30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AVUNJA MFUKO CDTF

Na Mwandishi Wetu, Dodoma


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Kahawa (CDTF).

Vilevile amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza mwenendo wa mfuko huo tangu ulipoanzishwa.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana alipozungumza na wadau wa zao hilo kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya kahawa alichokiitisha mjini Dodoma.

Alichukua hatua hiyo baada ya kubaini uundwaji wa mfuko huo si wa sheria, bali ni wadau wa zao hilo kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

“Wakati Serikali inapambana kupunguza makato ya ovyo kwa wakulima kumbe huku kuna chombo cha kuwachukulia fedha wakulima hii haikubaliki,”alisema.

Pia aliagiza kufungwa ofisi za CDTF kupisha uchunguzi na baada ya CAG kukamilisha uchunguzi na kukabidhi ripoti.

Alisema  kazi zote zilizokuwa zinafanywa na mfuko huo zitafanywa na Bodi ya Kahawa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema  majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo yanaingiliana na yale ya Bodi ya Kahawa ambayo ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya zao hilo, hivyo hakuna haja ya kuwa vyombo viwili vinavyofanya kazi moja.

Wakati huo huo,  alipiga marufuku wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa wanavijiji  badala yake kahawa yote itauzwa kwa  minada.

“Kahawa itauzwa katika minada tu,utaratibu wa kutoa vibali kwa wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa wananchi vijijini ni marufuku kuanzia sasa.

“Kama kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi,”alisema.

Alisema wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie uuzwaji wa zao hilo na kuwachukulia hatua wote watakaokutwa wananunua kahawa kwa wakulima.

“Anayetaka kahawa akanunue mnadani na si kwa wanavijiji lengo ni kuhakikisha mkulima anapata tija,” alisema.

Pia ameziagiza halmashauri zote zinazolima kahawa nchini kuanzisha vitalu vya miche ya kahawa na  kuigawa bure kwa wakulima.

Alishauri maofisa kilimo wawaelimishe wakulima wote wenye miti mikongwe waanzishe mashamba mapya.

Kuhusu suala la utafiti wa zao hilo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo itumie vyuo vyake vya kilimo kuanzisha vituo vyake vya utafiti vitakavyofanya kazi ya utafiti wa zao hilo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Joseph Kakunda alisema  atahakikisha maagizo hayo yanafanyiwa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles