23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

‘ATCL YAJIENDESHA KWA HASARA’

NA ESTHER MBUSSI -DODOMA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imebaini uendeshaji usioridhisha na matumizi makubwa kuliko mapato kwa baadhi ya mashirika likiwamo Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lililopata hasara kwa miaka mitatu mfululizo.

Kwa upande wake Kamati ya Bunge ya Bajeti imebaini kuwa Serikali imetekeleza bajeti yake ya kipindi cha nusu mwaka kwa asilimia 40.5 tu.

PIC ikisoma taarifa yake, ilizitaja taasisi nyingine zilizopata hasara kuwa ni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan-Trade), Chuo Kikuu Mzumbe, Shirika la Elimu Kibaha, Bodi ya Utalii (TTB), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB).

Akizungumza bungeni jana, Mwenyekiti wa PIC, Albert Obama, alisema hatua hiyo inatokana na kukosekana kwa usimamizi madhubuti huku baadhi ya mashirika na taasisi yanafanya uwekezaji wa mitaji ya umma bila kuzingatia sheria na mengine yanawekeza kwa kutumia mitaji ya umma lakini yamekosa mikakati ya kulipa madeni na kuendelea kutegemea ruzuku serikalini.

ATCL

Akizungumzia kuhusu ATCL alisema kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2014/2015 ilipata hasara ya Sh bilioni 94.3 na mwaka 2015/2016 ilipata hasara ya Sh bilioni 109.2 na mwaka 2016/2017 ilipata hasara ya Sh bilioni 113.7

“Katika kipindi hicho matumizi yaliongezeka kwa kiwango cha juu kulinganisha na mapato yaliyopatikana na hali hiyo ikiendelea hivyo uhai wa kampuni hiyo utakuwa shakani,” alisema.

TAN TRADE

Kuhusu Tan-Trade alisema imekuwa na matumizi makubwa kuliko mapato hali iliyosababisha nakisi ya Sh milioni 397.9 kwa mwaka 2013/2014, Sh milioni 614.6 kwa mwaka 2014/2015 na Sh milioni 838.2 kwa mwaka 2015/2016.

“Uchambuzi umebaini kuwa ongezeko hili la matumizi limechangiwa na ongezeko la matumizi mengineyo, mishahara na gharama za utawala wakati gharama za uwekezaji yaani gharama za maonyesho na kutangaza bidhaa na gharama za utafiti zimepungua kutoka asilimia 32.5 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 16.8 mwaka 2015/2016 ambazo zilipaswa kupanda ili kukuza kipato cha taasisi.

“Pia kupungu kwa uwekezaji kumeathiri mapato yatokanayo na upangishaji kipindi kisicho cha maonyesho, maonyesho ya viwanda, elimu na uhuru ambapo mapato yalipungua kutoka asilimia 22.3 ya mapato yote mwaka 2011/2012 hadi asilimia 8.5 ya mapato yote mwaka 2015/2016,” alisema.

Alisema hali hiyo imechangia kushuka kwa mapato mengineyo kutoka Sh bilioni 1.117 mwaka 2011/2012 hadi Sh bilioni 546.9 mwaka 2015/2016.

SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA

Pia alisema nakisi ya wastani wa Sh bilioni 1.2 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo katika shirika hilo.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo imeongezeka kutoka shilingi milioni 482 mwaka 2012/2013 hadi shilingi bilioni 3.2 mwaka 2014/2015, aidha katika miaka miwili ya mwisho nakisi imekuwa ikipungua hadi kufikia shilingi milioni 955 kwa mwaka 2016/2017.

“Katika upande wa vipaumbele, kamati imebaini kuwa baadhi ya taasisi zinazofanya uwekezaji wa mitaji hazina vipaumbele katika kuwekeza mitaji yake kwenye miradi ya maendeleo mfano Shirika la Suma JKT ambali limeshindwa kukamilisha miradi yake kwa kuwa haikuweka vipaumbele.

“Taasisi zimekuwa zikifanya uwekezaji mkubwa kwenye miradi ambayo haiendani na jukumu la msingi la kuanzishwa kwake kwa mfano Chuo Kikuu Mzumbe kwa kiasi kikubwa kimeacha jukumu lake la msingi la kuwekeza kwenye taaluma na kujikita kwenye miradi ya majengo na ardhi ambapo mtaji wake umetawanywa kiasi cha kugeuka mzigo mkubwa wa kulipa kodi ya ardhi na majengo ambayo hayajaanza kuzalisha,” alisema.

KAMATI YA BAJETI

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wake, Hawa Ghasia, alisema imebaini kwa ujumla Serikali imeweza kutekeleza bajeti yake ya kipindi cha nusu mwaka kwa asilimia 40.5 tu kutokana na changamoto mbalimbali.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni kama vile Sekta ya Afya na Maji kupata mgawo mdogo wa fedha ukilinganisha na mahitaji halisi ya sekta hizo zinazogusa maisha ya wananchi wengi.

“Sekta ya afya ilipata mgao wa shilingi bilioni 84 kati ya shilingi bilioni 168.2 zilizopangwa kwa nusu mwaka ambazo ni fedha za ndani.

“Sekta ya maji mjini na vijijini ilipata mgao wa shilingi bilioni 103.5 kati ya shilingi bilioni 204.3 zilizopangwa kwa nusu mwaka.

“Sekta ya kilimo ilipelekewa shilingi bilioni 11.3 kati ya shilingi bilioni 29.8 zilizopangwa kwa nusu mwaka ambazo ni fedha za ndani.

“Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambazo zinahudumia wananchi wengi zimepokea shilingi bilioni 165.9 kati ya shilingi bilioni 264.8 sawa na asilimia 31.36 tu ya fedha za ndani,” alisema.

Pia alisema Serikali bado haijakamilisha tathimini ya kubaini uwezo wa nchi kukopa na kulipa madeni ili iweze kukopa mikopo yenye masharti nafuu katika soko la kimataifa kwa lengo la kugharamia nakisi ya bajeti.

Alisema hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana Serikali ilikuwa imekusanya Sh trilioni 12.955 kati ya Sh trilioni 31.7 ilizokusudia kukusanya mwaka huu wa fedha.

Pia alisema kati ya fedha hizo zilizokusanywa, mapato ya ndani ni Sh trilioni 11.926 na ya nje Sh trilioni 1.028.

Alisema fedha zilizokusanywa zimetumika kwa matumizi ya kawaida ya Sh trilioni 9.815 na matumizi ya maendeleo Sh trilioni 3.14.

“Katika kipindi cha nusu mwaka, Serikali imefanikiwa kukusanya asilimia 44.4 ya mapato yote yaliyoidhiniswa na Bunge katika mwaka mzima. Kamati pia imebaini mwenendo wa makusanyo hadi kufikia nusu ya mwaka, Serikali imeweza kukusanya mapato kwa asilimia 82.8 ya malengo yaliyowekwa katika kipindi hicho,” alisema.

PATO LA TAIFA 

Ghasia aliongeza kuwa katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka jana, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 6.8 na ukuaji huo ukichangiwa zaidi na sekta za uchimbaji madini, habari na mawasiliano, biashara, ujenzi na uzalishaji wa viwanda.

Alizitaja sekta ambazo hazikuwa na ukuaji wa kuridhisha kuwa ni huduma za fedha, kilimo, upangishaji wa majengo na utawala.

BENKI KUFUNGWA

Kuhusu benki kufungwa alisema kamati yake inaishauri Serikali kupitia Benki Kuu (BoT) kuanzisha kitengo maalumu chini ya Idara ya Usimamizi wa Benki ili kiwe na jukumu la kuhakikisha bodi za benki za jamii zinaendeshwa kwa weledi na ufanisi na kuzisaidia kutoa ushauri wa kitaalamu.

Alisema kamati yake imebaini benki za jamii zimekumbwa na msukosuko baada ya benki tatu kuwekwa chini ya uangalizi na tano kufungwa kati ya benki 12 kutokana na usimamizi mbovu wa bodi zake.

KAMATI YA VIWANDA

Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilibainisha matumizi mabaya na yasiyo ya lazima ya fedha yanayofanywa na taasisi za Serikali.

Pia ilibaini muendelezo wa malimbikizo ya madeni ya Serikali inayodaiwa na taasisi binafsi ikiwamo Kiwanda cha Coca Cola, Kiwanda cha Pepsi (SBC) na Kiwanda cha Bakhresa.

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo bungeni jana, Mwenyekiti wake, Suleiman Saddiq, alizitaja baadhi ya taasisi ambazo hazifanyi vizuri kuwa ni Mradi EPZA, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Kiwanda cha General Tyre.

KIWANDA CHA GENERAL TYRE

Akizungumzia kiwanda hicho, alisema kamati haioni jitihada za dhati za kukifufua kwa sababu mara kwa mara imekuwa ikiomba taarifa ya utekelezaji wake na kupata taarifa zisizoridhisha.

Alisema mwisho wa mwaka wa fedha wa 2016/2017 Serikali ilikuwa haijatekeleza jambo lolote la kufufua kiwanda hicho bali iliamua kuunda tena kamati ya wataalamu kwa ajili ya kufanya tena upembuzi yakinifu ambao ungeshirikisha wadau mbalimbali.

“Kutokana na hali hiyo, kamati inaishauri serikali kufanya uamuzi stahiki na ili mradi huu utekelezwe wapewe wawekezaji binafsi jambo litakalopunguza majukumu.

“Lakini kama itashindwa ni vema kubadilisha matumizi ya ardhi ya mradi na fedha zinazotengwa zipelekwe katika miradi mingine inayotekelezeka na kuacha kupoteza muda na fedha katika mradi huo,” alisema.

EPZA

Alisema kamati yake inashauri kufutwa kodi zote za ardhi kwa maeneo yote yanayotambuliwa na kumilikiwa na EPZA ili kuipunguzia mzigo wa uendeshaji.

Alisema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba EPZA kumiliki ardhi kwa niaba ya Serikali kwa hiyo kuitoza kodi ya ‘premium’ na kodi ya ardhi ni sawa na kuomba fedha hazina na kuzirudisha hazina jambo ambalo ni usumbufu na gharama zisizo za lazima.

“Kuna baadhi ya maeneo yalikwishabainishwa na taratibu za awali za kuyaendeleza zilishakamilika lakini utekelezaji umekuwa ukienda taratibu jambo linalosababisha wananchi kushindwa kufanya shughuli zao za maendeleo na uzoefu huu umesababisha wananchi kuwa wazito wanapotakiwa kutoa maeneo yao kwa ajili ya miradi ya EPZA.

“Mfano mzuri wa ucheleweshaji ni eneo la EPZA-Kurasini ambapo mradi huu umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2011 ambapo takribani miaka saba sasa hakuna jambo ambalo EPZA inaweza kujivunia kuwa limefanikiwa,” alisema.

MADENI YATOKANAYO NA KODI YA SUKARI

Kuhusu upatikanaji wa vibali vya kutoa sukari vya viwandani bandarini na nyongeza ya asilimia 15 ya kodi ya kuingiza sukari ya viwandani, Saddiq, alisema kuna usumbufu usio wa lazima wa uagizaji huo.

Alisema hatua hiyo inasababisha baadhi ya viwanda kupunguza uzalishaji na vingine kufungwa kabisa.

“Pia wawekezaji wanalalamikia asilimia 15 ya kodi ya kuingiza sukari ya viwandani ambayo hurudishwa baada ya kuingiza mzigo na kufanyiwa uhakiki, fedha hii hairudishwi kwa wakati jambo linalosababisha kuwapunguzia mtaji.

“Kucheleweshwa kwa fedha hizo kumesababisha madeni kutoka viwanda vya Coca Cola ambayo inadai shilingi bilioni 5.5, Kiwanda cha Pepsi kinadai shilingi bilioni 8..4 na Bakhresa kinadai shilingi bilioni tisa,” alisema.

Alisema hali hiyo pia inatokana na taasisi za Serikali kutokuwa na uelewa mmoja katika kuhamasisha wawekezaji, wafanyabiashara na wenye viwanda na kusababisha usumbufu mkubwa na watu hao kuamua kufunga viwanda na biashara zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles