27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema, Polisi kupimana nguvu leo

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewahamasisha wanachama wake walio jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani kufurika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam wakati mwenyekiti wao Freeman Mbowe atakapohojiwa, huku jeshi hilo likionya raia yeyote kutosogelea eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa aliwataka vijana kuhakikisha wanaandaa mazingira ya kuhakikisha mwenyekiti wao anaenda polisi salama na kwa amani.

Dk. Slaa alisema: “Kesho tunakwenda saa tano, tumeandaa mawakili wetu wote waliopo ndani ya chama, tunataka polisi wajiandae kwa hoja, vijana andaeni mazingira kuhakikisha kiongozi wenu anaenda kwa amani na katika hali hii ningependa twende hata mahakamani.”

Baada ya kauli hiyo, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika alisisitiza kwa kuwataka wanachama wa chama hicho waliopo Dar es Salaam na mikoa ya jirani kufika kwa wingi kwenye ofisi za Makao Makuu ya Polisi.

“Nitoe wito kwa wanachama wa Chadema walioko Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam, waje kesho saa tano Makao Makuu ya Polisi, wafike kwa wingi kwa sababu kauli aliyoitoa mwenyekiti ni ya kutetea masilahi ya wananchi na tumekubaliana katika Mkutano Mkuu,” alisema Mnyika

MAWAKILI WATANO

Akizungumzia wito wa polisi, Dk. Slaa alisema Mbowe ataongozwa na wanasheria watano wa chama hicho kwenda kusikiliza alichoitiwa na polisi.

Msafara huo utaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu pamoja na mwanasheria wa chama hicho kutoka Makao Makuu, Peter Kibatala na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando na Halima Mdee.

POLISI YACHARUKA

Mara baada ya mkutano wa Chadema na waandishi wa habari kumalizika, Jeshi la Polisi nalo liliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa onyo kwa wananchi watakaojaribu kufuata wito wa chama hicho.

Katika mkutano huo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema yeyote atakayejihusisha na maandamano hayo atachukuliwa hatua za kisheria kwani ni batili na Jeshi la Polisi haliyatambui.

“Maandamano hayo ni batili kwa sababu kuu mbili, kwanza Bunge la Katiba lipo kwa mujibu wa sheria na hakuna sheria yoyote iliyokiukwa, kwahiyo kitendo cha kufanya maandamano kushinikiza kuvunjwa kwa Bunge hilo ni kinyume na sheria na jeshi letu haliwezi kuruhusu.

“Pili, hivi sasa kesi ya kuhoji uhalali wa kuendelea kwa Bunge bado ipo mahakamani na haijafikia mwisho, kwahiyo hata uamuzi haujatolewa. Maandamano yaliyopangwa na Chadema yanaingilia uhuru wa mahakama, jambo ambalo siyo sahihi,” alisema Chagonja.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Yeyote atakayekiuka katazo hili, Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria,” alisema.

MAANDAMANO PALE PALE

Dk. Slaa alisema pamoja na wito huo, wanaamini polisi, azimio la Kamati Kuu ya chama hicho la kufanya maandamano nchi nzima, lipo palepale.

“Polisi wanalipwa pesa kwa kodi za Watanzania walalahoi kwa kazi yao na jukumu lao ni kutoa ulinzi na usalama, sio kutunishiana misuli na vyama vya siasa au wananchi.

Azimio la Kamati Kuu, halivunjwi na Mungulu (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai – DCI, Isaya Mngulu) wala Chagonja  (Kamishina wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja),   maandamano yapo palepale na safari hii wakikataa kutoa kibali tutaandamana hivyo hivyo  watupige mabomu ili dunia nzima wajue kama hii sio nchi ya demokrasia,” alisema Dk. Slaa.

Alisema wakianza maandamano ya kupinga Katiba nchi nzima, nguvu ya polisi haiwezi kushinda ya wananchi kwakuwa polisi ni wachache na wanaohitaji Katiba yenye maoni ya Watanzania ni wengi.

MIKAKATI YA UKAWA

Akitaja maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema, Dk. Slaa alisema wamejadili namna ya kuunganisha nguvu na vyama vinavyounda Ukawa ili kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Desemba 14.

Alisema chama hicho kimeunda kamati itakayoratibu suala hilo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Safari, Naibu Katibu Mkuu Bara, Mnyika, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Lissu na Benson Kigaila.

“Kamati itaanza kazi baada ya mkutano huu kwa kukutana na viongozi wa vyama vingine vinavyounda Ukawa, na hii ni mikakati ya kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015,” alisema Dk. Slaa

Akizungumzia suala la Katiba, alisema  Rais Jakaya Kikwete alipokutana nao alikiri mchakato huo kutokamilika, lakini akashindwa kusitisha Bunge kwa kuogopa lawama kutoka kwa wajumbe wabunge hilo.

“Kikwete hana dhamira ya dhati, hawezi kufanya maamuzi magumu, anashindwa kuueleza umma kwa kuogopa kujiua kisiasa,” alisema Dk. Slaa.

Alisema pia kuwa viongozi waliomo bungeni wa vyama vya siasa wanapotosha wananchi kwa madai kuwa Katiba itapatikana na kwamba upotoshaji huo unaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro.

Habari hii imeandaliwa na Aziza Masoud, Veronica Romwald, Oliver Oswald, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. katika majadiliano ya sura za katiba itakayopendekezwa kuna mambo mengi ambayo bado yanaelea hewani, kwa maana kwamba hawakufikia muafaka. sasa hawa waandishi wa hiyo katiba inayotokana na hayo majadiliano wanaandika nini hasa???haya ni maajabu makubwa….

  2. Naona Tanzania kumekucha, utawala wa sheria lazima utambue haki za wananchi na mojawapo ni kuandamana kwa amani. Hii ni sheria ya umoja wa mataifa mbona CCM na polisi wake hawaelewi? Waende wakajifunze kenya na sehemu nyingine, mwaka huu Polisi kenya waliaka kumzuia Raila asiandamane na wafuasi wake toka Uwanja wa ndege wakati akitoka Marekani, lakini wapinzani walisema maandamano yako, polisi karibuni mtuue, nadhani hasira za wakenya zilikuwa kubwa sana na baadaye Rais aliona ataleta maafa akaamuru polisi maandamo yawepeo, hapakuwa na mauaji, wala vurugu. Polisi wa Tz wanatafuta sababu za kujeruhi watu na kutisha watanzania ili wasidai haki zao baada ya kuona bosi wao CCM amelikoroga katiba mpya ambayo haitapatikana kamwe kwa mchakachuo huo. Katiba mpya italetwa na Rais ajaye tena kwa kufuta yote yalioyoongelea katika bunge hili, na kuanza upya. Polisi acheni demokrasia ichukue mkondo wake, mtaweza kuendelea kuibeba wala kuilinda CCM. Wananchi ni wengi kuliko idadi ya polisi, kaazi kwenu.

  3. Polisi mtaua watu lakini damu zao zitawafuata hadi kaburini na kizazi chenu chote. Jifunzeni yaliyotokea Misri, Libya na sehemu nyingine, ni kujidanganya kwamba hayawezi kutokea nchini Tanzania, hatuyatafuti wala kuyafurhia lakini ukweli lazima usemwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles