30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jipu tena MSD

Untitled-2*Mwandishi wa Mtanzania abaini dawa zake zauzwa duka binafsi Mwananyamala

*Alipohoji mwenye duka akambambikia kesi ya ujambazi, Kamanda Fuime ang’aka

 

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

DAWA za kutibu binadamu zinazomilikiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), zimegundulika kuuzwa katika duka moja la mfanyabiashara binafsi lililoko eneo la Mwananyamala kinyume na agizo la Serikali.

Hayo yalibainika wiki iliyopita baada ya mwandishi wa habari na mhariri sanifu wa gazeti hili, Dennis Luambano, kwenda katika Duka la Damaco lililoko nje ya Hospitali ya Mwananyamala na kununua dawa zenye nembo ya MSD huku akinyimwa risiti za kodi zinazotambuliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) na kupatiwa iliyoandikwa kwa mkono.

Akizungumzia tukio hilo katika chumba cha habari cha gazeti la Mtanzania, Sinza Kijiweni, Luambano alisema dawa hizo zinauzwa kinyemela kwa wauzaji kutowapa risiti wanunuzi na kwamba mmiliki wa duka hilo anatumia nguvu ya fedha kuficha uovu anaoufanya.

Luambano alisema baada ya kununua dawa hizo na kuanza kuhoji dawa za Serikali kuuzwa katika duka binafsi, alikamatwa na polisi waliokuwa na mmiliki wa duka hilo aliyemtaja kwa jina la Herman Manyanga na kubambikiwa kesi ya ujambazi na utapeli.

“Asubuhi ya Aprili 18, mwaka huu mtoto wangu, Bahati alipata ajali ya gari akiwa na wenzake eneo la Bamaga karibu na Kituo cha Sayansi. Akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kupata matibabu.

“Pale Mwananyamala daktari alinielekeza kwenda kununua dawa duka la hospitali lakini baadhi ya dawa hizo hazikuwepo ikanilazimu kwenda kununua nje. Nilikwenda duka la Damaco lililoko nje ya hospitali na cheti cha daktari na kuuziwa ‘urine bag, catheter na dripu’ tatu zenye nembo ya MSD lakini muuzaji akaninyima risiti ya TRA, nilipong’ang’ania akinipa ya kuandika kwa mkono,” alisema Luambano.

Alisema wakati akirejea wodini aliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu, kuhusu dawa hizo ambaye alimtaka azipige picha pamoja na risiti kisha amtumie kupitia kwenye simu yake ya kiganjani kwa ajili ya ufuatiliaji jambo ambalo alilitekeleza kisha akarudi wodini.

Luambano alisema baadaye mwanaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi hivyo aliondoka na dawa zilizosalia alizonunua kwenye duka la Damaco na kuendelea na uchunguzi wa suala hilo ambalo Bwanakunu alieleza kuwa ametoa maagizo kwa watendaji wake kulifanyia uchunguzi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

“Katika kufuatilia habari hiyo nilimtafuta mmiliki wa duka la Damaco kupitia simu ya kiganjani ili nipate maelezo yake na yeye alisema limemshtusha hivyo hawezi kuliongelea kwenye simu, akanitaka niende dukani kwake jambo ambalo sikuliafiki bali nilimwalika yeye ofisini kwake lakini alisita na kuomba nichague sehemu nyingine aje azione hizo risiti kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua.

“Sikuona tatizo, nikamwelekeza eneo ninaloishi ni Mikocheni akasema atafika, alikuja kweli akaniita Baa na Restaurant ya MRC iliyo jirani tu na kwangu nikaenda kumuonyesha risiti na dawa hizo pamoja na kupata maelezo yake.

“Alipoziona dawa na risiti alitaharuki huku akisema hata mwandiko kwenye risiti ameshaujua hivyo akaaga kwenda dukani kwake kutafuta ukweli kabla ya kunipa maelezo yake,” alisema Luambano.

Akisimulia zaidi sakata hilo, alisema Manyanga alimpigia simu baadaye akimtaka wakutane saa 10 jioni siku hiyo hiyo katika Baa na Restaurant ya MRC kwa ajili ya kumpa maelezo yake lakini alipofika aliwekwa chini ya ulinzi wa askari polisi ambao walimfunga pingu huku wakimtuhumu kwa ujambazi.

“Nilikwenda na kumkuta yuko amekaa peke yake. Kabla sijakaa wakaja vijana wawili wakatoa pingu wakanifunga huku wakinieleza kuwa wameambiwa na Manyanga mimi ni jambazi hivyo wakanipeleka kituo cha polisi Oysterbay na kuniweka ndani,” alisema.

Alilaumu kuwa aliwekwa rumande bila kuchukuliwa maelezo hadi alipotolewa na mkuu wa kituo ambaye pia aliitisha jalada alilofunguliwa na baada ya kulipitia aliwaamuru askari wachukue maelezo yake kisha wampe dhamana.

“Kabla sijatoa maelezo niliuliza kosa langu nikaambiwa ni jambazi. Jalada langu lilipewa namba OB/RB/7795/2016,” alisema.

 

RPC Fuime ashangaa

Luambano alieleza zaidi kuwa alifika tena kituo cha polisi Oysterbay siku iliyofuata akiwa ameandamana na wahariri wawili wa Gazeti la Mtanzania aliowataja kuwa ni Ratifa Baranyikwa na Charles Mullinda ambao baada ya kushindwa kuonana na mpelelezi ya kesi hiyo walikutana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (RPC), Christopher Fuime ambaye baada ya kusikiliza sakata hilo alishtuka na kuagiza polisi kufanya uchunguzi kuhusu dawa za Serikali kuuzwa mitaani.

“Hivi MSD wanashindwaje kumkamata mtu anayeuza dawa za Serikali wakati risiti na kidhibiti cha dawa kipo? Wanataka nini tena wakati jambo hili liko wazi? Na mnaona jinsi wananchi wanavyolichezea Jeshi la Polisi, huyu bwana amegundua kuwa amefanya kosa atalipuliwa amekimbilia polisi kuja kubambikia kesi mwandishi, sasa uongo wa aina hii ndio polisi wakichukua hatua wanalaumiwa.

“Nimewaagiza vijana wangu kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu jambo hili kwa sababu jalada lipo hapa kwetu na sisi bwana ni kazi tu, tutachukua hatua haraka na wananchi watajua,” alisema Kamanda Fuime.

Wakati Kamanda Fuime akitangaza kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hilo, Mkurugenzi Bwabakunu alisema bado uchunguzi wao unaendelea.

Alipoulizwa Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, iwapo taasisi hiyo inalifanyia kazi suala hilo alisema limekwishafikishwa mezani kwake na linafanyiwa kazi kwa kushirikiana na MSD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles