27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti ya CAG yamtia hasira JPM

CAG*Avunja Bodi ya TCRA, amtumbua mkurugezi kwa ufisadi wa trilioni moja

Na Bakari Kimwanga, Dodoma

NI wazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imempa hasira Rais Dk. John Magufuli, baada ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Ally Simba.

Rais amemsimamisha kazi Dk. Simba kutokana na kile alichodai kushindwa kusimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), kitendo kilichosababisha nchi kukosa mapato ya Sh bilioni 400 kwa mwaka – zaidi ya Sh trilioni 1 kwa kipindi cha miaka mitatu tangu walipoingia mkataba na Kampuni ya SGS Machi 22, 2013.

Uamuzi wa Rais Magufuli umekuja siku moja baada ya CAG, Profesa Mussa Assad kuwasilisha taarifa ya ukaguzi kwa mwaka 2014/15 kwa wabunge mjini Dodoma juzi.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ikulu, Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kufanya kikao kazi, kati yake na viongozi, wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Machi 22, 2013, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliingia mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano.

“Lakini mpaka sasa, Kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na udhibiti wa mapato ya simu ya ndani (offnet), hali ambayo imesababisha Serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa Sh bilioni 400 kwa mwaka,” ilisema taarifa hiyo.

Pamoja na hatua hiyo, Rais Magufuli ametangaza kuvunja Bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja.

Pia amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo mara moja.

Licha ya kutoa agizo hilo, Rais Magufuli  amewataka Waziri Mbarawa, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Faustine Kamuzora na naibu wake, Mary Sassabo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji mapato ya simu za ndani uanze kufanya kazi na nchi ipate mapato yanayostahili.

“Waziri nakuagiza chukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya Serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayekwamisha jambo hili,” alisema Rais Magufuli katika taarifa hiyo.

 

MIEZI 9

Dk. Simba amedumu katika wadhifa huo kwa miezi tisa tangu alipoteuliwa Julai 6, mwaka jana na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kwa mamlaka aliyopewa chini ya sheria Na. 12 ya mwaka 2003 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania Kifungu cha 13 (1).

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Simba alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

 

TAARIFA YA CAG

Juzi akiwasilisha taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali bungeni, CAG Profesa Assad, alisema TCRA inaendesha mfumo wa udhibiti wa mawasiliano ya simu (TTMS) ambao unafuatilia mwenendo wa mawasiliano ya simu kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano waliopewa leseni, bila njia sahihi.

Alisema mfumo wa mawasiliano kwa sasa unaweza kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya kimataifa, lakini haujaweza kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya ndani.

“Kukosekana kwa mawasiliano ya kutosha kati ya taasisi muhimu zinazoweza kunufaika na mtambo huu, kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kumesababisha Serikali kuendelea kupoteza mapato yatokanayo na mawasiliano ya simu za ndani,” alisema Profesa Assad.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles