27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai ampa kibarua katibu wa Bunge

 jobNa Elizabeth Hombo, Dodoma

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameagiza Ofisi ya Katibu wa Bunge kuratibu uchaguzi wa Kamati Sita za Kudumu za Bunge.

Kwa mujibu wa Waraka  Na 04/2016 wa Mabadiliko ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge uliotolewa jana, Spika pia amefanya mabadiliko ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.

Kuhusu uchaguzi, Spika ameagiza ofisi ya Katibu wa Bunge kuratibu uchaguzi wa Kamati ya Nishati na Madini kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa nafasi za mwenyekiti na makamu mwenyekiti.

Kamati nyingine ni Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)  nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) nafasi ya mwenyekiti, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) nafasi ya mwenyekiti na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, nafasi ya makamu mwenyekiti.

Ndugai alisema  Ibara ya 96 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imelipa uhalali Bunge kuunda Kamati za Bunge za namna mbalimbali kadri itakavyoona inafaa kwa ajili ya utekelezaji bora wa madaraka yake.

Alisema pia kwa mamlaka aliyopewa chini ya Kanuni ya 116 (3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Aprili 2016, amelazimika kufanya mabadiliko ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge.

Spika alisema sababu kubwa iliyomfanya kufanya mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa kila Mbunge ikiwa ni pamoja na wabunge wengine wanne wapya walioapishwa Aprili 19,  anakuwa mjumbe kwenye kamati mojawapo ya Bunge.

Alisema  mabadiliko hayo ni kwa ajili ya kuhakikisha  kuwa kwa kadri inavyowezekana, muundo wa Kamati za Kuduma za Bunge unazingatia aina za wabunge (jinsia, pande za Muungano na vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni), ujuzi maalum, idadi ya wajumbe kwa kila kamati na matakwa ya wabunge wenyewe.

Aliwataja wabunge walioapishwa kuwa ni Shamsi Vuai Nahodha na Wabunge wa Viti Maalum, Ritha Kabati (CCM), Oliver Semuguruka (CCM) na Lucy Owenya ( Chadema).

Wabunge waliobadilishwa ni Neema Mgaya kutoka Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwenda Huduma na Maendeleo ya Jamii, Bernadeta Mushashu kutoka Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwenda Kamati ya Huduma na Maendeleo ya jamii na Kunti Majala kutoka Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwenda Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Wengine ni Ussi Salum Pondeza kutoka Kamati ya Nishati na Madini kwenda Kamati ya Katiba na Sheria, Richard Ndassa kutoka Kamati ya Katiba na Sheria kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Sebastian Kapufi kutoka Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mabadiliko hayo pia yanawahusu Atupele Mwakibete kutoka Kamati ya Sheria Ndogo kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Omar Kigoda kutoka Kamati ya Miundombinu kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Dk Godwin Mollel kutoka Kamati ya Katiba na Sheria kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Pia wamo Dk Raphael Chegeni kutoka Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwenda Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Ibrahim Hassanali Raza kutoka Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Abdulaziz Abood kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwenda Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Wengine ni Emanuel John kutoka Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Jacqueline Msongozi kutoka Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenda Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Josephine Genzabuke aliyetoka Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenda Hesabu za Serikali na Suleiman Sadick kutoka Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii kwenda Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles