23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwigulu afichua ufisadi wa kutisha Hazina

Mwigulu Nchemba
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Jonas Mushi na Raphael Nolescus (TUDARCO), Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amesema wameokoa zaidi ya Sh bilioni 40 zilizokuwa zilipwe kama mshahara wa mwezi uliopita kwa watumishi hewa 14,074 wa umma.

Pamoja na hilo, pia alisema Serikali itakuwa makini katika ulipaji wa madeni kwani tayari wamebaini kuwepo kwa madeni yasiyo sahihi ambapo katika deni la Serikali la shilingi bilioni 500 wamegundua deni sahihi ni shilingi bilioni 140.

Hayo aliyasema katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wakati akielezea kile ambacho Wizara imekibaini baada ya kubadilisha mfumo wa ulipaji wa mishahara.

Katika hilo alisema mfumo huo umewasaidia kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 40 za mwezi mmoja tu zilizokuwa ziliwe na wajanja wachache ambao walikuwa wakiutumia mfumo wa zamani wa kulipa mishahara kwa hundi katika kila taasisi.

“Wizara iliamua kubadili mfumo wa ulipaji mishahara kwa watumishi baada ya kubaini kuwepo kwa malipo hewa kwa mfumo wa zamani wa kulipa dirishani, ambapo taasisi za Serikali zilikuwa zikileta taarifa zisizo sahihi za wafanyakazi ambao wengine walishafariki, kuhamishiwa katika taasisi nyingine ama kuachishwa kazi,” alisema Nchemba.

Alisema mfumo wa sasa wa kulipa mishahara kwa kutuma moja kwa moja katika akaunti ya mtumishi, unaondokana na kusainisha majina ya watu wasiokuwepo kwani kila mtumishi atapaswa kuwa na akaunti na malipo yatafanyika kutokea hazina moja kwa moja.

Alisema wanataka kuona keki ya taifa inayopatikana inagawanywa sawa ili kupunguza tabaka kubwa la walionacho na wasionacho, hivyo mishahara hewa inayolipwa inaweza kutumika katika shughuli za maendeleo ya kijamii.

Akizungumzia madeni yasiyo sahihi, Mwigulu alisema kuna watendaji wasio waadilifu ambao wamekuwa wakiongeza madeni wanayoidai Serikali ili wajinufaishe wenyewe.

Alitolea mfano wa mtendaji ambaye hakutaka kumtaja kwa kile alichodai kuwa vyombo vya dola tayari vinashughulikia suala hilo, kwamba aliongeza tarakimu katika kiasi kilichokuwa kikidaiwa na mwalimu mmoja.

Alisema badala ya Sh milioni tano zilizokuwa zikidaiwa ikawa Sh milioni 500 na mwalimu huyo alipohojiwa alisema yeye hadai kiasi hicho.

“Tayari mimekwisha agiza vyombo vya dola vimshughulikie mtendaji huyo na sitaki kumtaja asije akatoroka au kufanya njama zozote za kukwepa mkono wa dola,” alisema Nchemba.

Akionya kuhusu mwenendo huo wa ufisadi, Mwigulu alisema: “Kila mmoja atimize wajibu wake na afuate maadili ya kazi yake, tumepeleka fedha za maendeleo ya miradi na tutahitaji taarifa sahihi za matumizi ya fedha hizo na atakayefanya ubadhirifu wowote hatutasita kumchukulia hatua za kisheria.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles