27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mramba, Yona wajiandaa kusafisha hospitali leo

1.Basil-Mramba-na-Daniel-Yona-wakiwa-mahakamani-hapo-leo.Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, ambao walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka miwili jela, kuanzia leo wataanza kutumikia kifungo chao cha nje kwa kufanya usafi katika Hospitali ya Palestina, Sinza,   Dar es Salaam.

Mawaziri hao walibadilishiwa adhabu ya jela na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje mwishoni mwa wiki iliyopita na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukamilika   mchakato wa kufikia hatua hiyo.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, alisema sheria ya huduma kwa jamii namba 6 kifungu namba 3(1) ya mwaka 2002 inasema mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni miaka mitatu kushuka chini, mahakama inaweza kumpa adhabu ya kutumikia jamii.

Mramba na Yona ambao baada ya rufaa walibakiwa na adhabu ya miaka miwili, walitiwa hatiani kwa kutumia madaraka vibaya na walitakiwa kumaliza kifungo Novemba 2016.

Hata hivyo, Hakimu huyo alisema Magereza walifikisha barua mahakamani hapo Desemba 5 mwaka jana, yenye kumbukumbu namba 151/DAR/3/11/223, wakipendekeza kifungo cha nje kwa mawaziri hao.

Hakimu Mkeha, alisema baada ya kuipokea barua hiyo mahakama iliamuru watu wa huduma za jamii kuchunguza kama wanastahili kupewa adhabu hiyo na   walifanya hivyo na kurudisha ripoti kwamba wanastahili.

Alivitaja vigezo vya kupewa adhabu hiyo kuwa ni umri.   Mramba na Yona wana miaka 75.

Kigezo kingine ni endapo wahusika ni wakosaji wa mara ya kwanza, na kingine ni kama watuhumiwa wanajutia kosa lao na wanakubali kuitumikia jamii bila kulipwa na kuangalia umbali wanakoishi na eneo analokwenda kufanyia shughuli za jamii pamoja na tabia za washtakiwa.

Alisema sheria haijapendekeza makosa yapi wasipewe kifungo cha nje, isipokuwa inatamka kwa yeyote aliyefungwa kuanzia miaka mitatu kushuka chini.

“Mramba na Yona baada ya kuridhika kwamba wanashtakiwa, wamepangiwa kufanya usafi Hospitali ya Palestina Sinza kila siku kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa na watatumikia mpaka Novemba 5, 2016.

“Watakuwa wanafanya kazi kwa saa nne, wenyewe wameridhia kutumikia adhabu hiyo na endapo watakaidi watarudishwa kifungoni,” alisema Hakimu Mkeha.

Hata hivyo, Mramba na Yona walirudi gerezani kwa ajili ya kukamilisha taratibu, wanatarajia kuanza kutumikia adhabu hiyo Jumatatu.

Julai 6  2015, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh milioni tano, Mramba na Yona, huku ikimuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, baada ya kumuona hakuwa na hatia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles