PUNDA HATARINI KUTOWEKA DUNIANI

0
4

LONDON: Uingereza

PUNDA  huenda wakatoweka duniani kutokana na mahitaji makubwa ya ngozi wa wanyama hao nchini China, ambako hutumika katika vyakula vya masuala ya afya na kutengenezea dawa za asili.

Habari zinasema nyama ya punda pia hupendwa kwa kiasi kikubwa nchini humo.

Kwa sababu hiyo hivi sasa   punda wamepungua kwa kiasi kikubwa China  na kwa sababu huzaa mara chache, hali hiyo imesababisha wafanyabiashara wa wanyama hao kuwatafuta katika  nchi nyingine duniani.

Habari zinasema bara la Afrika ndilo linaweza kukabiliwa na idadi kubwa ya punda ambao ni sehemu muhimu ya maisha ikizingatiwa hutumika katika uchukuzi wa mizigo na kilimo, hasa kwa familia maskini.

Kwa mujibu wa habari hizo, bei ya punda katika baadhi ya maeneo imeongezeka maradufu katika miaka michache iliyopita, huku mahali pengine wezi wakiwaiba na kuwauza.

“Siku moja nilipoamka sikumkuta punda wangu.  Nilipotafutatafuta nikamkuta amekufa, akiwa amechunwa ngozi,” alisema Anthony  Wanyama  (29) raia wa Kenya, hivi karibuni.

“Hivi sasa sina fedha za kutosha.  Sijalipa kodi ya nyumba, sijawalipia karo watoto wangu, na nina watu wanaonitegmea,” aliongeza Anthony huku machozi yakimlengalenga.

Kwa mujibu wa takwimu, idadi ya punda katika China imepungua kwa kiasi kikubwa kutoka milioni 11 mwaka 1990 hadi milioni tatu hivi sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here