31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu za Magufuli kutohudhuria sherehe ya mabalozi

MAGU+PHOTONa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HATUA ya kutoonekana kwa Rais Dk. John Magufuli katika sherehe ya kutakiana heri ya mwaka mpya na wanadiplomasia (Sherry Party), imezua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania.

Kutokana na kutokuwapo kwa rais katika sherehe hiyo iliyofanyika juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, alimwakilisha na alisoma hotuba kwa niaba yake.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, alisema ilikuwa ni sahihi kwa Rais Magufuli kuwakilishwa na Waziri Mahiga katika sherehe hiyo.

Alisema hatua hiyo ilitokana na Rais Magufuli kuwa nje ya Dar es Salaam, ambapo asipokuwapo huwakilishwa na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya Nje.

“Rais alikuwa nje ya Dar es Salaam ndiyo maana akawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na ‘Sherry Party’ ni hafla ya kutakiana heri ya mwaka mpya na wanadiplomasia.

“Na Cocktail (mchapalo) hufanyika kila mwaka na huwa ya muda mfupi ambao wanadiplomasia husikiliza hotuba ya rais kuhusu sera yake ya mambo ya nje. Hivyo kwa kuwa Rais Magufuli hakuwepo, hotuba yake ilisomwa na Waziri Mahiga jambo ambalo ni sahihi na hakuna kosa lolote,” alisema Msigwa.

Akizungumza suala la mabalozi hao kuwekewa makatarasi chini, alisema si karatasi za kawaida, huwa zimeandikwa jina la balozi au nchi anayowakilisha ambapo hutakiwa kusimama katika eneo lake husika alilopangiwa.

“Suala la kuwekewa karatasi mbele si geni, huwa linafanyika kila mwaka na pindi zinapowekwa huandikwa jina na cheo cha mwanadiplomasia anayewakilisha nchi husika, na baada ya kusomwa hotuba hupita mbele na kumpa mkono kiongozi.

“Na kwa jana (juzi), aliyesimama mbele alikuwa ni Mheshimiwa Waziri Dk. Mahiga, naibu waziri pamoja na mkuu wa itifaki, na walifanya hivyo kwa sababu walikuwa wakimwakilisha Rais Magufuli katika hafla,” alisema.

 

Balozi Cisco atoa maoni

Aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Falme za Kiarabu, Abdul Cisco Mtiro, alisema alichofanya Rais Magufuli kutuma mwakilishi katika hafla hiyo haijawahi kutokea tangu Serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne.

“Ni kweli Rais Magufuli ndiye kwa mara ya kwanza amefanya kitu tofauti na marais wote waliomtangulia kutuma mtu kwa niaba yake, hiyo haijawahi kutokea,” alisema Balozi Mtiro.

Balozi Mtiro ambaye ni mwanadipomasia aliyebobea, alisema hafla hizo ambazo hufanyika kila mwaka humwezesha rais husika kutoa mwelekeo wa nchi yake katika sera ya Serikali kuhusu mambo ya nje.

“Sherry Party ni Standard Party na kwa kawaida huchukua dakika zisizozidi 30 ambapo rais hatoa ‘speech’ (hotuba) ya dakika tano kuelezea mwelekeo wa sera ya nchi yake kuhusu mambo ya nje na baadaye hupeana mkono na mabalozi na kuondoka.

“Sherry Party ni hafla ambazo hufanyika kila mwaka ambapo ambapo rais anakutana na mabalozi, hakuna viti, ndiyo maana uliona vile vikaratasi vya majina ya mabalozi kuwekwa pale ingawa utaratibu ni kwamba mabalozi wenyewe wanajua utaratibu kwamba nani alitangulia kutoa hati za utambulisho katika lile kundi, ndiyo wanafuata wengine kadiri walivyoingia nchini.

“Ni utamaduni wa nchi za Jumuiya ya Madola, na Uingereza ambako ndiko tulichukua utamaduni huo, zamani ilitumika soda na maji, lakini miaka ya karibuni vinawekwa pia vinywaji vikali,” alisema.

 

PROFESA LIPUMBA

Akizungumza hali hiyo katika moja za makala zake, Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mabalozi wengi waliopo hapa nchini na ambao nchi zao zinaisaidia Tanzania wameomba fursa ya kukutana na Rais Magufuli lakini wamekwama.

Kutokana na hali hiyo alisema kiongozi huyo wa nchi ameendelea kuwabeza mabalozi waliopo hapa nchini kwa kutohudhuria sherehe maalumu ‘Sherry Party’ ambayo rais huwaandalia mabalozi na kuwaeleza sera na malengo yake ya kuboresha uhusiano wa Tanzania na mataifa ya nje.

“Katika Sherry Party ya mwaka huu, rais kawakilishwa na Dk. Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje. Kwa kuwa Rais Magufuli ndiyo kaingia madarakani, mabalozi wengi walikuwa na shauku ya kumuona na kumsikiliza,” alisema.

 

HOTUBA YA MAGUFULI

Katika hotuba yake kwa wanadiplomasia hao iliyosomwa na Waziri Mahiga juzi, Rais Magufuli alisema hatua ya kurudia uchaguzi Zanzibar ndiyo njia sahihi ya kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani humo.

Alisema kufanyika uchaguzi huo wa marudio kutasaidia kuondoa mvutano wa kisiasa uliopo na kusisitiza kuwa mazungumzo kati ya vyama vya siasa yaliyoanza Novemba mwaka jana, hayakufikia mwafaka wa namna ya kutatua tatizo hilo.

“Zanzibar ina mfumo wake wa siasa, ina Katiba na ina Tume Huru ya Uchaguzi. Hatua ya kufanya uchaguzi ndiyo njia sahihi katika hali ya sasa katika kumaliza tatizo hilo.

“Chama kikuu cha upinzani (CUF) wanadai wameshinda, lakini chama tawala na vyama vingine vinaona haja ya kufanya uchaguzi wa marudio ili kuondoa kasoro,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema mlango wa mazungumzo juu ya namna ya kufanya uchaguzi wa marudio kuwa huru na haki na kufuata taratibu za kimataifa uko wazi na kuwa ni imani yake nchi marafiki wa Zanzibar na Tanzania wataunga mkono juhudi hizo.

“Kama ilivyo kwa Watanzania wengi wanavyoona, njia ya kuthibitisha ushindi ni boksi la kura na kukataa kushiriki ni kukataa kufikia mwafaka na Serikali na kujinyima haki ya miaka mitano ijayo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema bado kuna siku 40 ambazo zinatosha kuwa na mazungumzo ya kuja na suluhisho la tatizo hilo.

Zanzibar inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio Machi 20 kutokana na uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mabalozi waliopo nchini, ambaye pia ni Balozi wa Zimbabwe, Edzai Chimonyo, alisema mgogoro wa Zanzibar unaweza kumalizwa kwa mazungumzo ya pamoja visiwani humo.

Alisema wananchi wa Zanzibar wanapaswa kuweka tofauti zao pembeni na kujali masilahi ya nchi kwa masilahi yao na taifa lao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles