23 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

TCRA YAWAONYA UWOYA, MOBETTO

NA AZIZA MASOUD,DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewapa onyo na kuwataka kuomba radhi mwanamitindo na mjasiriamali Hamisa Mobetto na mwigizaji Irene Uwoya, kutokana na kukiuka kanuni za maudhui mtandaoni 2018, kwa kuchapisha picha za utupu katika mtandao wa Instagram.

Katika shauri lililosomwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui TCRA,  Valerie Ndeneingo Sia Msoka, lilisema Hamisa alikiuka kanuni hizo Juni 23 na Aprili 10, mwaka huu, kwa kuchapisha picha Instagram zinazomwonyesha mama mjamzito akiwa ameshika tumbo juu kidogo ya sehemu za siri akiwa katika mitindo mbalimbali ya utupu, zinazohamasisha watoto kuiga tabia mbaya.

Msoka alisema Mobetto alikubali hizo picha ni zake na alizipiga akiwa nchini Kenya kwa malipo mwaka jana, kabla ya kupitishwa kwa sheria hizo za mtandaoni na hakuchapisha katika kurasa zake, hivyo ni ngumu kuwataka watu wengine wazifute picha zake.

“Kwa kuwa amekiri picha ni zake, kamati inaona anawajibika kama ifuatavyo: Hamisa anapewa onyo, endapo atatenda tena kosa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake, pili, aombe radhi na kuwaelimisha mashabiki zake juu ya matumizi ya picha zisizo na maadili,” alisema Msoka.

Kwa upande wa Irene Uwoya, Msoka alisema  mrembo huyo alichapisha picha kwenye mtandao wake wa Instagram Juni 26, mwaka huu, zikionyesha maungo yake, hivyo kuhamasisha ngono, kinyume cha maadili ya Tanzania.

Msoka alisema baada ya mashauriano, Uwoya alikiri kosa na kuomba radhi, huku akisema alifanya hivyo kwa kumuiga ‘role model’ wake, ambaye ni Beyonce.

“Kwa maelezo ya Irene Uwoya, kamati ya Maudhui imeamua kumpa onyo, endapo atatenda tena kosa hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa, kamati inaamua Irene aombe radhi katika ukurasa wake wa Instagram,” alisema Msoka.

Baada ya kumalizika kwa shauri hilo, saa moja baadaye, Hamisa na Irene waliomba radhi na kuhamasisha jamii kupitia kurasa zao za Instagram kutokuchapisha picha zenye ukakasi kwa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles