31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SUMAYE: TUNAPITIA WAKATI MGUMU


NA  OSCAR ASSENGA, TANGA.

WAZIRI MKUU mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Fredrick Sumaye amesema upinzani unapitia wakati mgumu kuliko nyakati zingine.

Amesema kutokana na hali hiyo,demokrasia ya kweli ya vyama vingi, inapoteza mwekeleo kwa sababu kumekuwapo na chaguzi nyingi za marudio ambazo zinazoigharimu Serikali fedha nyingi.

“Tunafanya chaguzi nyingi ambazo zinaigharimu Serikali fedha za walipa kodi wa nchi hii ambazo zingetumika kuwasaidia kuleta maendeleo mengine,”alisema Sumaye.

Sumaye, aliyasema hayo juzi,wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa udiwani wa Kata ya Makorora, Zainabu Ashirafu.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kumpigia kura mgombea wa Zainabu kupitia chama hicho ili waletee maendeleo.

Alisema fedha nyingi ambazo zinatumika kwenye uchaguzi hizo, zinapotea kwa sababu zingeweza  kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwamo za afya na elimu ili kuhakikisha wanaondokana na vikwazo kwenye maeneo hayo.

Alisema kunapokuwa na demkorasia ya kweli, watu wakishachagua viongozi ambao wanawataka kutokana  na sera ya vyama vyao ambavyo vitawafaa, hauwezi kwenda kuwachokonoa, badala yake unatakiwa kuacha uamuzi wa wananchi usimame kwa kipindi kinachoruhusiwa kikatiba ambacho ni miaka mitano

“Leo (juzi),tunarudishwa kwenye uchaguzi wa kata 72, uchaguzi unagharimu zaidi ya milioni 70…uchaguzi wa kata unagharimu zaidi ya milioni 250,madiwani walio wengi wa kata leo tunarudia uchaguzi wametoka kwa sababu ya kununuliwa, ni wachache waliofariki dunia… hapo ndio unajua hakuna demokrasia,”alisema Sumaye.

Alisema penye demokrasi makini chama kinachotawala kinatakiwa kutumia fedha kwenye maendeleo ya watu na sio kununua watu vitendo vinaonyesha ukandamizishaji kwani zingeweza kuzitumia  kwenye kusaidia miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na shule za sekondari za kata ambazo zimekuwa changamoto kwa baadhi ya maeneo.

“Makorora mnazahanati nyie…mna shule ya sekondari ya kata? fedha hizo zinapotea zingeweza kuwasaidia kuondoa changamoto mbalimbali maeneo yenu,tunapoteza muda wananchi kwa mwezi mzima,”alisema Sumaye.

Alisema wananchi watakuja kujuta, wakati majuto ni mjukuu kama vyama vya upinzani havitafanya kazi kwa sababu ya nguvu ya serikali  na watakaogeukiwa baadae ni sisi wana CCM kwani hata wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 sote tuliimba wataisoma namba lakini hivi sasa ni wote ambao wanakumbana na dhahama hiyo.

“WanaCCM tuliimba wimbo wa wataisoma namba, sasa kila mahali wanaisoma namba, nataka niulize wana CCM namba tunaiusoma sisi pekee yetu au wote..hali mbaya ya uchumi iliyosambaa imewaacha wana CCM jibu ni hapana

kwani kila mtu anaisoma,”alisema

Alisema upinzani unapokufa,Watanzania watarudi kwenye mfumo wa  chama kimoja na  vyama vya vibaraka vingi na hakuna mtu atakayehangaika kuwahudumia wananchi.

Alisema lengo la upinzani ni kusaidia kuikosoa Serikali pale inapokosea.

Sumaye, alisema Watanzania waache tabia ya kufikiria upinzani ni uadui,unatakiwa kufutwa kwani ukifa amani itatoweka kutokana na uwopo wa chama kimoja

“Niwaambie CCM ikiendelea na utaratibu huu, wananchi wenyewe ndiyo watateseka,tunaomba lisitokee…nimetoka CCM nimekuwa Waziri Mkuukwa miaka 10,  sikupata faida yotote, nilitaka tuje kuleta nguvu ya vyama na nguvu ipo ndio maana CCM inaiogopa,inanunua madiwani na wabunge,”alisema.

Naye kwa upande wake,Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga,Yosepher Komba (Chadema), alisema wananchi wasipokuwa na msimamo utakuwa ni mchezo wa kuigiza kwani wanaweza kujikuta wakifanya uchaguzi kwa kipindi chote cha miaka mitano kuliko iliyokuwa miaka ya nyuma ambapo kiongozi akichaguliwa anasubiri miaka mitano ndio uchaguzi au labda itokee amefariki dunia.

“Niwaambie watu wa Tanga, tunakumbuka maisha yetu miaka 80 wakati ukiwa mkoa wa  viwanda,hivi sasa serikali ya awamu ya tano imekuwa inasema ni kujenga viwanda niwaulize tokea serikali imeingia madarakani,imejenga vingapi kama sio kuwanunua viongozi wa upinzania nchi nzima,”alihoji.

ZITTO

Akiwa katika mkutano wa udiwani mjini Kilwa mkoani Lindi jana, kwa mwaliko wa Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala (Bwege), kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema anashangazwa na watu wanaotoka upinzani kwa ahadi za kuteuliwa ukuu wa wilaya, nafasi ambazo siku yoyote wanaweza kunyang’anywa.

Alisema anashangazwa kuona mtu amepata fursa ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa kuaminiwa na wananchi, halafu anatoka kwa sababu ameahidiwa ukuu wa Wilaya na sababu nyingine nyepesi.

“Watu wanaacha ubunge kwenda CCM ili wateuliwe ukuu wa wilaya, ninawaambia wananchi msivunjike moyo, hao hawajui wanafanya nini,” alisema.

Alisema safari ya kupigania demokrasia ni ngumu lakini anaifananisha na treni inayokwenda Kigoma, ambayo katika kila kituo kuna abiria wanaoshuka na wanaopanda, kuna wengine wakishuka Luiche, kituo kimoja tu kabla ya kufika mwisho wa safari

“Kuna watu ambao hawataki shida, ni wepesi kukata tamaa wasituambukize woga wao na jambo kubwa kuliko yote ni kwamba tunapaswa kupambana kwa ajili ya kupanua zaidi demokrasia na ushirikiano wa upinzani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles