31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani legelege huchochea chama tawala kuwa fisadi

mbowe1MWAKA 1990 ulinukuliwa ukisema kwamba unafikiri kutokuwapo kwa chama cha upinzani kulichangia chama tawala nchini Tanzania kutelekeza uwajibikaji wake. Je, unafikiri ilikuwa ni makosa kwa mataifa huru ya Afrika kuchagua Serikali za chama kimoja?

‘‘Kamwe sikutetea hili kwa kila nchi, lakini nilifanya hivyo nchini Tanzania kutokana na sababu zetu za msingi. Hata hivyo mwaka 1990 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliondoa mfumo wa Serikali ya chama kimoja na kuwa mfumo wa vyama vingi

“Jambo la msingi ambalo nililifanya wakati nikitoa maelezo yangu nilisema kwamba chama chochote kikikaa madarakani kwa muda mrefu  hupoteza misingi yake na kuwa fisadi.

‘‘Chama cha Kikomunisti cha Urusi, CCM ya Tanzania na chama cha Kihafidhina cha Uingereza vyote vimekaa madarakani muda mrefu na vimekuwa fisadi na hii wakati mwingine inatokana na udhaifu wa upinzani au kutokuwapo kabisa kwa upinzani.’’

Hiyo  ilikuwa ni sehemu ya  mahojiano kati ya Mwandishi wa habari, Ikaweka Bunting na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyochapishwa Januari 1, 1999.

Kwa mtazamo huu wa Mwalimu Nyerere unaweza kujiuliza hivi  ni kweli ilikuwa nia yake kutoka moyoni kwamba Serikali ibadilishe mfumo kutoka chama kimoja  au alisema hivyo baada ya kusoma upepo wa shinikizo la kimataifa hasa nchi wahisani kwamba bila kubadilisha mfumo misaada itayeyuka?

Kama ndio  ulikuwa  mtazamo wa Mwalimu kwamba nchi ibadilishe mfumo maana chama kilichoko madarakani kimekuwa fisadi kutokana na kukaa muda mrefu,  mbona yeye hakubadilisha mfumo huo akingali madarakani  ukizingatia  alikaa muda wa miaka 24 ambayo si haba?

Ni takribani miaka 24 tangu nchi yetu ibadilike kutoka  mfumo wa chama kimoja hadi vyama vingi. Mabadiliko ambayo  hapo awali Watanzania walipoulizwa kwenye maoni  ni mfumo upi wanaupenda,  asilimia 80 walipendelea kuendelea na mfumo wa chama kimoja.

Watanzania kutokukubaliana na mabadiliko inawezekana ni matokeo ya kisaikolojia kwamba mwanadamu huwa ni mwoga kupokea jambo jipya ambalo hajui hatima  yake  au ni sababu  ya kukaa na chama kimoja kwa muda mrefu huku wakiendelea kumwamini  Baba wa Taifa.

Kwenye kitabu cha ‘‘The Psychology of Lean Improvent: Why Organizations must overcome Resistance and change the Culture’’  kilichoandikwa na Chris A. Ortiz mwaka 2012 katika  ukurasa wa 30 anasema kwamba  ili kuepuka  jamii kukataa mabadiliko inabidi pawepo uhamasishaji, maombi ya uwazi, kiongozi kuwa nyuma ya watu wake pamoja na mawasiliano bora.

Ni katika muktadha huu wananchi walibadilisha uelekeo  na hatimaye kuanza safari ya mfumo mpya japo wengi wao waliendelea kuwa na hofu huku wakiwachukulia wenzao wanaoingia vyama pinzani  kama  wasaliti au waleta vurugu.

Kwa kutumia  hofu  ya wananchi  iliyojengeka kwenye mtazamo hasi baadhi ya wanasiasa kutoka CCM wakati wa  kampeni  kipindi cha uchaguzi wamekuwa wakiwalaghai kuwa wasichague upinzani kwani nchi inaweza kuingia kwenye machafuko.

Hata hivyo wananchi wamekuwa wakipuuzia  na kuona vyama pinzani vina  manufaa hasa baada ya vyama hivyo  kuibua  vitu  vyenye maslahi ya jamii mfano masakata ya ufisadi. Ni katika hali hii kura  zao zimekuwa  zikiongezeka na  kupungua.

La kujiuliza ni mazingira yapi husababisha upinzani kupata kura za kupanda na kushuka hasa ngazi ya Urais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi? Mfano mwaka 1995  NCCR- Mageuzi ilipata  kura asilimia 27.77,  mwaka 2000 CUF asilimia 16.26,  mwaka 2005 CUF asilimia 11.17,  mwaka 2010 Chadema asilimia 27.05  na mwaka 2015 Chadema(Ukawa) asilimia 39.97

Rais wa zamani wa China, Mao  Dze Dong aliwahi kusema: ‘‘Bila utafiti huna haki ya kusema.’’ Hata hivyo zipo sababu  za  wazi zinazoweza kusababisha  kupanda na kushuka kwa upinzani mfano mgongano wa kimaslahi ambapo inasemekana kuna nguvu ya kugombania mnofu wa nyama  ndani ya vyama hivyo.

Ulafi wa madaraka ni sababu mojawapo inayosababisha  vyama vya upinzani kupanda na kushuka kwani ni  jambo la kawaida kusikia vyama hivi vikigombania nafasi za juu hasa za uenyekiti na hivyo kuhatarisha uhai wa vyama hivyo.

Vyama vya upinzani ni vyepesi kupigania demokrasia kutoka chama tawala huku vyenyewe vikishindwa kufanya hivyo. Si jambo geni kusikia kuwa viongozi wa ngazi za juu huendesha vyama hivyo kimabavu  huku waking’ang’ania madaraka na kushindwa kuyatoa kwa wengine hasa vijana.

Vyama vya upinzani hupenda kukosoa chama kilichoko madarakani wakati ndani ya vyama hivyo viongozi wakichukia kukosolewa. Ni katika mazingira ya namna hii mwanachama mwenye uwezo wa kukosoa anaweza kuitwa msaliti au kibaraka wa CCM na kuambulia kutimuliwa.

Ni kweli chama kilichoko madarakani kinaweza kuwa na mawakala (agents) wake ndani ya upinzani ili kuusambaratisha  lakini kuna haja ya kuchukua tahadhari maana kutimuana  kunaweza kuzaa balaa kwani  huwezi jua anayetimuliwa ana wafuasi wangapi.

Kama ilivyo kwa CCM kufanya uteuzi kiupendeleo kwenye nafasi zenye ulaji, ndivyo ilivyo kwa  baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa vikilaumiwa na wafuasi wao  kwamba wanaoteuliwa kushika nafasi za wabunge wa viti maalumu ni ndugu wa viongozi wa ngazi za juu.

Ukosefu wa umoja ni changamoto nyingine inayovikabili vyama hivi kushindwa kutimiza malengo japo katika uchaguzi wa mwaka jana vyama vinne vilijaribu kuunda Ukawa na kuleta mchakamchaka kwa CCM lakini kumbuka ACT-Wazalendo na vyama vingine vilikuwa pembeni.

Kama ilivyo kwa CCM  kutafunwa na  dhambi ya ufisadi  ndivyo inasemekana kwa baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo wakati mwingine hupata kigugumizi kuweka hadharani mapato na  matumizi  huku tukiambiwa baadhi ya viongozi ni matajiri waliojilimbikizia mali.

Ukosefu wa rasilimali fedha na watu pamoja na kushindwa kuweka mizizi vijijini ukilinganisha na CCM iliyokaa  madarakani muda mrefu ni kizunguzungu kwa vyama vya upinzani vinavyochipukia.

Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa mwanafalsafa  alituachia fumbo zito kulifumbua  kwani pamoja na kusema chama kikikaa madarakani  muda  mrefu  huwa fisadi ndiye  aliyesema kiongozi bora atapatikana CCM.

Hata   hivyo bila  upinzani Taifa litazama,  lakini kwa kasi ya Rais Magufuli akifanikiwa kuboresha maisha ya walalahoi  huku upinzani  ukikosa ubunifu na kubakia kulalamika eti anatumia ajenda zao, kuna uwezekano CCM ndani ya vimajipu vidogo vidogo visivyoonekana kwa darubini ikaendelea kutawala kwa muda mrefu hadi hapo kitakapopatikana kizazi kipya chenye fikra mbadala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles