30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe awekewa pingamizi Chadema

Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu kwa madai ya kukiuka katiba ya chama hicho na maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Pingamizi hilo limewekwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo.

Barua ya Mbarouk yenye kumbukumbu namba  Mbarouk/UCH/14 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema na Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyoandikwa Septemba tano, inasema kufikia Septemba 14 siku ya uchaguzi mkuu wa chama hicho, Mbowe atakuwa ametumikia vipindi viwili katika nafasi ya mwenyekiti wa taifa.

Barua ya Mbarouk inasema kwa  mujibu wa katiba ya Chadema, kama ilivyothibitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, hakuna mwanachama anayeruhusiwa kuchaguliwa kuongoza kwa zaidi ya vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja.

“Msajili wa Vyama alikuwa ametoa maelekezo kwamba chama kiitishe Baraza Kuu na Mkutano Mkuu Maalumu kwa lengo la kubadilisha kipengele kinachoweka ukomo wa uongozi kama litaona kuna haja hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu. Hata hivyo hadi naandika barua hii hakuna dalili zozote kwamba mkutano mkuu maalumu utaitishwa na maandalizi ya uchaguzi yanaendelea bila kujali agizo la msajili wa vyama,”alisema Mbarouk katika barua hiyo.

Alisema katika kipindi chake cha uongozi Mbowe alisimamia  vikao vya chama  vilivyofanya maamuzi ya kuvunja katiba waziwazi.

“Mfano Novemba 2013, Mbowe alisimamia kikao cha kamati kuu kilichomvua nafasi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama, Zitto Kabwe na wenzake bila kuzingatia mamlaka ya kikao hicho. Kwa mujibu wa Sura ya Sita ibara ya 6.3.6(b) ya katiba ya Chadema toleo la mwaka 2006 ‘kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua’,”alisema.

Alisema baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 chama kilipata nafasi tano za kuteua nafasi wabunge wa viti maalumu kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambapo Kamati Kuu kilipitisha majina ya Suzan Kiwanga, Chiku Abwao, Halima Mdee, Mhonga Ruhanywa na Grace Kiwelu lakini Mbowe alibadilisha majina hayo.

“Mbowe alibadilisha majina ya Chiku Abwao na Susan Kiwanga  huku akiwapachika Susan Lyimo na Lucy Uwenya. Baadaye Mbowe alikiri kosa na kuomba msamaha katika kikao cha Kamati Kuu,”alisema.

Alisema hayo yote yanadhihirisha pasipo shaka kwamba mwenyekiti huyo amekosa uaminifu hivyo anapaswa kunyang’anywa nafasi hiyo ya uenyekiti.

“Ninatambua kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama Sura ya Saba ibara ya 7.3.1, uchaguzi ngazi ya taifa unapaswa kusimamiwa na wazee wastaafu wa chama hata hivyo hadi naandika barua hii sina taarifa kuhusu kuteuliwa kwa kamati hii. Hivyo basi nimelazimika kuandika barua yangu ya pingamizi kwako nikiamini kwamba utaifikisha katika chombo husika kinachoshughulikia uchaguzi,”alisema Mbarouka.

Alipotafutwa na gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani kuzungumzia barua hiyo, Mbarouk alisema ni kweli ameandika barua hiyo na kwamba aliikabidhi juzi Septemba 6 katika ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama.

“Ni kweli nimeiandika mimi na nilikabidhi jana (juzi) katika ofisi ya katibu mkuu wa chama,”alisema Mbarouk.

Kwa upande wake Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alipoulizwa na gazeti hili endapo ni kweli barua hiyo imewafikia, alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa atampigia baadaye.

Hata hivyo baada ya Makene kumpigia simu mwandishi alimtaka amtajie lengo la Mbarouk kumpinga Mbowe, baada ya mwandishi kufanya hivyo aliahidi angepiga tena simu, lakini hadi gazeti linakwenda mtamboni hakupiga simu.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. Huyu bwana keshashindwa mapema kama kweli anagombea nafasi hii. Anataka kupata uongozi wa Chadema ngazi ya kitaifa kwa kutumia kanuni muflisi ambazo kwa hakika hawezi kufanikiwa. Kama ni mwanasiasa makini anayejiamini ajieleze vizuri kwa hoja madhubuti ili wanachama wamchague lakini kama anafikiri kuwa hayo malalamiko ndiyo yanayoweza kumpa nafasi ya uenyekiti Chadema taifa namshauri aende Mkuranga kulima matikiti maji.

  2. Kama kweli Mbowe hafai kuwa mwenyekiti wa CHADEMA tutajua siku ya uchaguz, kama ni suala la mkutano mkuu mimi sio msemaji wa chama ila hata nikiitwa kiherehere wa chama sawa tu, ila ukweli ni kwamba kesho mkutano mkuu utafanyika na ulishaitishwa siku nyingi hivyo mbaruku anadanganya kusema hajui kama mkutano mkuu umeitishwa.

  3. Mbaruku acha kutapa tapa mambo ya kina mdee mara zitto yanatoka wapi? Sisi tuambie wewe pale tabora na nje ya tabora umefanya nini kwaajili ya CHADEMA na utafanya nini kama ukiwa mwenyekiti hiyo ndio siasa. lakini kaka unaanza kulialia tu sasa hatujui hata umefanya nini na utafanya nini ambacho Mbowe alishindwa kutekeleza. labda niseme MBOWE hadi sasa hapaswi kubezwa na usitegemee KINANA ama NAPE NAUYE atakushauri kuwa Mbowe anafaa kuwa mwenyekiti kwasababu hawataki CHADEMA iwe na viongozi imara kama akina Mbowe, Mwakibinga, DR. Slaa ama Jesca Kishoa. Nashauri umwage sera zako chapa ilale. mkutano mkuu ni kesho nakukaribisha kamanda wangu mbaruku, pia nakushauri hata ikitokea umeshindwa uchaguzi suluhisho si kuhama chama cha msingi ni kuendeleza mapambano tu.

  4. Mh.mbaruku nakupongeza sana kwa mawazo finyu unayopewa na washauri wako chadema imetoka mbali inataka kwenda mbali hivyo mbowe ndo chaguo letu wengi tunaopenda maendeleo ya chama na tunao taka mabadiliko ya kweli. KATIBU MWENEZI JIMBO LA SIHA KAMANDA DANIEL NKINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles