27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mgomo wa wafanyabiashara watikisa Kariakoo

Baadhi ya maduka Kariakoo yakiwa yamefungwa baada ya maofisa wa TRA kuanza uhakiki wa watumiaji  wa mashine za risiti za kielektroniki (EFD) jijini Dar es Salaam. Picha na John Dande
Baadhi ya maduka Kariakoo yakiwa yamefungwa baada ya maofisa wa TRA kuanza uhakiki wa watumiaji wa mashine za risiti za kielektroniki (EFD) jijini Dar es Salaam. Picha na John Dande

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wa maduka ya soko la Kariakoo wameanza mgomo kwa muda usiojulikana kuanzia jana, sambamba na kuishinikiza Serikali kupunguza kodi ya asilimia 18 wanayotozwa kupitia mashine za kielektroniki (EFDs).

Wamefikia hatua hiyo ikiwa ni siku moja baada ya TRA kutangaza kufanya ukaguzi endelevu na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wale watakaokaidi kutumia mashine hizo.

Wakizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao walisema kuwa walifikia hatua ya kufunga maduka ili kupinga makato ya kodi kubwa inayowakosesha maslahi.

Mmoja wa wamiliki wa duka la nguo, Kibatala Kimweli, alisema ameamua kufunga duka ili asifanyiwe uhakiki na TRA, kwani tangu ameanza kutumia mashine hizo amebaini kupata hasara inayotokana na kukatwa kodi ya asilimia 18.

“Kilio chetu tunataka punguzo la kodi kwani ikiwa kubwa faida inakuwa ndogo, ndiyo maana mnaona hali hii ya mgomo inaendelea, kama walivyosema ni zoezi endelevu na sisi tutafunga maduka bila kuacha halafu tuone watatoa wapi kodi na nani atatumia mashine zao,” alisema.

Kimweli alitaja sababu nyingine za kufunga maduka hayo kuwa ni kutopatiwa elimu ya kutosha wafanyabiashara wengi, kama ilivyokuwa imeamuliwa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 22, mwaka huu.

Naye Halima Bakary, alidai kuwa mfumo unaotumiwa na Serikali unawatoza kodi kubwa, hali inayowafanya wafanyabiashara wengi kukwepa na kutumia njia nyingine zisizokubalika.

Akizungumzia kuhusu mgomo huo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema kwamba wao wataendelea kusimamia sheria kuhakikisha kila mfanyabiashara anatumia mashine hizo kwa ajili ya kulipa kodi.

“Sheria tunazozitumia zimetungwa na wabunge ambao ndio wanawawakilisha wafanyabiashara hao, hivyo suala la kusimamia sheria lipo mikononi mwa TRA na hawatakuwa tayari kusimamisha uhakiki wa mashine hizo kwa wafanyabiashara wadanganyifu na wale wasiozitumia kabisa, lazima watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

Kayombo aliongeza kuwa wafanyabiashara hao wameanza mgomo baada ya hivi karibuni kufanyika kwa ukaguzi wa kila duka na kubaini kuwapo kwa baadhi yao wanaotumia mashine ambazo hazijasajiliwa TRA, ikiwamo na wengine wasiozitumia.

Alisema kuwa wamebaini uwapo wa baadhi ya wafanyabiashara wasiotoa risiti halali kulingana na thamani ya bei ya bidhaa wanazouza.

Kayombo alisema TRA itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wanaoshawishi wenzao kufunga maduka na kuacha kutumia mashine za EFD’s, kwani hadi sasa tayari baadhi yao wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Aliongeza kuwa katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam maduka 70 yalibainika kutotumia stakabadhi, na kati yao 11 yamefungiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles