30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Sukari kaa la moto

pombe* Magufuli awatangazia vita wafanyabiashara CCM, ChaAsema haogopi CCM, wala Chadema

 * Profesa Semboja adai Rais amekiuka mkataba wa kimataifa

* Dk. Slaa asema sukari yaweza kuing’oa Serikali

 

Na Waandishi Wetu

KATIKA lugha ya kawaida suala  la sukari linaloendelea nchini linaweza kufananishwa na ‘kaa la moto’ kutokana na kughubikwa na mambo mengi, huku serikali ikijitahidi kwa kila njia, kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana.

Rais John Magufuli kwa mara nyingine amezungumzia uhaba wa sukari kwa kuitaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujielekeza kwenye uwekezaji katika sukari.

Rais alitoa kauli hiyo jana alipozindua majengo makubwa ya vitega uchumi yaliyojengwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF eneo la Corridor,   Arusha jana.

“Angalieni wananchi wanavyotaabika leo, kisa watu wachache wameficha sukari.

“Mngekuwa mmewekeza kiwanda cha sukari tusingekuwa na tatizo hili, sasa nawaomba mbadilike kwa ajili ya Watanzania,”alisema na kuongeza:

“Kama mtaamua kununua sukari nitafurahi, kuna kundi la wafanyabiashara wachache wanaouza sukari watakavyo, hili hatutalikubali kwa sababu  wapo wanaokwenda Brazil kuleta sukari iliyoharibika.

“Hawa wanaleta hapa na kuwauzia Watanzania bila kujali madhara kwa afya watakayopata. Wafanyabiashara wa aina hii sitaenda nao, awe kutoka CCM, Chadema, CUF au kokote, kwangu ni mkong’oto tu”.
Rais  alitahadhalisha kuwa iwe mara ya mwisho kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini kumualika kuzindua majengo makubwa ya biashara badala yake wamualike katika uzinduzi wa viwanda.

“Majengo haya yamegharimu zaidi ya Sh bilioni 60, tujiulize hawa wananchi waliosimama hapa hawana ajira wananufaikaje na haya majengo, majengo mengi ya mifuko ya hifadhi hayana wapangaji, hili nalijua.

“Sijasema  mmefanya vibaya kuyajenga kwa kweli leo siwapongezi kwa asilimia 100, lakini kama mkinialika kufungua mlipowekeza kwenye viwanda nitawapa hizo asilimia zilizobaki.

“Viatu tunavyovyaa vinatoka nje ya nchi, PPF na NSSF mngeamua kufungua kiwanda cha ngozi, leo kwenye uzinduzi huu mngekuwa mnaandikisha vijana kwa ajili ya ajira.

“Tuna mifuko saba ya Hifadhi ya Jamii nchini na inachangia pato la taifa kwa asilimia 12, wakati nchi nyingine sekta hiyo inachangia pato la taifa kwa asilimia 40,” alisema Rais Magufuli.

Profesa Semboja amkosoa

Mtaalam wa Masuala ya Uchumi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Semboja Haji amekosoa msimamo wa Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati soko la sukari nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari     katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dar es Salaam jana, Profesa Semboja alisema msimamo huo wa Rais  ni kinyume na makubaliano ya mkataba wa kimataifa juu ya bidhaa hiyo.

Alisema soko la sukari halipaswi kuingiliwa na  haikuwa busara kwa Rais Magufuli na Serikali yake kuliingilia kwa sababu kitendo hicho kinaishtua dunia nzima.

“Sukari ni bidhaa muhimu katika maisha ya mwanadamu, kufanikisha matumizi yake mbalimbali hasa majumbani na viwandani ambako mara nyingi hutumika katika kutengeneza vinywaji mfano soda, hivyo ni bidhaa inayopaswa kutazamwa mno.

“Tunajua kila nchi ina bodi ya sukari ambayo inatambulika kimataifa, bodi ina mamlaka ya kusimamia kuanzia uzalishaji, uuzwaji na soko kwa ujumla.

“Lakini   tangazo lile la kwanza la Serikali lilionyesha wazi kuingilia soko hilo. Duniani ukiingilia soko la sukari kila nchi inashtuka kwa sababu kuna makubaliano,” alisema.

Akitoa mfano, Profesa Semboja alisema: “Yaani ni sawa na mpira, wachezaji wako uwanjani… upande mmoja unafunga goli lakini kocha (Serikali) ambaye yupo nje ya uwanja anapinga na kusema kuwa lile si goli…. wakati refa (bodi) ndiyo yupo uwanjani akisimamia mchezo huo.

“Kwa maneno mengine ni kwamba Serikali imesema wale watakaobainika kuwa wameficha sukari watashughulikiwa kwa kupelekwa mahakamani, lakini hii ni kinyume cha sheria kwani wanapaswa kupelekwa mbele ya bodi   wahojiwe kwanza”.

Alisema wafanyabiashara hao wanapaswa kuhojiwa na bodi kwanza kabla ya kupelekwa mahakamani  kujua sababu zilizowafanya kuweka bidhaa hiyo ndani na si kuipeleka sokoni.

“Huwezi kujua kwa nini wameiweka ndani kwa sababu huenda mfanyabiashara amekubaliana na mteja kwamba afike kuichukua  akaisambaze lakini leo unakwenda kuikamata bila kumhoji,” alisema.

Alisema ingawa sukari ya Tanzania inapendwa zaidi nje ya nchi lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa wakihakikisha kuwa soko la ndani limejitosheleza ndipo wanapoiuza nje ili kupata faida.

“Hata ningekuwa mimi ndiyo mfanyabiashara ni wazi kwamba ningependa nipate faida lakini kwanza makubaliano ni kwamba lazima soko la ndani litosheleze ndipo bidhaa iende nje na haya ni makubaliano ya  mataifa na si  taifa.

“Hii inamaanisha kuwa soko la sukari si la nchi moja ni la ushirikiano… ndiyo maana inapotokea nchi moja imeishiwa sukari nchi nyingine hulazimika kwenda kuisaidia kwa kuiuzia bidhaa hiyo,” alisema.

 

Dk. Slaa: Sukari inaweza kuangusha serikali

Naye Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa amesema sukari ikikosekana katika Taifa lolote kwa   wiki moja tu, Serikali husika inaweza kuanguka.

Amesema sukari ni sawa na mahitaji mengine muhimu katika maisha ya binadamu, hivyo ni vigumu kuitenganisha na siasa.

Akizungumza na MTANZANIA akiwa  Canada anakoishi hivi sasa, Dk. Slaa alisema sukari ni mahitaji muhimu kwa binadamu kwa kuwa watu wengi asubuhi hupata kikombe cha chai ambayo lazima itumie sukari.

“Sukari kama ulivyo mkate, nyama, unga na mchele ni mambo muhimu katika maisha ya watu wengi na hivyo huwezi kutenganisha na siasa, ikikosekana kwa wiki moja tu, Serikali inaweza kuanguka,” alisema.

 

Dk. Slaa ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Karatu mkoani Arusha, alisema serikali makini haiwezi kukaa kimya au kupuuzia upungufu au hujuma yoyote katika jambo muhimu kama sukari.

“Hatutaki kurudi kwenye kipindi cha RTC-Kampuni za Biashara za Mikoa (Katika miaka ya 1980 ambako kulikuwa na mgao wa bidhaa muhimu).

“Lakini pia itakuwa Serikali ya ajabu itakayoruhusu watu wachache kuhujumu serikali kwa kuficha bidhaa muhimu na kutengeneza au kuongeza makali ya upungufu wa hitaji hilo muhimu,”alisema.

 

WAPINZANI

Nayo Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imesema kuadimika kwa sukari nchini kumesababishwa na uamuzi wa kukurupuka wa Rais John Magufuli kuzuia uingizwaji wa sukari nchini bila kufanya tathimini.

Imesema kama lengo lilikuwa ni kulinda viwanda   nchini asingezuia sukari pekee kwa sababu viwanda vipo vya aina mbalimbali na bado bidhaa zinaingia kutoka nje nchi.

Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu  alisema Rais Magufuli alipaswa kutafakari kabla ya kupiga marufuku bidhaa hiyo nyeti inayotumiwa na kila familia nchini.

Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema) alisema hatua hiyo ya mkuu wa nchi inaweza kuogopesha wawekezaji  kuwekeza nchini.

“Wawekezaji wanataka kuwekeza katika nchi inayoheshimu sheria na si kuendeshwa kwa  matamshi na amri, wengi wanahofia kupoteza mitaji yao.

 

Serikali yakamata sukari Kilombero

Wakati huohuo, Serikali imekinyang’anya Kiwanda cha Sukari Kilombero tani 622.4 za sukari zilizokuwa zimehifadhiwa  kiwandani hapo  na mjini Morogoro.

Sukari hiyo ilikamatwa jana katika oparesheni maalumu iliyoitwa ya kusaka wahujumu uchumi wa bidhaa hiyo mkoani humo.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe.

Alitaja ambako sukari hiyo ilikuwa ‘imefichwa’   kuwa ni  katika  Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (K1) tani 429, Kilombero (K2) tani 135   na mjini Morogoro  tani 58.4.

Dk. Kebwe alisema sukari yote ilibainika ni  mali ya Alneem Enterprises.

Wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola alisema makachero wa taasisi hiyo wakishirikiana na wenzao wa Jeshi la Polisi walikamatwa tani 4,579.2 za sukari iliyofichwa katika maghala ya mfanyabiashara, Haruni Daudi Zacharia.

Katika taarifa yake   mwishoni mwa wiki iliyopita, Mlowola alieleza kuwa shehena hiyo ya sukari ilikamatwa Mei 5.

Alisema  uchunguzi ulibaini kuwa ni mali ya Kampuni ya Al-Naeem inayomilikiwa na Zacharia na   ilinunuliwa katika Kiwanda cha Sukari Kilombero.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles