23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mabomu, vilio vyarindima Kiwanda cha Urafiki

Askari wakiimarisha ulinzi katika geti la kuingilia katika Kiwanda cha nguo cha Urafiki, Ubungo jijini Dar es Salaam baada ya kutokea vurugu zilizosababishwa na wafanyakazi wanaodai malimbikizo ya mishahara yao.Picha na Jumanne Juma
Askari wakiimarisha ulinzi katika geti la kuingilia katika Kiwanda cha nguo cha Urafiki, Ubungo jijini Dar es Salaam baada ya kutokea vurugu zilizosababishwa na wafanyakazi wanaodai malimbikizo ya mishahara yao.Picha na Jumanne Juma

NA MARTIN MAZUGWA, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi     jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, Dar es Salaam, waliokuwa wameitisha mgomo wakitaka menejimenti ya kiwanda hicho iwalipe stahili zao.

Polisi   wa Kituo cha Urafiki walijaribu kuwatuliza wafanyakazi hao bila mafanikio ndipo walipolazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi hao waliokuwa wakiwashambulia polisi kwa mawe.

Habari zinasema vurugu hizo zilizuka baada ya pande mbili kushindwa kuafikiana kuhusu malipo ya malimbikizo na madeni ya wafanyakazi yanayofikia Sh bilioni 9.5 huku uongozi wa kiwanda ukidai hauna uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.

Katika vurugu hizo watu watatu walipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Palestina, Sinza  huku mtu mmoja akishikiliwa na polisi akidaiwa kumpiga na kumnyang’anya simu mwanamke katika vurugu hizo.

Mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Hassani Mwanji,aliliambia MTANZANIA kuwa madai yao yalitakiwa kuwa yametekelezwa Aprili 30 mwaka huu kama mahakama ilivyokuwa imeamua, lakini wanashangaa hadi sasa  hawajalipwa fedha zao kitu kinachosababisha washindwe kufanyakazi.

“Tunashindwa kuelewa uongozi wa Kiwanda cha Urafiki  kushindwa kutimiza maagizo ya mahakama   kutupatia haki yetu, tumechoshwa na ahadi zao , tunataka haki yetu,” alisema mfanyakazi huyo.

Naye Meneja Rasilimali watu wa kiwanda hicho, Dicksoni Machilila, alisema   kiwanda   hakina uwezo wa kulipa deni hilo kutokana na kushuka   uzalishaji.

Alisema kwa sababu hiyo hivi sasa kinafanya kazi  kwa zamu moja badala ya tatu zilizokuwapo awali.

“Kiwanda hakijakataa kulipa madeni yao kama Mahakama ilivyoagiza  kwamba tulitakiwa kulipa fedha hizo Aprili 30 lakini itakuwa haitawezekana kutokana na kushuka   uzalishaji wa kiwanda,” alisema.

Alisema Watanzania wana asilimia 49 katika kiwanda hicho, huku mwekezaji (Mchina) akimiliki asilimia 51 kwa sababu hiyo mamlaka ya uamuzi wowote yako mikononi mwa Wachina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles