26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sheria yaja kutenga siasa, biashara

job ndugai*Tume ya maadili kupeleka muswada bungeni

*Wabunge wapinga,wasema wanalipwa kidogo

 

Na Elizabeth Hombo, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amewatangazia wabunge kuwa Tume ya Maadili na Utumishi wa Umma inatarajia kupeleka muswada wa sheria bungeni kwa ajili ya kutenganisha biashara na uongozi.

Ndugai, alitoa kauli hiyo  Dodoma jana  alipozungumza   kwenye semina ya kwanza ya   wabunge wanachama wa  Chama cha Wabunge Wanaopambana Rushwa (APNAC) katika Bunge la 11.

“Ninaomba niwaarifu jambo muhimu na ninaomba mnisikilize kwa makini. Nimepata ujumbe kutoka Tume ya Maadili na Utumishi wa Umma inayoongozwa na Jaji Salome Kaganda  kwamba wana nia ya kuleta muswada wa sheria bungeni wa kutenganisha uongozi na biashara.

“Muda si mrefu nitawaalika waje watoe semina au watoe maelezo kwa wabunge wote   muweze kuielewa vizuri.

“Sasa wale wenzangu ambao ni wavivu kusoma, wasome sheria hiyo na kuielewa kwa sababu ubunge wetu tunauchanganya na biashara ili mambo yaende sawasawa.

“Wale ambao tumezoea  kusema ndiyoo…naomba sheria hii ikija muisome kwa makini na muelewe maana wengi wetu wabunge tumekuwa tukichanganya na biashara ili kuweka mambo sawasawa.

“Unaweza kupitisha sheria halafu ukaendelea na biashara, hapo utakuwa umejiweka pabaya,”alisema.

Aliwatahadharisha wabunge ambao wamekuwa wakiunga mkono na kupitisha sheria mbalimbali kuwa makini kuhusu sheria hiyo.

Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema katika nchi zilizoendelea imekuwa ni kawaida   mfanyabiashara anapokuwa mbunge anakabidhi biashara kwa mtu mwingine.

“Nchi zilizoendelea unakabidhi biashara kwa mtu halafu unaendelea na ubunge lakini sisi hapa kwetu imekuwa ngumu. Hivyo naomba msome hiyo sheria vizuri tuielewe. Ni sheria nzuri kwa sababu   malengo yake ni mazuri.

“Sasa sisi waswahili tulivyo… kumkabidhi mtu biashara yako kwa miaka mitano ni jambo gumu na baada ya miaka hiyo mitano kuisha unaweza ukaendelea mpaka 20 ukiwa bungeni hivyo kukaa miaka yote halafu unarudi unamwambia aah mzee vipi biashara yangu imefikia wapi hapo,”alisema.

Aliwaasa wabunge kuwa makini na vishawishi vya rushwa na kwa vile nafasi zao ni nyeti wafanye kazi kwa unyoofu.

“Nafasi tulizonazo ni nyeti, kwa mwenendo wa Serikali ya awamu ya tano yawezekana kabisa wakawapo watu ambao wanaona umakini huu maslahi yao na hivyo wakaona njia pekee ni kuwarubuni, nawaasa msishawishike,”alisema Ndugai.

Aliwataka kuwa mfano katika jamii kwa kudhibiti rushwa kwa kuwa wabunge ndiyo wanaopitisha sheria mbalimbali.

“Mna wajibu wa kudhibiti rushwa na kuwa mfano katika jamii na mna jukumu la kupitisha sheria ya kupiga vita rushwa kwa miswada inayopita bungeni.

“Mnavyopitisha bajeti ya serikali mhakikishe vyombo vinavyopambana dhidi ya rushwa vinatengewa bajeti ya kutosha,”alisema Ndugai.

Alimkumbusha  Waziri wa Utawala Bora Waziri wa Ofisi ya Rais,Tamisemi,Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki kuwa wabunge wanakumbwa na ukata mkubwa hivyo Serikali iwaangalie kutokana na majukumu waliyonayo.

“Najua mna pressure kutoka kwa wananchi kuwapa fedha, kuchangia harusi, misiba, kununua madawati, kulipa ada ya wanafunzi hivyo kutokana na hilo mnajikuta ni hohehahe na inabidi sasa ahangaike huku na kule na baadaye kujikuta anaingia kwenye kona mbaya.

“Tatizo jingine ni mikopo ya benki yenye riba kubwa nayo inawasumbua sana wabunge wangu na inawaweka katika mazingira magumu.Naomba hili pia litazamwe.

“Pia ukata kwa ujumla wake na waziri uko hapa…naomba nikwambie kwamba wabunge hawa hawako vizuri, kuna haja ya kuweka mambo yao vizuri. Maana huwezi ukampa mtu madaraka halafu mfukoni hana kitu na ana majukumu mazito,”alisema.

Waziri   Kairuki aliwataka wabunge kuwa sehemu ya kupambana na rushwa na   kila mmoja kwa nafasi yake awe msafi.

“Ifike wakati hata tusilaumiwe kwa sababu kitendo cha kutumiwa tu inaleta shaka. Hivyo chombo hiki kiendelee kuchangia mapambano ya rushwa na tutaleta sheria bungeni,”alisema Kairuki.

Alisema adhabu ambayo inatolewa kwa wahusika haiendani na hasara ambayo taifa linapata.

“Kama serikali tutahakikisha watoa taarifa tunawalinda na tutahakikisha TAKUKURU inakuwa huru,”alisema.

Akitoa mada katika semina hiyo, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Davis alisema bado rushwa ni tatizo nchini kwa kuwa inafanywa kwa usiri.

“Rushwa ni makubaliano kati mpokeaji na mtoaji hivyo ni ngumu kuwabaini na rushwa kubwa inafanywa na wanasiasa na wale wenye uwezo  wa uchumi,”alisema.

Alisema adhabu ya wale wanaokamatwa na rushwa bado ni ndogo na imekuwa ikilalamikiwa kwa sababu haiendani na kosa.

“Na rushwa kama haijaondoka kwenye mawazo ya mtu hata tukiwa na sheria ni bure. Cha kufanya ni lazima lianzie kwa wabunge wenyewe na tusiwe na ujasiri wa kuwanyooshea vidole wengine bali tujiangalie wenyewe kwanza,”alisema.

Akichangia mada katika semina hiyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM) alisema ni kesi nyingi za mafisadi ambazo zimelepekwa mahakamani lakini wanapewa muda mchache.

“Mshahara wa mtu unajulikana, halafu mnasema kukamata rushwa kubwa ni ngumu, itungwe sheria ajieleze hizo mali kapata wapi.

“Na wako ambao wamepelekwa mahakamani  lakini kesi za wengine haijulikani zinaishia wapi kwa sababu wengine wanahonga.

“Hivyo kinachotakiwa kutungwa sheria, aitwe ajieleze akishindwa kujieleza anyang’anywe mali zake na apelekwe jela,”alisema Keissy.

 

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alisema kitendo cha kutenganisha biashara na uongozi kwa   wabunge ni ngumu kwa sababu mishahara na marupurupu yao madogo.

“Kwa nchi yetu haiwezekani. Kwa sababu ukiangalia mishahara, marupupu kwa nchi hizi za Afrika Mashariki (EAC) Tanzania ni ya mwisho. Ukizungumza hivyo mtu asiwe na kitu chochote cha kumwingizia kipato ni ngumu na haiwezekani.

“Mfano; mshahara wa mbunge wa Kenya uko zaidi ya mara 10 ya mbunge wa Tanzania na bado anafanya kazi zake. Mbunge ni mtu ambaye hayuko juu ya sheria ingawa anatunga sheria,”alisema Shabiby.

 

Aeshi Hillaly

 

Naye Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillaly alisema kwa hali ilivyo hivi sasa, ni vigumu kumtenganisha mbunge na biashara na  ni jambo lisilowezekana.

 

Paresso

Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso (Chadema), alisema hajajua maudhui ya muswada huo hivyo akiusoma ndiyo  atajua.

“Uletwe tuusome lakini ni vigumu kwa hali ya sasa kumtenganisha mbunge na biashara,”alisema.

 

Kikwete

Mwaka 2008, Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa mara ya kwanza alitangaza kutenganisha siasa na biashara.

Alisema upo ushahidi wa migongano ya maslahi kwa baadhi ya wabunge na mawaziri ambao ni wafanyabiashara na wanasiasa, jambo ambalo huweka katika mazingira magumu ya utendaji.

“Nchi za wenzetu hasa zile za kibepari zinazo taratibu nzuri za kushughulikia hali hizi… taratibu unaomtaka mtu mwenye shughuli za biashara anapokuwa mbunge au waziri kuacha kujishughulisha na biashara zake.

“Unakuwapo utaratibu rasmi unaotambuliwa kisheria wa wadhamini wanaoendesha hizo shughuli bila ya yeye kujihusisha nazo. “Anapoacha uongozi wa siasa kama atapenda atachukua tena mali yake na kuendelea na shughuli zake.

“Ni makusudio yangu kuwa utaratibu huu tuuanzishe hapa nchini. Viongozi wetu wachague kufanya jambo moja kwa wakati mmoja ama biashara au ubunge na uwaziri.

“Kwa ajili hiyo ni makusudio yangu kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Uongozi ili tuingize utaratibu huo,”alisema Kikwete.

Alisema ni  jambo lenye maslahi kwa taifa na litasaidia  kujenga heshima ya viongozi wa umma mbele ya macho ya wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles