29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ya Maalim Seif kuishi hotelini Dar

0D6A8296Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SIRI imefichuka kuhusu hatua ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, kuishi hotelini jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amekuwa akiishi katika Hoteli ya Serena jijini hapa tangu aliporuhusiwa kutoka Hospitali ya Hindu Mandal Machi 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa ofisa wa ngazi za juu wa CUF, alishangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuhoji kiongozi huyo kuendelea kuishi hotelini hapo.

Alisema hatua ya kiongozi huyo kuishi hotelini ni matokeo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kushindwa kutekeleza ahadi ya kumpa nyumba pindi anapokuwa Dar es Salaam katika shughuli zake.

Alisema kutokana na hali hiyo imekuwa ni utaratibu kwa kiongozi huyo kufikia katika hoteli hiyo na gharama za kuishi hotelini hapo hulipwa na SMZ kwa mujibu wa sheria.

“Tangu mwaka 2010 Maalim aliahidiwa atapewa nyumba na Serikali ya SMZ lakini hilo halijafanyika, hiyo nyumba hajapewa hadi leo ndiyo maana mara zote akija Dar hufikia hotelini.

“SMZ ndiyo wenye jukumu la kulipa na si vinginevyo, kwani hata kama kama kuna viongozi wa SMZ wamepewa nyumba kwa muda wote, lakini Maalim Seif hajapewa, sasa kama unataka kujua kwa undani unaweza kuwauliza viongozi wa Serikali wao ndiyo wenye majibu zaidi,” alisema ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Gharama zilizotumika kwa siku 7

Kwa mujibu wa chumba anachoishi kiongozi huyo chenye hadhi ya rais ambacho hutozwa kwa Dola za Marekani 2,801.50, ambapo dola moja ni sawa na Sh 2,180. Hivyo kwa siku saba hadi kufikia leo Serikali imemlipia Maalim Seif,  Sh milioni 42.946.

Kauli ya CUF

MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamad Masoud Hamad, alisema hatua ya Maalim Seif kuishi hotelini inatokana na maagizo ya daktari wake ambaye amemtaka apumzike kwa sasa.

Alisema kutokana na hali hiyo baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali alipokuwa akipatiwa matibabu alikwenda katika Hoteli ya Serena anapofikia kila mara anapokuwa jijini Dar es Salaam.

Alipoulizwa ni nani anayelipa gharama za kuishi hotelini hapo, Hamad alisema wanaoweza kuzungumzia suala hilo ni viongozi wa SMZ.

“Magufuli (Rais), alipokwenda kumwona alimuuliza ni nani anayemlipia gharama za hoteli na Maalim alisema wazi ni SMZ, lakini ninachotaka kuwaambia Maalim Seif hana nyumba Dar es Salaam.

“… kama wapo viongozi waliopewa nyumba wa SMZ ni hao lakini si Maalim Seif, tangu mwaka 2010 hana nyumba na hufikia hotelini, hana nyumba ya Serikali wala yake binafsi,” alisema Hamad.

SMZ wazungumza

Alipotafutwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema Maalim Seif anastahiki zake kama kiongozi wa SMZ ikiwemo kupatiwa haki ya matibabu pamoja na mahala pa kuishi.

“SMZ ni wajibu wake kuwahudumia viongozi na wananchi wake kwa ujumla, Maalim Seif bado ni Makamu wa Kwanza wa Rais hivyo ana wajibu wa kuhudumiwa.

“Na katika hili anahudumiwa na SMZ ikiwemo kulipiwa hoteli pindi awapo nje ya Zanzibar na si hilo tu pia tunahusika kumpa stahiki zake zote ikiwemo matibabu.

“Kwa kawaida pindi kiongozi yoyote wa kitaifa anapokuwa Dar es Salaam na kama hana nyumba SMZ hulipa malazi ya kiongozi wake na Maalim bado ni kiongozi na hata kama akiondoka kwenye uongozi bado anazo stahiki zake ikiwemo kuhudumiwa kama kiongozi mstaafu,” alisema Waziri Aboud.

Alisema pamoja na hali hiyo kwa sasa Serikali ya Muungano ndiyo inayolipa gharama za Maalim Seif kuishi hotelini kwa agizo la Rais Dk. John Magufuli.

Alisema ahadi ya Rais Magufuli ya kusaidia kulipia hoteli anayoishi Maalim Seif inaonesha ni namna gani Serikali zote mbili ya Muungano na ile ya Zanzibar zinavyoshirikiana kwa dhati.

“Kwa ubinadamu wake Rais Magufuli tunamshukuru sana kwani inaonesha namna gani kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano alivyo na mapenzi mema  na Zanzibar pamoja na viongozi wake.

“… ila pamoja na yote SMZ bado ina wajibu wa kutekeleza wajibu wake wa kuwatunza viongozi wake wote wakiwemo waliokuwa ndani ya Serikali pamoja na wale waliostaafu,” alisema Aboud.

Viongozi wamimika kumjulia hali

Tangu aliporuhusiwa kutoka hospitali kwa kiongozi huyo alikokuwa amelazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, viongozi mbalimbali wamekuwa wakimiminika kumjulia hali.

Machi 9, mwaka huu Rais Dk.  John Magufuli, alikwenda  katika Hoteli ya Serena kumjulia hali kiongozi huyo.

Maalim Seif yupo hotelini hapo kwa mapumziko baada ya kutolewa hospitalini hapo Machi 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa.

Katika mazungumzo yake na Rais Magufuli, Maalim Seif aliwawahakikishia Watanzania kuwa afya yake inaendelea vizuri na kwamba anaendelea na shughuli zake na siku chache zijazo ana matumaini ya kurejea katika hali yake ya kawaida.

Mbali ya kukutana na kiongozi huyo wa nchi, siku iliyofuata hasimu wake wa kisiasa ambaye ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein naye alikwenda kumwona pamoja na wanasiasa mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Msimamo wa Maalim

Maalim Seif, amesema mikutano yake ya hivi karibuni na Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein haikuwa na agenda yoyote ya kujadili hali ya kisiasa inayoendelea visiwani Zanzibar.

Kauli hiyo ya Maalim Seif aliitoa baada ya kuibuka minong’ono baada ya kutembelewa  na viongozi hao wa juu wa Serikali.

Hatua hiyo ya kukutana na viongozi hao ilizusha hisia kuwa huenda kulikuwa na jambo zito la kisiasa hasa ikizingatiwa kwamba zilikuwa zimebaki siku takriban 10 kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani humo ambao kiongozi huyo wa upinzani ametangaza kuwa chama chake hakitashiriki.

Maalim Seif alisema Dk. Shein alikwenda kumjulia hali kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Rais Magufuli na watu wengine wenye mapenzi mema, hivyo hakuna haja kwa Wazanzibari kuwa na hofu yoyote.

“Tusingeweza kuzungumza lolote wakati afya yangu siyo nzuri sana. Unapozungumza mambo mazito kama hayo ya uchaguzi lazima uwe mzima kimwili na kiakili,” alisema Maalim Seif baada ya kujuliwa hali na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Maalim ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana alisusia uchaguzi huo wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.

Marudio hayo ni kutokana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya awali kutokana na kile kilichodaiwa kukiukwa kwa taratibu.

Jecha na karatasi za kura

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, amesema ZEC imefanya marekebisho ya katarasi za kura na zinatarajiwa kufika visiwani humo Machi 17, mwaka huu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyotolewa jana Jecha alisema baada ya kubainika kasoro katika jina la mgombea wa Chama cha ADA-TADEA, ZEC imefanya marekebisho.

“Tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mashirikiano iliyoyaonesha katika kusahihisha kasoro zilizojitokeza na tunapenda kuwahakikishia wananchi na jumuiya za kimataifa kuwa uchaguzi utakuwa wa haki, huru na uwazi,” alisema Jecha katika taarifa yake.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles