31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge la Katiba: Posho zazua balaa

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

Na Fredy Azzah, Dodoma

WAKATI vikao vya Kamati za Bunge Maalumu la Katiba vikiendelea mjini hapa, kundi la wajumbe wa Bunge hilo limeibuka na kulalamikia hatua ya kutolipwa posho za kujikimu.

Kutokana na hali hiyo    wajumbe hao ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao gazetini, wamedai wamekuwa wakiishi maisha ya tabu hali inayochangiwa na Ofisi ya Bunge Maalumu kushindwa kuwalipa posho za siku 11 mfululizo bila maelezo.

Wajumbe hao waliiambia MTANZANIA kuwa hawajalipwa posho tangu Agosti 16 mwaka huu, hali inayochangia kupungua kwa ufanisi wa kazi, hasa katika vikao vya kamati.

Kwa mujibu wa wajumbe hao,  hatua ya kutolipwa inatokana na hofu iliyotanda mjini Dodoma ya kuvunjika kwa Bunge ambako Wizara ya Fedha ililazimika kuzirudisha fedha hizo Hazina kwa hatua zaidi.

“Tunaishi kwa shida sana leo (jana) tuna siku ya 11 hatujalipwa na sababu haielezwi ni nini, maana sasa tunaishi kwa kuombaomba mikopo kutoka kwa ndugu na jamaa.

“Ila tambua sisi baadhi yetu wa kundi la 201 wengi wetu tuna uwezo wa kawaida tu tofauti na wenzetu ambao ni wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,” alisema mjumbe huyo.

Mjumbe huyo alisema kila kitu wanachofanya kuanzia kula na kuishi kinategemea fedha, hivyo kutokulipwa kunawafanya washindwe kutekeleza vema majukumu yao.

“Hata ukiangalia mitaani sasa hivi hawaonekani, yote ni kwa sababu hakuna fedha,” alisema mmoja wa wajumbe hao.

Kauli ya Bunge

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, alikiri kutolipwa kwa wajumbe wa Bunge hilo tangu Agosti 16.

Alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Bunge hilo zilikuwa hazitoshi kulipa posho yote kwa wajumbe hao hivyo walilipwa Sh 70,000 ya posho ya kikao pekee.

“Kwa siku wajumbe hao hulipwa Sh 300,000, kati yake Sh 70,000   ni posho ya kuhudhuria kikao kwa siku na Sh 230,000  ni posho ya kujikimu.

“Walikuwa wamelipwa sitting allowance (posho ya kikao) mpaka Jumamosi, fedha tulizokuwa nazo hazikutosha kulipa per diem mpaka tarehe 16, leo tutawalipa fedha zao mpaka tarehe 31.

“Tunawalipa wiki moja moja siyo kwa sababu ya ukosefu wa fedha wala kuogopa Bunge litavunjika, ni kwa sababu tukiwapa fedha nyingi sana watatoweka hawa, wao wanakasirika lakini tumeshauriana tukaamua tuwalipe hivyo,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini hapa, fedha za kulipa wajumbe hao kwa wiki iliyopita zilikuwapo lakini zilirudishwa Hazina.

Mwigulu afafanua

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alikiri fedha hizo kurudishwa Hazina.

Alisema fedha hizo ziliingia kwenye akaunti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa makosa badala ya akaunti ya Bunge Maalumu la Katiba.

“Hilo ni suala la utawala tu, fedha ziliwekwa A/C (akaunti) badala ya A/C ya Bunge Maalumu, kwa ajili ya accountability (uwajibikaji) Bunge Maalumu limefungua Akaunti Maalumu,” alisema.

Jinamizi la posho liliibuka Februari mwaka huu lilipoanza Bunge Maalumu la Katiba, ambako baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walilalamikia malipo ya Sh 300,000 kila wanapofanya kazi za Bunge hilo.

Wajumbe wa Bunge hilo la Katiba walijitokeza hadharani kudai nyongeza ya malipo hayo jana bungeni mjini Dodoma, katika kikao cha kupatiwa rasimu ya kanuni za kuongoza Bunge hilo.

Miongoni mwa walioibua suala hilo ni   Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa na Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi, wote ni wabunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndasa alisema Bunge hilo ndilo linalotengeneza Katiba lakini kiasi ambacho wabunge hao wanalipwa ni kidogo, kisichotosheleza mahitaji ya kuishi katika mji wa Dodoma.

Mjumbe huyo pia alilalamikia kitendo cha wajumbe wanaotoka Zanzibar kuongezewa posho na kudai kwamba kitendo hicho kinaleta ubaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles