27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Katiba ya Tanganyika yaingizwa kwenye Muungano

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

NA FREDY AZZAH, DODOMA

WAKATI Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiendelea na msimamo wa uwapo wa mfumo wa Serikali tatu, Bunge Maalumu la Katiba limeanza kujadili baadhi ya sura ambazo ziliachwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya Katiba ya Tanganyika.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alisema sura hizo ni pamoja na ile ya Serikali za Mitaa na suala la ardhi.

Kwa mujibu wa iliyokuwa Tume ya Warioba, maeneo hayo yaliachwa kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika.

Sitta alisema kuwa suala la Serikali za Mitaa liliwasilishwa kwenye Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, ambaye alilitoa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).

Alisema waziri huyo aliwasilisha andiko la Jaji Warioba kuhusu ardhi, maliasili na rasilimali za taifa lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya Katiba ya Tanganyika.

“Tumechukua hayo ya tume ili kuendelea kuiboresha rasimu yetu hii tuliyonayo,” alisema.

Alisema kuwa pendekezo jingine kutoka kwa wajumbe wa Bunge hilo ni malengo ya maendeleo, uchumi na jamii.

“Tunataka Serikali isione kuwa kazi yake ni kuongoza watu tu, wajue kwamba wanatakiwa kuhakikisha wanawaendeleza watu kiuchumi,” alisema Sitta.

Katika hatua nyingine, alisema kuwa Kamati ya Uongozi imeunda kamati ndogo ya watu 10 kupitia suala la Mahakama ya Kadhi, uraia pacha na muundo wa Bunge.

Alisema kuwa kamati hiyo inaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu na ina wajumbe watano kutoka Zanzibar na watano kutoka Bara.

Sitta alisema kuwa kamati zote zinatarajiwa kumaliza kazi zake Agosti 27, na Septemba 2 wajumbe wataanza kujadili sura zote.

Alisema pamoja na hali hiyo, wajumbe wamependekeza Katiba mpya itambue haki za walaji ili iwapo mtu akinunua kitu kibovu imlinde.

“Baada ya kazi ya Bunge kwisha, tutakuwa na Katiba bora Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, Katiba ya viwango kabisa,” alisema Sitta.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Hawa ccm wasidanganye wananchi kwa kuwataka ukawa kurudi huku wakiwa wamesha ichakachua yote sasa waende kujadil nn na wakati wameibomoa yote? Ukweli ni kwamba hawana katiba bora ya taifa labda ya chama chao na wasilazimishe matakwa ya chama chao kuwa ya taifa .

  2. SUALA LA MAHAKAMA YA KADHI NCHI YA TANZANIA HAINA SURA YA KIDINI KAMA INGEKUA INA SURA YA KIDINI INGEKUA NI NCHI YA KIKRISTO NA SIO VINGINEVYO. KADHI HII NI MLENGO WA DINI YA KIISLAM ASILI YAKE NCHI ZA KIARABU NDIKO KULIKO NA MIFUMO HIYO YA KADHI LAKINI SIO TANZANIA. MACHAFUKO YATAINGIA ENDAPO HAMTATUMIA AKILI NA HEKIMA JUU YA SUALA HILO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles