31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NCAA YAJIPANGA KUFIKIA WATALII MILIONI 5

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA      |   

MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), imeanza utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli la kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2020.

Hayo yalisemwa juzi na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Japhet Hasunga, alipokuwa akifungua jukwaa la wawekezaji katika sekta ya utalii lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) mjini hapa.

Akizungumza na wawekezaji kutoka kampuni za mawakala wa utalii, wamiliki wa mahoteli, kambi za kitalii na wadau wengine wa sekta hiyo, Hasunga alisema watatumia jukwaa hilo kufikia malengo yanayotarajiwa.

“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeelekeza hadi kufikia mwaka 2020, tuwe tumefanikiwa kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni 2.

“Lakini, lengo hilo limesharekebishwa na Rais Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye uzinduzi wa ujenzi wa rada nne, ambapo aliagiza ifikapo mwaka 2020, tuwe tumefikia watalii milioni 5.

“Kuandaliwa kwa jukwaa hilo na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kunatoa fursa pana ya kuwasikiliza wawekezaji hao kutoka sekta ya utalii ikiwamo kufanya nao kazi kwa pamoja.

“Lengo la jukwaa hili ni kuwaleta pamoja wawekezaji hawa ili tujadiliane nao na kuzungumzia maendeleo ya sekta hii ya utalii ikiwamo kuona vivutio katika eneo letu la Ngorongoro.

“Tumewaita ili kuona ni uwekezaji wa aina gani unatakiwa kuwapo kwenye eneo hilo, kwani tayari tumeshawatembeza kwenye baadhi ya maeneo,” alisema Hasunga.

Kwa upande wake, Naibu Mhifadhi anayeshughulikia Uhifadhi, Maendeleo ya Jamii na Utalii, Dk. Maurus Msuha, alisema jukwaa hilo limefanyika kwa lengo la kuongeza uwekezaji kutokana na kuwa na vivutio vingi.

“Tumekuja kuwaeleza wawekezaji fursa zilizopo, pia namna gani tunaweza kushirikiana kutumia fursa hii ya upekee wa Bonde la Ngorongoro,” alisema Dk. Msuha.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles