30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kambi ya Wazee yenye watoto wasiokuwa na ‘baba’

pNa Asifiwe George, Aliyekuwa Mwanza

YAPO baadhi ya makundi mbalimbali katika jamii ambayo yamesahaulika katika huduma za afya hususani wazee, walemavu na wagonjwa wa akili.

Pamoja na kwamba kuna vituo maalumu ambavyo vimetengwa kwa ajili yao lakini hawana wasimamizi na wahudumu wa kuwapa mahitaji yao ipasavyo.

Wazee wanaoishi katika Kituo cha Ustawi wa Jamii cha Bukumbi, Kijiji cha Kigongo, Kata ya Idetemya wilayani Misungwi mkoani Mwanza, wanaiomba Serikali kuwapatia huduma za afya katika zahanati ya kituo chao.

Wazee hao wanaeleza changamoto ya huduma za afya na uzazi wa mpango katika ziara ya waandishi wa habari iliyoratibiwa na taasisi inayojishuhulisha na ongezeko la idadi ya watu na uzazi wa mpango (TCDAA).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazee hao wanasema kwamba, katika zahanati hiyo hakuna dawa na wanapoumwa wanalazimika kununua.

Mwenyekiti wa Kambi hiyo, Helena Emmanuel, anasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za huduma za afya, huduma za uzazi wa mpango pamoja na baadhi ya wazee na walemavu wasiojiweza kufukuzwa kambini.

“Tunapofika katika zahanati yetu daktari anatupima vizuri lakini hakuna dawa, hivyo anatuandikia na kutuambia tukanunue kwenye maduka ya dawa.

“Kwakweli hii ni changamoto kubwa kwetu kwa sababu wakati mwingine tunapoandikiwa dawa fedha za kununulia tunakosa hali inayosababisha tuendelee kuumia na hatuna sehemu ya kujipatia kipato,” anasema Helena.

Anasema changamoto nyingine ni ongezeko la watoto wanaozaliwa katika kambi hiyo ambao baba zao hawajulikani.

Anasema huduma ya uzazi wa mpango inahitajika kituoni hapo kwa sababu kuna wasichana wanaoishi katika kambi hiyo wanabeba mimba za mara kwa mara ambazo baba zao hawafahamiki.

“Katika kambi hii tunaishi wazee, walemavu na wagonjwa wa akili na idadi kubwa ya watu wanaopata ujauzito ni wagonjwa wa akili na wale wanaoanguka kifafa.

“Kwa sasa hapa kambini tupo watu 78 lakini wapo walemavu saba ambao wamefukuzwa wameambiwa waende vijijini wakati hawana uwezo wa kujitafutia, mimi sina uwezo wa kuwasaidia kwa sababu ni mlemavu,” anasema.

Ofisa Mfawidhi wa Makao hayo, Michael Bundala, anasema kuna watoto 17 ambao wamezaliwa ndani ya kambi hiyo na mama zao wanaishi humo lakini baba zao hawajulikani.

“Watoto walikuwa wengi mno lakini hivi karibuni tuliwapunguza wale waliotimiza miaka 18 na kuwapeleka katika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili yao, tusingefanya hivyo wangekuwa watoto zaidi ya 800.

“Idadi hiyo inaongezeka kwa sababu baadhi yao wanapeana ujauzito wenyewe kwa wenyewe na wasichana wengine wanapata kutoka kwa vijana wanaoishi nje ya kambi ,” anasema Bundala.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Kata ya Idetemya, Sebastian Kisumu, anasema ipo changamoto ya vijana wa nje kuwapa mimba wasichana wanaoishi katika kambi hiyo na kusababisha ongezeko la wategemezi.

Anasema wapo wataalamu mbalimbali ambao wanafika katika kambi hiyo kutoa elimu ya uzazi wa mpango lakini wengi wao hawaipokei hali inayosababisha kuwa na idadi kubwa ya watoto ambao hawana baba.

“Sasa umefika muda wa kuchukua hatua na kuwasimamia vijana wetu kwa kuhakikisha wanatumia huduma za uzazi wa mpango kwa lengo la kupunguza watoto wanaozaliwa mara kwa mara ambao wanakuwa tegemezi kwa Serikali,”anasema Kisumu.

Consolata Edward mwenye watoto sita anasema mara nyingi hupata ujauzito wakati anapoanguka kifafa hivyo hushindwa kuelewa amepewa na nani.

“Mimi nililetwa na Serikali katika kituo hiki kutokana na ugonjwa wa kifafa, huwa nashangaa nina ujauzito lakini sijui nani aliyenipa. Kuna wataalamu wa uzazi wa mpango kutoka Maria stopes walikuja na kunishauri nifunge kizazi.

“Lakini kabla hawajanifunga waliponipima walikuta nina ujauzito wa mizezi saba, nilishangaa sana kwa sababu mtoto mdogo ana mwaka mmoja.

“Nina watoto sita na kila mtoto simjui baba yake, hawa wakubwa hawataki kukaa na mimi kwa sababu wananiogopa mmoja nilimpiga nikamkaba shingo hata nikimwambia aje hataki,” anasema Consolata.

Anasema kwa sasa watoto hao wameanza kusoma na jina la baba waliloandikishwa shuleni ni Bundala ambaye ni Ofisa Mfawidhi wa Makao hayo ya Wazee Wasiojiweza.

Consolata anakabiliwa na changamoto ya sare za shule hivyo anaiomba Serikali imsaidie ili watoto wake waweze kuendelea na masomo.

Mtaalamu wa Uzazi wa Mpango, Shida Masumbi, anasema njia za uzazi wa mpango hutumika na wanaume na wanawake kwa madhumuni ya kupanga uzazi ili kuwa na familia bora.

Anasema ni vigumu kusema kuna njia iliyo bora zaidi ya uzazi wa mpango kwa kuwa kila njia ina faida na hasara zake hyivyo mwanamke na mwanamume wana maamuzi juu ya mipangilio wa kupata watoto.

Masumbi anasema kufanya uchaguzi utumie njia ipi kupanga uzazi si kitu rahisi kwa kuwa kuna mambo mengi ya kuzingatia kabla ya kufanya maamuzi yoyote.

“Inabidi ujifunze njia mbalimbali ili kuweza kubaini ni njia ipi itakayokufaa pamoja na mwenzi wako kupanga uzazi.

“Mnaweza pia kuwasiliana na muuguzi au daktari anayehusika na masuala ya uzazi wa mpango kwa ushauri ili muweze kuchagua njia sahihi itakayowafaa,” anasema Masumbi.

Anasema huduma za uzazi wa mpango ni nzuri kwa sababu zinamwezesha mwanamke kupumnzika kwa muda mrefu na kuweza kujishughulisha na shughuli zake za kiuchumi.

Mtaalamu huyo anasema kuna njia tatu za uzazi wa mpango ambazo ni njia ya muda mfupi, muda mrefu na ya kudumu.

Kulingana na mtaalamu huyo, njia za muda mrefu ni kitanzi, kipandikizi na njiti wakati za muda mfupi ni sindano, vidonge na kondomu na za kudumu ni mume au mke kufunga kizazi.

“Baadhi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango husababisha maudhi madogo madogo ambayo ni kukosa hedhi, kuongezeka siku za hedhi, kutokwa na damu kwa muda mrefu na kuona matone madogo madogo ya damu,” anasema Masumbi.

Anasema  pamoja na maudhi hayo lakini kuna faida kama vile kuzuia vifo kwa mama na mtoto, mama kupumnzika kwa muda mrefu na kujishughulisha na kazi nyingine za kimaendeleo.

Anasema mwitikio wa matumizi ya uzazi wa mpango ni makubwa kwa sababu wanaume 300 walijitokeza kufunga kizazi kwa mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles