alizokuwa anatuma, pia alikuwa akitoa taarifa kwa mwenye namba 0767 500***, akimweleza namna anavyopambana na wabunge wenzake kwa kuwatukana.

Habari zinapasha kuwa polisi wamekuwa wakifuatilia suala hilo kwa muda licha ya kuwa mara nyingi namba hiyo huwa imezimwa.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa Septemba 28, mwaka huu polisi waliokuwa wanachunguza suala hilo walifanikiwa kuipiga namba hiyo na kupokewa.

Chanzo cha habari kinaeleza kuwa baada ya namba hiyo kupokewa aliyepokea aliulizwa ni wapi alipo na kama inawezekana afike kwenye viwanja vya Bunge kuchukua mzigo wake.

“Aliambiwa hivyo kwa sababu SMS ya kwanza inasemekana kuwa ilitumwa na mtu aliyekuwa kwenye viwanja vya Bunge, na yule kijana aliyepokea simu bila kujua aliwaelekeza polisi nyumbani kwao akisema ndipo alipo mwenye simu.

“Polisi walipofika huko walimtaka kijana aliyekuwa nyumbani apige ile namba na akapokea yule kijana aliyewaelekeza polisi,” alisema.

Wakiwa wanafanya uchunguzi askari polisi waliipiga simu 0767 500*** ambapo ilipokewa na kigogo mmoja wa ngazi za juu serikalini ambaye baada ya mahojiano alitakiwa afike kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.

Kigogo huyo baada ya maelezo alimtaka askari anayefanya upepelezi wa kesi hiyo kuwa mvumilivu kwani muda ambao alikuwa akihitajika kituoni isingiwezekana kutokana na kuwa anapiga kura bungeni kuhusu Katiba Mpya.

Chanzo hicho kilisema pamoja na majibu hayo, mpelelezi huyo aliingiwa na hofu baada ya kutajiwa jina la kigogo huyo wa ngazi za juu serikalini.

CATHERINE MAGIGE

MTANZANIA ilipomtafuta mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM), alikiri kupokea matusi na kufungua kesi katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati mjini  Dodoma.

Alisema Septemba 2, mwaka huu alipokea matusi kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi hali iliyomshitua na kuamua kuizima ili isitumiwe tena kumpigia wala kutuma sms.

Alisema kuwa baada ya kuzungumza na baadhi ya watu walimshauri kufungua kesi polisi ili uchunguzi ufanyike na anayetuma matusi hayo akamatwe.

Alieleza kuwa Septemba 3, mwaka huu alikwenda Kituo Kikuu cha Polisi Kati Dodoma na kufungua jalada la kesi dhidi ya mtu huyo aliyekuwa akimtukana kwa sms.

“Nilipokuwa pale polisi sasa ndiyo nikaifungulia ile namba na kumbe kuna sms nyingine zilikuwa zimeshatumwa zikawa zinaingia kwa fujo.

“Ukijaribu kuangalia unaona sms ya kwanza ilitumwa na mtu akiwa kwenye eneo la viwanja vya Bunge, nyingine Naam Hotel na nyingine maeneo ya Uwanja wa Ndege hapa hapa Dodoma,” alisema Magige.

Alisema kuwa tangu hapo polisi waliendelea na uchunguzi wa suala hilo na jana alipata taarifa kuwa washukiwa wao wamekamatwa.

“Hii simu inaonekana kazi yake kubwa ilikuwa ni kututukana sisi na wakati mwingine kuongea na kutuma sms kwa (jina tunalihifadhi), kwa mfano usiku wa Septemba 28 inaonekana kwamba simu hiyo iliongea kwa sekunde zaidi ya 1,300 (dakika 21.6), na sijui walikuwa wanaongea nini.

“Kwa kweli mimi hata sielewi tumefika wapi kama viongozi tunaweza kuwa tunatumia simu kutukanana hivi,” alisema.

LUCY MAYENGA

Kwa upande wake Lucy Mayenga, alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema amekuwa akitukanwa kwa njia mbalimbali za mtandao kwa takribani miezi minne sasa.

Alisema kuwa baadhi ya matusi yalipitishwa kwa watu wake wa karibu jambo ambalo lilimfanya aumie, lakini asijue cha kufanya.

Alisema kuwa Septemba mbili alivyoanzwa kutukanwa Magige, baadhi ya sms zilizokuwa na matusi zilimtaja pia Catherine.

“Sasa tukaongea na Lucy mimi wakati huo sikuwa Dodoma na tukashauriana pia na watu wengine ndipo alipoamua kufungua kesi.

“Nilivyokuwa natukanwa mimi nilikuwa sina muda wa kufuatilia na niliona ni kama nitu kitapita tu ndiyo maana sikufuatilia, sasa ilivyohamia kwa Catherine na huko nikawa natajwa na mimi pia, nikaona hapa sasa imefika mbali,” alisema.

KAULI YA VICKY

Akizungumza tuhuma hizo, Vicky alisema anashangazwa na taarifa za kukamatwa kwake kwani muda wote yeye alikuwa nyumbani kwake na hakuna jambo kama hilo.

“Mimi silijui suala hilo… Sijakamatwa na muda huu nipo hapa nyumbani kwangu na sasa ninajiandaa ili nirudi tena katika vikao vya Bunge,” alijibu kwa kifupi Vicky.

JESHI LA POLISI

Akizungumza sakata hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, awali alisita kidogo na baadaye alisema hakuna taarifa zozote katika mkoa wake za kukamatwa kwa mbunge huyo huku akitaka kujua taarifa hizo zimetoka wapi.

“Nani kakwambia masuala hayo… hakuna taarifa kama hizo, hatujamkamata mbunge yeyote usiku huo wa jana,” alisema Kamanda Misime.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles