31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wachina wa Magufuli waidai Serikali trilioni 1.3/-

Waziri John Magufuli
Waziri John Magufuli

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

WACHINA wa ‘samaki wa Magufuli’ walioachiwa huru wanadai meli na samaki zilizokuwamo, ambavyo vyote vina thamani ya Dola za Marekani 3,220,000.

Mbali na kutakiwa kulipa fedha hizo, pia inatakiwa kulipa Sh trilioni 1.3 ikiwa ni gharama zote, ikiwamo meli, samaki, mawakili na mabaharia wake.

Hayo yalisemwa  Dar es Salaam jana na Wakili wa Wachina hao, Kapten Ibrahim Bendera na Wakili John Mapinduzi, walipokuwa wakizungumzia hatima ya madai hayo.

“Tunadai meli na ikiwezekana na samaki waliokuwamo, thamani ya meli ya Tawaliq 1 kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Uvuvi ni Dola za Marekani milioni 2.5, thamani ya samaki zilizokuwamo ni Dola za Marekani 720,000.

“Hivi sasa  tunasubiri maelekezo kutoka kwa wenye meli ili tuendelee na mchakato wa madai hayo, wateja wangu wanaendelea na taratibu za kurudi kwao,” alisema Kapteni Bendera.

Wakili John Mapinduzi alisema Serikali inatakiwa kulipa gharama zote kuanzia meli, samaki, gharama za mawakili na mabaharia wake.

“Serikali italipa karibu Sh  trilioni 1.3, ile haikuwa meli ya kawaida, ilikuwa ni kama kiwanda, ilikuwa inafanya kazi ya kuvua na kusindika,” alisema.

Ijumaa iliyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru Wachina wa ‘samaki wa Magufuli’ na kuamuru Jamhuri iwarejeshee vitu vyao, ikiwamo meli ya Tawaliq 1.

Wachina hao waliachiwa kwa mara ya pili  kwa vile  mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28  mwaka huu, lakini walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.

Washtakiwa hao ni Nahodha wa meli, Hsu Chin Tai na Wakala wa Meli ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing, waliokuwa wakikabiliwa na mashataka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, aliwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Harufani.

“Mheshimiwa Hakimu, Jamhuri tunaifahamisha mahakama kwamba hatuna haja ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa, maombi yetu tunawasilisha chini ya kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002,” alidai Mwangamila.

Wakili wa washtakiwa, Kapten Ibrahimu Bendera, alikubaliana na maombi hayo na kuiomba mahakama iwarudishie hati zao za kusafiria, meli iliyokamatwa na                             samaki waliokuwamo ikiwezekana.

Mahakama  ilikubali kuwaachia huru washtakiwa wote na kuamuru warejeshewe vitu vyao vilivyokuwa vinashikiliwa.

Mahakama ya Rufaa iliwaachia Machi 28 mwaka huu na kuwafutia adhabu ya kifungo cha miaka 30 na faini ya Sh bilioni 22 waliyopewa baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu Februari 23 mwaka 2012  kwa   uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Washtakiwa hao waliachiwa baada ya Mahakama kubaini sheria zilikiukwa wakati wa uendeshwaji wa kesi hiyo katika mahakama za chini.

Washtakiwa waliachiwa na kukamatwa nje ya mahakama kisha kufunguliwa kesi mpya yenye mashtaka yanayofanana katika Mahakama ya Kisutu.  Walidaiwa kwamba wote kati ya Januari 10, 2009 na Machi 8, 2009 kwa pamoja walivua samaki bila leseni katika Ukanda wa Bahari wa Uchumi wa Tanzania.

Katika shitaka la  pili,  watuhumiwa  wote   walidaiwa kati ya Januari 10, 2009 na Machi 8, 2009 walichafua bahari na kuathiri viumbe vilivyomo ndani ya bahari kinyume cha sheria.

Jamhuri ilidai shtaka la tatu ni kwa ajili ya mshtakiwa Zhao Hanguin ambaye ni wakala wa meli.

Alidaiwa kuwa  huku akijua ni kosa kuvua samaki katika ukanda huo bila leseni, alimsaidia mshtakiwa wa kwanza kukwepa kuchukuliwa hatua na kupata adhabu kwa kosa alilotenda.

Washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2009 na boti ya askari wa doria wa   Tanzania, Afrika Kusini, Botswana.  Leseni waliyokuwa nayo ilikuwa imemaliza muda wake Desemba mosi, mwaka 2008.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. kichwa kisicho na akili huchongea Kiwiliwili. Serikali lipeni hizo fedha za walipa kodi na sisi wanyonge tuendelee kuteseka kwa shida ndani ya nchi yetu.

  2. Alipouza nyumba za serikali kwa bei wananchi na viongozi walikaa kimya, alipowaambia wakazi wa Kigamboni wapige mbizi watu walicheka, anapotumia lugha za kishairi kubeza na kukandamiza wapinzani hasa anpokuwa Bungeni baadhi ya watu umuita shujaa na Daktari wa kweli. Sasa hili la meli na mali zake limetuibua wengi na sasa ndipo tunapobaini kuwa Dk Magufuli, NI KIONGOZI WA KUKURUPUKA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles